mamayoyo1
JF-Expert Member
- Jul 25, 2018
- 1,011
- 1,019

Madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo kutoka Hospitali kuu ya jimbo la Shandong nchini China wanatarajia kuja nchini mwezi wa nane mwaka huu kwa ajili ya kufanya kambi maalum ya matibabu ya moyo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Makubaliano hayo yamefikiwa leo katika kikao cha pamoja cha viongozi kutoka Hospitali hiyo na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika kikao hicho Kiongozi wa msafara huo Wang Zhifeng alisema wataalamu hao ambao watakuja nchini watafanya upasuaji wa moyo wa kufungua na bila kufungua kifua pia watabadilishana ujuzi wa kazi na wenzao wa JKCI.
“Wataalamu wetu kutoka Hospitali ya Shandong wakija hapa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete watakuja na vifaa tiba ambavyo watavitumia katika upasuaji watakaoufanya. Pia mtatuambia ni vifaa gani vingine ambavyo mnavihitaji ili wataalamu wetu watakapokuja waje navyo”, alisema Zhifeng .
Aliendelea kusema kuwa kabla ya kuja kwa wataalamu hao hapa nchini kutaanza na program ya madaktari, wauguzi, wataalamu wa usingizi, mafundi sanifu wa moyo na Wahandisi wa vifaa tiba kwenda katika Hospitali hiyo kwa ajili ya mafunzo ya muda mfupi ya magonjwa ya moyo na mashine za moyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Prof. Mohamed Janabi aliwashukuru viongozi hao kwa kutembelea Taasisi hiyo na kusema kuwa kuja kwa wataalamu hao ni matokeo ya mkataba wa mahusiano uliosainiwa mwezi wa nane mwaka jana.
Makubaliano yaliyosainiwa katika mkataba huo ni kutolewa kwa mafunzo ya muda mfupi kwa madaktari, wauguzi, mafundi sanifu wa moyo na wahandisi wa vifaa tiba, kujenga jengo jipya la Taasisi hiyo, kutoa msaada wa vifaa tiba na kufanya kambi maalum za matibabu ya moyo ambazo zitasaidia kuwajengea uwezo wataalam wa hapa nchini.