Bwana au Bibi Mgonjwa ametoa hoja zake kwa mujibu wa tafakuri na maono yake. Hapa chini nimejaribu kujibu baadhi ya hoja hizo kwa kutumia lugha nyepesi nay a uungwana ili angalau tuelimishane juu ya yale ya msingi hasa kwa wale wanokurupuka na kuizun gumzia hoja ambayo tayari ilikwishafanyiwa kazi na baadhi ya watu kwa takriban miaka 30 na ushee baadhi yao wakiwa wale wa Baraza la Kiswahili, Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili na Chuo Kikuu mlimani na wale waliokuwa katika MRADI WA KUKIWEKA KISWAHILI KATIKA PROGRAMU ZA MICROSOFT KATI YA MWAKA 2004-2006>
Matumizi ya Komp[yua [zawadi ya utandawazi] yalidhihirisha sanjari na kuwepo kwa programu za uundwaji Istilahi kwamba inawezekana kabisa kutafsiri SOMO LOLOTE lile katika Kiingereza na kuwa katika Kiswahili kwa kipindi kifupi mno kuliko mangimeza na viongozi wetu wanavyowazia.
Mgonjwa ameota hoja kubwa ya utandawazi na kile Watanzania wanachotakiwa kukifanya ili wajibu athari za utandawazi. Ila yeye katufanya Watanzania kama sisi tu ndio tunaotakiwa kujirahisisha lakini sio wengine. Hili sio sahihi. Na sisi tunacho cha kuringia na hasa pale tutakapokuwa tunafunsha kwa lugha yetu ya Kiswahili na kufanya utafiti kwa kutumia lugha hiyo hiyo WAGENI watataka UKARIBU MKUBWA ZAIDI nasi ili wafaidi siri na uhondo wetu mwingine uliojificha katika lugha yetu. KIwangu mimi ni kwamba: KISWAHILI HAKIKA MALI, ISIPOKUWA KWA ASIYE NA AKILI!
Nimejaribu kumjibu hoja moja baada ya moja, kwa kuchukua zile zisizojirudia au zisizo na uzito wowote wa kuzungumziwa kama ifuatavyo:
1. Kiswahili hakina umuhimu-
Kwa mantiki ya bwana au bibi huyu ni kwamba tunaweza kufuta kabisa Kiswahili na bado Tanzania ikaendelea kuwa kweli ni Tanzania na nchi ya Waafrika wanaojivunia utamaduni, heshima, utu na tofauti yao ndani ya wingi wa jamii mbalimbali katika medani ya jamii za kimataifa yenye kustaarabika na kuheshimika!
2. Jitihada za kukuza Kiswahili ni counterproductive
Ana maana toka Kiswahili kianze kutumiwa na serikali, shule za msingi hakuna faida yoyote iliyopatikana. Wasomi wale wale wa ukasuku wanaotokana na
Uinglishi wameendelea kuzalishwa na hakuna tofauti yoyote ya maana hapa nchini. Sijui kama statistiki zilizopo hazitaona aibu kumshuhudia.
3. Kiswahili kimetusaidia kupata uhuru na kujenga umoja wetu.
Baada ya kauli yake hiyo hapo juu kwamba jitihada za kuendeleza Kiswahili ni Counterproductive hii kwa hakika ni hoja ya kujinyonga mwenyewe. Maana anaki-dismiss kitu halafu anakiri kwamba huko nyuma tayari kilishakuwa na faida. Kifalsafa tunasema hii ni fallacy or reasoning.
4. Kiswahili kitakuwepo hadi mwisho wa dunia
Fallacy nyingine inakuja hapa anaposema kama hapo juu halafu anadai kitakuwepo bila kukuzwa wala kuendelezwa. Lugha sio kitu 'static' ni kitu hai kitu kinachokuzwa kutokana na matumizi na sio kwa kuundwa kwa idara au kampuni fulani kuiendeleza. Watanzania wanaokwaza leo katika kuanzisha shule za sekondari na vyuo vinavyotumia Kiswahili wanaweza kufanya hilo na msaada wanaohitaji ni hiyo ruhusa tu! Na bwana huyu au bibi huyu tutamuomba awe mgeni rasmi wakati wa mahafali ya kwanza ya Kidato cha IV, V na Chuo Kikuu na Mungu akimruhusu tutataka ashuhudie kwa macho yake mwenye kile kinachoweza kufanywa na Watanzania watakaokuwa wanalelewa kwa maziwa halisi ya mama yao na ambao si msukule bali watu wenye roho na akili zao huru na endelevu!
5. Ni lugha inayo 'link' makabila yote..
Mpaka hapa niseme tu hoja za mbishaji hazikinzani hata kidogo na hoja zangu bali zinaitia nguvu na ninamshangaa kwa kichwa cha habari chenye ujumbe tofauti na kile kilicho katika mada yake.
6. Leo kiswahili Tanzania hakihitaji shule, vitabu, wala,
Hili sina haja la kulizungumzia maana kuna wanaosema ukibishana na nani basi hakuna atakayeona tofauti....
7. kiswahili hakina msaada wowote katika mapambano
Hili linafurahisha maana nadhani bwana huyu au bibi huyu ni wale wasiofahamu kwa kina athari na majibu kwa utandawazi duniani. Kiswahili kina mchango mkubwa sana katika mapambano ya kimataifa. Kwani kiswahili sio tu anachodani ndicho kwacho bali kiswahili ni roho ya Watanzania. Na ukitoka nje bila roho yako tutakuita ;maiti' au sio? Kama kweli unaweza kutoka mwenyewe.
Au kwa lugha nyepesi Mgonjwa kweli anataka kutuambia kwamba unaweza kujenga nyumba ya biashara na heshima ya kimataifa bila msingi! Ajabu kweli, tena mchangani karibu na bahari alikouziwa Mmasai Kiwanja asubuhi na jioni kurudi ni bahari!!!!!!
8. Wenye upeo mdogo wa fikra mara nyingi wamekuwa wakilinganisha mchango wa lugha la kijapani, kikorea, kichina, nk katika maendeleo ya nchi husika.
Hivi kweli wale wenye upeo mdogo ni wale wanaotetea kiingereza kwa sababu ya kasumba za Kiingereza au Kifaransa au Kireno miongoni mwa baba na mama zoa ambazo kwazo nao wataka vilevile matoto yao yasomeshwe kwa lugha za nje wakiwa na imani mafaniko yao yatakuwa kama yao huku wakisahahu zama zinazobadilika. Na kwamba sasa ni wale wanasoma Kiarabu, Kihindi, Kirusi,
Kichina, Kikorea, Kujapani, Kihispania ndio wanaoukata na sio tena Kiingereza au kifaransa peke yake? Tulikotoka sipo tulipo na tulipo sipo tunapokwenda-fursa hazitwaliwi na wale wanaoishi katika ya jana bali kwa kutabiri ya kesho na keshokutwa!
9. kuimarika kwa lugha ni prerequisite ya maendeleo.
Umesema mwenyewe! Na ushahidi wa takwimu zote duniani zinaonesha kwamba walioimarisha lugha zao wenyewe sio sawa na Watanzania.
Pamoja na kuwa na wahandisi na madaktari waliofundishwa kwa lugha zote ila Kiswahili nchi haijapata Mtanzania wa kutengeneza pampu ya maji ili ile ya Ruvu ikiharibika iwe 'replaced' nayo; pasi Mgonjwa anayotumia haitengenezwi na Mtanzania; la kutisha zaidi sindano anayotumia kushona shati lake la mtumba iinatoka nje; na vingi vingine tu ambavyo kama biashara, menejimenti, uchumi na taaluma nyingine za uzalishaji mali na ujasiriamali zingelifundishwa kwa Kiswahili leo ingekuwa ni kitu cha kawaida kutengenezwa na Watanzania na kuuzwa ndani na nje ya nchi!
Na Mgonjwa Ukimwi atambue kuwa hakuna anayesema Kiingereza kife ili Kiswahili kistawi. La, hasha, tunazitaka lugha zote ziimarishwe na ukweli ni kwamba ikiimarisha Kiswahili Kiingereza Kitaimarika zaidi na sio vinginevyo. Na suala sasa litakuwa ni kuhusu lugha ya tatu, ne, tano na kadhalika kwamba iwe ni Kihausa au Kiarabu, Kichina au Kiafrikaans, Kihindi au Kizulu na kadhalika! Wenzetu wa Netherlands wameweza hili kiasi ambacho kila anayemaliza elimu ya sekondari anaweza kuandika na kuzungumza angalau lugha tatu kwa uchache!
10 Wanataka kutusahaulisha umuhimu wa wakati
Umuhimu wa wakati hapa mbona anaupitua- wakati sote tulikuwa kwenye dunia
ya tatu na India, Korea, China na kadhalika wakati wa uhuru vipi mbona wenzetu wametuacha papa hapa kama sio lugha zao kuwa 'the deciding factor' kwenye take-off zao?
Labda mwenzetu huyu hajafikia levo ya PhD. kwa hiyo katika mchanganyiko wake anadhani kwamba katika thesis moja unaweza kuuliza maswali yote na kushughulikia hypothesis zote. Rudi shule au endelea na shule upate mantiki ya unayoyazungumza.
Ukirejea nyuma hao Waingereza na Wafaransa unaowasema miaka kama 100 hivi iliyopita walikuwa wanaamini mtu hawezi kuelimika bila kutumia LUGHA YA KILATINI. Na wewe unataka kuturudisha huko huko kwa maono yako ukidhani kwamba Kiingereza, Kifaransa na Kireno haviwezi kufa kama kilivyokufa Kilatini? Lugha hufuata mkondo wa maendeleo ya kibiashara na kiuchumi na sio vinginevyo. Nadharia ya globalization na development zinakwambia kwamba ukiwa dhaifu kitamaduni na kilugha una hatari ya kufa na kutoweka kuliko wale walio imara katika utamaduni wao wenyewe sio wa kuiga na lugha yao wenyewe na sio lugha ya kuazima ambayo haisitiri matakao!
11. Hoja ni kwamba kuna factors nyingi sana (za ndani na nje) zilizosababisha maendeleo
Nakubaliana nawe moja kwa moja. Pengine ungelianza kuhoji pia matamshi kama vile ili tuendelee tunahitaji vitu vinne:
i. Watu [wa aina gani?]
ii. Ardhi [inayotumika kuzalisha kwa kutumia teknolojia gani?]
iii. Siasa safi [Ni ujamaa uliokufa kibudu au ni ubepari au ni demokrasia ya kijamaa?]
iv Uongozi bora [Ni ule unaoamini wakubwa kula ni haki, na wadogo kula
ni dhambi au ?]
Binafsi Mgonjwa Ukimwi mimi ninaamini kwamba ili tuendelee kama taifa hapa Afrika tunahitaji vitu vifuatavyo:
i. Watu wanaoelimishwa kwa kuzingatia mazingira, utamaduni na lugha yao ya asili
ii. Kutoamini kwamba nchi tajiri au kwa kutumia vitu fulani vya nchi tajiri basi na sisi tunaweza kuukata. Maana sijaona hata ndugu yangu mmoja ambao ni matajiri wa kutisha akigeuka na kusema aninyanyue mimi ndugu yake damu damu ndio itakuja kuwa watu baki?
iii. Kuiga jinsi baadhi ya mawaziri wetu na makatibu wao wakuu walivyoanza kuwapeleka watoto wao kusoma Uchina na sio Uingereza au Marekani/
iv. Kuipa mikoa ruksa ya kuendeleza shughuli zao za kiuchumi na kijamii wao wenyewe bila kuingiliwa ila kwa sababu za msingi katika maendeleo yao. Hii ikiwa ni pamoja na kutafuta wafadhili na wawekezaji toka nje.
v. Mawaziri wapatiwe malengo na performance contact ili kazi wanayotumwa kufanya ijulikane na utendaji kazi wao upimike kila baada ya miezi 6 au mwaka mmoja.
vi. TBS waanzishe na kutekeleza programu kabambe ya kuhakikisha viwango vya huduma na sekta ya ukarimu vinaandaliwa na hoteli na mabaa yote hata ya Uswahilini yanafikia kiwango hicho ili Wajapani, Warussi, Wachina na wazungu wasione kinyaa hata kidogo kuingia huko na kustarehe! Kwa maneno mengine usafi na huduma bora kwenye vijiji na miji ya Tanzania kunaweza kututajirisha kama Ubelgiji inavyofaidika na utalii kutokana na sifa hizo.
vii. Dhahabu na madini yote yanayozalishwa hapa nchini yanadiwe hapa hapa Kariakoo na sio kwingineko.
viii. Mradi wa Magari ya Nyati ugeuzwe mradi wa kutengeneza au japo kuassemble matrekta makubwa kwa madogo kwa ajili ya kukibadilisha kabisa kilimo cha nchi hii. Ikiwezekan nusu ya hela za EPA ziende huko.
ix. Vituo vyote vya mipakani [Border posting] vigeuzwe miradi mikuu ya kiuchumi na nchi jirani kwa kurushusu wawekezaji kushirikiana na serikali ili vituo hivyo viwe kama vile Uwanja wa Ndege wa Dubai lakini huu sasa ni uwanja wa magari na waendao kwa barabara ili biashara kubwa ifanyike huko kwa faida ya masikini wa Tanzania. Biashara na nchi jirani ndio uti wa mgongo wa uchumi wa
taifa hili na tusidanganyane kuwa ni kilimo
x. ATC iache biashara ya ndege za abiria kwa watu bianfsi nayo iingilie madege makubwa ya uchukuzi wa shehena za kibiashara zitakazofikishwa kwenye maeneo ya mipakani kwa ajili ya kununuliwa na wafanyabiashara wa nchi jiriani na hivyo kuwa na IMPORT AND RE-EXPORT business ya haja.
xi. Mahospiali kadhaa yaongezwe ubora na hasa vifaa vya kisasa na hata madakatari kutoka nje ili tuchume fedha za kigeni kwa kutibu mawaziri wetu na wale wa nchi jirani hapa hapa Tanzania.
xii. Baadhi ya wawekezaji kwenye sekta ya elimu wahimizwe kuboresha huduma zao ili shule za msingi ziwe na wanafunzi 100,000 kutoka Kenya,Rwanda, Malawi, Zambia, Kongo, Burundi na kadhalika. Na vivyo hivyo shule za sekondari ziwe na wanafunzi 50,000 wa nje wakati vyuo visiwe na chini ya wanafunzi 20,000 wa nje. Fedha hizo zizungushwe kuongeza fursa za kielimu na kimafunzo kwa Watanzania.
Shule hizo ziendelee kutumia Kiingereza kumfurahisha mgonjwa wa ukimwi lakini mapato yake yatumike kuendeleza shule na vyuo vya Watanzania vinavyotumia kiswahili toka msingi hadi chuo kikuu!
12. utandawazi unatutaka tuachane na nationalistic policies na tufungue mipaka yetu (including mipaka ya kitamaduni na kifikra).
Wenzangu mnamuelewa Mgonjwa katika hili. Mimi simuelewi. Labda akishapona kama atapona!
13. Athari za utandawazi tunaweza kuzitumia kwa faida endapo tutajifunza lugha za kimataifa.
Hii ni hoja yangu pia ya msingi. Kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya kufundishia
kutatulazimisha pia kuwafunza wakina HUba-Kiarabu, Kiingereza, Kichina, Kijapani, KIhindi, Kikorea na kadhalika ili wakina Migiro waongezeke lukuki. Angalia hapo juu pia!Matokeo yatakuwa tofauti na hivi sasa ambapo wadogo zake au watoto wa mgonjwa wanalazimishwa kukremu na kisha kudub au kutepu Chemistry, Physics, Biology, Mathematics, Accounting, Manafgement, Economics bila kuweka chochote cha maana kwenye bongo asili yao ya kisha ukiandika kitu kidogo kwa Kiingereza ukakiweka kwa Internet tayari mzungu Uingereza au Marekani au Australia au Canada anakidaka na kukikuza kuwa kitabu na kukiuuza na hulipwi chochote kwa mchango wako na kwao hili sio plagiarism maana wewe ndiye uliyeiba lugha yao!
14. Utandawazi unaleta free-movement of capital and labour
Sawa. Na utandawazi huo kama nilivyoonesha hapo juu pia UNAIBA KUSHOTO NA KULIA vitu kadhaa kwa sababu elimu ya Geology ambayo inawezekana kabisa kuandaliwa vitabu vyake ndani ya mwaka mmoja tu waulize wazee wa TAASISI YA UCHUNGUZI wa Kiswahili kina Mwesiga, Mulokozi na maprofesa kama Madumula, Kahigi na kadhalika watakwambia hilo- Barrick wasingeona ndani Tanzania. Tumepuuza Kiswahili sasa tunaibiwa sasa tunalia nini?????
15. tutang'ang'ania kufundisha future labour force yetu kiswahili.
Kwa kweli ndugu hapa umechemsha tena ya kutokota! Kwani sasa hivi wanatumia lugha gani? Wewe hujamuona Mwalimu wake Huba nini? Sasa ili walimu na wafanyakazi wengine wafanye kazi yao kufundisha au kutimiza kile wanachotaka bila kukwamishwa na lugha Kiswahili hata ukipinge hadi kaburini utasikia kinakuimbia funeral dirge na huku kikiendelea kutesa. KIswahili hujaambiwa ndugu yangu: " TITI LA MAMA TAMU, LINGINE HALIISHI HAMU ?"
Tafadhali ubalozi wa Japani, INdia, Uchina, Korea Kusini, Uarabuni/UAE , Norway, Denmark, Sweden na kadhalika mpeni Mgonjwa kabla hajaondoka fursa ya kwenda kuibadili kauli yake huko majuu kwa majuu. Maana hapa anazungumza asichokiexperience wallahi vile! Ukizungumza lugha yako ndugu unatesa, ukiitumia lugha yakjo kibiashara uannyanyasa; na ukiitumia kujifunza UNAUUUA!
16. kufundisha kiswahili katika levels zote nikufanya maisha ya watanzania yawe magumu mara kadhaa.
Hoja hii inapwaya. Kwa sababu tatizo hapa sio lugha ila QUALITY -mnajenga madarasa na mashule na walimu mnawajengaje? Ndio swali la kuulizwa! Na haiwezekani kuendelea na bisahara njaa ya mtu kulipwa kisichomtosha hata wiki moja kama mshahara wa mwezi mzima umtarajie mtu huyu atakuwa na moto na ari ya kumuelimisha mtu mwingine. Kama ulivyosema mwenyewe, kwa maneno mengine Kiingereza sio kitu pekee kinachoweza kuleta maendeleo ya mtu kuna
factors kaba kaba za kuangalia.
Kwa taarifa yako hivi sasa huko Uchina kuna wachina wapatao milioni 200 [narudia milioni mia mbili na ushee] amabo wanajua Kiingereza simply sio kwa sababu ya kuwapikia au kuwauzia vitu wazungu bali kwa saabu ya kuonesha tu kwamba wao sio nani hii na wakitaka kitu kinafanyika. Kwa hiyo usitukalishe mkao wa kuliwa tukalishe mkao wa kula. TBC ya China ilifanya hivyo, yaani, kufundisha wachina 200 milioni chini ya miezi sita kiiingereza safi, je TBC, yenu muhimu ni matangazo ya mpira wa mguu na ule mpira mwingine tu?
17. wachezaji wa mpira hawafundishiki kwasababu ya lugha
Je, mwalimu angelijua Kiswahili ingelikuwaje. Mbona unataka wewe kutuuza sisi tu lakini sisi tusinunue wengine.Tuseme kwamba Kikwete anahakikisha kuwa Wachezaji wote wanafunshwa Kiingereza cha mama ndio waingie Taifa stars. Kocha mwenyewe kumbuka
Mbrazil kwa hiyo lazima naye asome Kiingereza toka kwenye Kireno chake halafu ndio wakutane katikati. Sasa unatuambia papo hapo tutafanya maajabu. Mimi siamini kwamba tumekuwa vinyozi. Bali tumeacha tu kunyolewa. Na majinwele kama kichaka sasa yatisha wallahi vile!Mafanikio yataka utamaduni bwana na utamaduni uko kwenye lugha na sio teknolojia laini au ngumu. Sijui kama unanielewa Mgonjwa wangu?
18. mahoteli yetu ya kitalii yanashindwa kuajiri wafanyakazi wa bei nafuu wa vijijini kwa sababu ya lugha.
Msanifuni jamaa anayokazania kutuuza kwa bei sawa na bure wallahi. Mwambieni nchi zenye biashara kubwa ya Utalii wahudumu wake wachache sana wanajua Kiingereza na sio hivyo kama anavyodhania yeye. Kazi hapa kama alivyosema mwenyewe factors zingine baba wee au mama weee!
19. nasikitika kwamba wanaokuwa mstari wa mbele kukikumbatia
kiswahili ni watu kama mimi ambao tayari tuna angalau uelewa mdogo wa lugha
nyingine.Na kwa sababu hii anataka wengine nao baada yake waendelee kuwa na uelewa mdogo wa kila kitu au kama mwenyewe vile ambavyo angeliiweka : 'Jack of all rades but master of none!' Kweli kuna elimu zinazotaka Kiingereza na lugha nyingne kama Kiarabu cha kwendea Dubai na kadhalika lakini kwa wale wasiolazimika kuhitaji lugha ngeni katika kazi zao kwanini tuwalazimishe kusoma kwa lugha za Kigeni? Mwandishi wa gazeti la Kiswahili au Redio au TV kama vituo vyake ni vya Uswahilini tu mwachie asome kwa Kiswahili. Kama anatoka nje ya mipaka asome na Kiarabu ili aende Misiri na sio Kiingereza au asome Kifaransa kama anaenda Madagascar au Kireno kama anaenda Msumbiji. Hii ndio sawa, hivi ndivyo ipasavyo kuwa soma ukatumie, sio soma usahau!!
20. Hitimisho
Mawazo ya mwenzetu ndio hayo. Yeye anaamini Kiswahili kama jongoo kinaweza kwenda chenyewe tu. Kikitumbukia kwenye maji haya. Kikiingia kwenye moto haya.Lakini la ajabu ni imani yake ilivyo ya rohoya paka eti KISWAHILI HAKIWEZI KAMWE KUFA!
Hii inapingana na nadharia ya mifumo na tabia zake duniani. Mwalimu wangu katika levo ya Masters aliniambia kwamba chochote hai ili kiendelee kuwa HAI lazima kiingize, kichakache na kisha kitoe. Sasa hapa nimekanganyikiwa maana Mgonjwa ananiambia tena kwa maneno mazito kwamba Kiswahili kitaendelea tu kuwepo hata kama hakiingizi labda kwa nguvu za miujiza fulani lakini sio kwa sayansi niliyoisoma na ninayoijua!
Pili, tatizo la kuwa na nafasi isiyotumika kama ilivyo hadithi ya mikono isiyo na kazi ni kukaribisha vishawishi vingi kwa Watanzania na Waafrika. Ninaamini tena sana kwamba Kiswahili kingelikubalika kwenye nchi zenye migogoro Afrika leo nchi hizo zingelikuwa na umoja na amani kama tulio nao Watanzania.
Kwanini basi tuwe na choyo ya Kiswahili kuendelezwa ili kuwanusuru wenzetu wa Afrika ya Kati, Burundi,Comoro, Rwanda, Kongo hadi kazi hiyo tunaawachia BBC?
Yeyote anayekataa Kiswahili kuchukua nafasi yake inayostahili katika Taifa hili sio tu anataka Tanzania pale ilipobakia toka mwaka 1970 bali anadhani majibu ya utandawazi yatatokana na kuukabili utandawazi huko majuu na sio humu humu ndani kwetu.