WATAFITI 15 WA UDOM WANG'ARA TUZO ZA KITAIFA, WATAMBULIWA KWA UCHAPICHAJI WA TAFITI KIMATAIFA

University of Dodoma (UDOM)

Public Institution
Joined
Feb 24, 2024
Posts
50
Reaction score
55
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimeendelea kuimarisha nafasi yake katika utafiti wa kitaaluma baada ya watafiti wake 15 kutambuliwa katika Tuzo za Utafiti za Kitaifa kwa kuchapisha matokeo ya tafiti zao katika majarida yenye hadhi ya juu kimataifa.



Watafiti hao wa UDOM ni miongoni mwa washiriki 154 kutoka vyuo vikuu mbalimbali nchini walioshiriki katika tuzo hizo, hatua inayoakisi mchango unaoendelea wa Chuo katika kukuza utafiti, uchapishaji wa kitaaluma na uzalishaji wa maarifa yenye ushindani wa kimataifa.

Watafiti wa UDOM waliotambuliwa ni Prof. Godlisten G. Kombe, Dkt. Amos Luanda, Dkt. Asumin Selemani Kantinga, Dkt. Naima A.M. Hersi, Dkt. Salma Maneno Masawa, Dkt. Kelvin Ngongolo, Dkt. Marwa Emmanuel, Dkt. Mhuji Kilonzo, Dkt. Nyemaga Masanje Malima, Dkt. Ramadhani Bakari, Dkt. Emmanuel Mang’ombe, Dkt. Eric Mutegoa, Dkt. Joyce Elisadiki, Dkt. Mwumvaneza Moses na Dkt. Paul Majani Matao.



Vyeti vya pongezi kwa watafiti hao vimetolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, wakati wa hafla ya ufunguzi wa Maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yanayofanyika tarehe 18 Agosti, 2026 katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara, mkoani Tanga.

Akizungumzia mafanikio hayo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Prof. Lughano Kusiluka, amewapongeza watafiti hao kwa kukiwakilisha vyema Chuo na kuendelea kujenga taswira yake katika medani ya utafiti na uchapishaji wa kitaaluma.

Prof. Kusiluka pia amewahimiza watafiti wengine nchini kuendelea kufanya tafiti zenye ubora na matokeo chanya, hususan zile zinazoweza kutoa suluhisho kwa changamoto za jamii na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya Taifa.

Kutambuliwa kwa watafiti hao 15 kunaongeza ushahidi wa mchango wa UDOM katika kuibua na kuendeleza tafiti zenye ubora, kuchapisha matokeo katika majarida yenye hadhi ya juu kimataifa na kuzalisha maarifa yanayoweza kutumika katika kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii.



Mafanikio hayo pia yanaakisi umuhimu wa kuunganisha utafiti wa kitaaluma na mahitaji halisi ya maendeleo, ili maarifa yanayozalishwa katika vyuo vikuu yawe nyenzo ya kuleta mabadiliko katika sekta mbalimbali za uchumi na ustawi wa jamii.

Hafla hiyo imewakutanisha viongozi wa Serikali, wawakilishi wa taasisi za elimu, mafunzo na utafiti, watafiti, wabunifu pamoja na wadau mbalimbali wa sekta za elimu, sayansi, teknolojia na ubunifu.

UDOM inaendelea kuimarisha nafasi yake katika utafiti na ubunifu kwa kuhamasisha uzalishaji na usambazaji wa maarifa yenye tija, sambamba na dhamira ya kutumia taaluma na tafiti kuchangia maendeleo endelevu ya Taifa.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…