SoC02 Watanzania tunakwama hapa

SoC02 Watanzania tunakwama hapa

Stories of Change - 2022 Competition

mwanzajo

Member
Joined
Jun 11, 2016
Posts
19
Reaction score
3
UTANGULIZI
Tanzania ni miongoni mwa nchi nyingi zilizoko kusini mwa Jangwa la Sahara ambazo zimepiga hatua kubwa katika suala la utoaji wa elimu kwa watu wake. Kwa miaka ya hivi karibuni, tumeshubudia mabilioni ya fedha yakiwekezwa kwenye sekta ya elimu ambapo tumeona ongezeko kubwa la shule,vyuo pamoja na kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi na wanachuo mfululizo.

Vilevile, kumefanyika maboresho ya kisekta kwenye mitaala ya elimu hususani shule za msingi, sekondari, vyuo pamoja na vyuo vya ufundi ili kuweza kuwanufaisha WATANZANIA kielimu, kiuchumi na kijamaa pia.

Pamoja na uwekezaji huu mkubwa kwenye sekta ya elimu nchini, bado WATANZANIA walio wengi wanakosa maarifa mahsusi, ujuzi pamoja na stadi za kazi jambo ambalo huwafanya washindwe kufanya vizuri kwenye hatua mbalimbali za kuomba kazi au kufanya kazi husika. Tafiti zinaonyesha kuwa ,kuna tofauti kubwa sana kati ya wasomi wanaotegemewa na WAAJIRI na wale wasomi wanaozalishwa toka VYUONI.

Mwaka 2015, Rais mstaafu wa Tanzania, muheshimiwa Dr. Jakaya Kikwete aliweka bayana kuwa, wasomi wengi wa kitanzania HAWAAJIRIKI kwa sababu hawana maarifa na ujuzi wa kazi unaohitajika kwenye soko la ajira la ndani na nje ya nchi yetu (Business times,September, 2015).

Andiko langu ,linaangazia sababu mbalimbali zinazofanya WATANZANIA wengi kukwama au kushindwa kwenye mashindano mbalimbali ya kutafuta kazi au kufanya kazi. Zifuatazo ni baadhi tu (siyo zote) ya sababu ambazo nimeona zinasababaisha WATANZANIA wengi kukwama kupata ajira pindi wanaposhindanishwa na waombaji wengine ama ndani au nje ya nchi:

Mosi: Barua za maombi ya kazi; WATANZANIA wengi hawana kabisa weledi wa kuandaa barua nzuri za kuombea kazi. Wengi wao huandikiwa na marafiki zao na wengine huandaa barua ambazo hazina sifa wala ubora unaotakiwa na wa ajiri hivyo kuwafanya waondolewe kwenye mchakato wa usaili mapema sana.

Pili: Wasifu binafsi wa mwombaji(CVs); Kama ilivyo kwa upande wa barua za kuombea kazi, pia kuna tatizo kubwa sana kwa wasomi wetu kuandaa CVs zenye kuonyesha ubora na ufanisi wa kazi mbalimbali ambazo mwombaji alishafanya. Wengi wao huandaa CVs ambazo hazieleweki wala hazina mpangilio wa kitaalam kama inavyotakiwa.

Tatu: Ukosefu wa ujuzi wa kutosha na maarifa toshelezi. Ndiyo, WATANZANIA wengi wamesoma. Wengine wana digrii moja, wengine mbili, wengine tatu wengine zaidi ya hapo. Lakini baadhi ya wasomi hawa wanakosa maarifa na ujuzi sahihi wa vitu walivyosomea. Wengi wao hushindwa kabisa kujibu maswali yanayohusiana na taaluma zao walizosomea.

Nne: Uwezo mdogo wa kuongea na kuandika Kiingereza. Lugha ya Kiingereza imekuwa ni tatizo kubwa sana kwa WATANZANIA, si kwa wasomi wachanga au waliobobea wanaoweza kuimudu lugha hii ipasavyo. Kutokujua lugha hii kwa ufasaha, huwafanya wasomi wa kitanzania kukosa namna ya kujieleza vizuri hivyo hushindwa kujiamini wawapo kwenye ushindani na pia hushindwa kuelezea vizuri wanapopewa mitihani ya kuandika.

Tano: Uelewa mdogo wa mambo mbalimbali (General Knowledge): Achilia mbali digrii na ujuzi walio nao, WATANZANIA wengi hawajui mambo mengi nje ya taaluma zao. Mara nyingi kwenye nafasi zenye ushindani huwa kuna maswali ambayo yako nje ya kazi inayoshindaniwa, WATANZANIA wengi huwa wanakwama hapa maana wamebobea tu kwenye vitu vyao walivyovisomea.

Sita. Uelewa mdogo kuhusu shirika au kampuni ulikotuma barua ya maombi ya kazi; Ni muhimu sana kuwa na taarifa au dondoo za kampuni au shirika linaloenda kukufanyia usaili. WATANZANIA wengi siyo watafiti kwa asili, wengi wao huenda kwenye usaili bila kuwa na historia fupi ya aidha shirika au kampuni husika hii huwafanya wapoteze alama pindi waulizwapo maswali kuhusu kazi au bidhaa zitolewazo na wa ajiri tarajiwa.

Saba: Maandalizi duni kabla ya kuomba kazi: Kama ilivyo ada, ili ufaulu mtihani vizuri sharti ujiandae vizuri kwa kusoma na kufanya maswali mbalimbali. Hivyohivyo, ili ufaulu usaili fulani ni lazima ujiandae kujibu vizuri maswali yao kabla ya kufanya usaili. WATANZANIA wengi hawafanyi hivyo, wengi wao wanakurupuka tu na kukimbilia kwenda kufanya usaili. Lazima ujiandae maana kuna usaili wa aina mbalimbali. WATANZANIA wengi wanakwama hapa pia.

MAPENDEKEZO:
Baada ya uchambuzi huu wa kitaalam naomba kupendekeza mambo yafuatayo ambayo yakifanyika kwa ufasaha, yatawasaidia WATANZANIA wengi kwa kiasi kikubwa sana.

Moja: pamoja na serikali kuwekeza sana kwenye elimu pamoja na miundo mbinu yake, ni wakati sasa serikali yetu iwekeze zaidi kwenye uandaaji wa walimu bora na wataalamu wengine wanaoandaa wataalamu wapya. Elimu ya nadharia iwe tu asilimia 20 na asilimia 80 iwe ni elimu vitendo kwa ngazi zote za elimu hapa nchini.

Mbili: Kuwepo na lugha moja maalumu ya kufundishia. Kwa sasa taifa limepotea. Sera ya elimu imeweka bayana kuwa kwa ngazi ya sekondari na vyuo lugha ya kufundishia ni Kiingereza. Lakini wapi! Ukienda huko ni kiswahili tu! Mnasoma kwa kiswahili lakini notisi mnaandika kwa Kiingereza. Hatari sana hii! Kwa mtindo huu ni ngumu sana kupata wasomi wanaoweza kujieleza kwa ufasaha kwa lugha ya kigeni.

Tatu: Vyuo vikuu, vyuo vya kati pamoja na mabaraza ya kazi waandae warsha au makongamano mengi ya mara kwa mara ili kuwanoa wahitimu wapya kabla hawajaingia kwenye soko la ajira.

NNE: WATANZANIA wajenge tabia ya kujisomea; Watanzania wengi hawapendi kujisomea ili kupata maarifa mengine mapya. Wengi wetu tulisoma tu kwa ajili ya mitihani ya shule au vyuo, baada ya hapo hakuna tena kujisomea kwa ajili ya maarifa mengine au mapya. Kujisomea husaidi mtu kuongeza thamani ya maarifa aliyokuwa nayo.

Tano: WATANZANIA wajenge tabia ya kujutolea kufanya kazi bure au kwa ujira mdogo kwenye kampuni au mashirika makubwa ili kuweza kupata maarifa, ujuzi na stadi mpya za kazi ambazo hazikufundishwa chuoni au shuleni.

HITIMISHO
Natoa rai kwa wasomi wetu, vijana kwa wazee kwamba jukumu la kuwa Bora au kuwa mtumishi Bora ni la kwako binafsi na si mtu mwingine. Kila mtu anaouwezo wa kuwa mtu Bora pale anaposhindanishwa na mtu mwingine. Pamoja na kuwa serikali imeshindwa kutuandaa kuwa Bora sana, basi tujione kuwa tunalojukumu kubwa la kufanya kama kweli tunataka kuwa Bora na imara mbele ya mataifa mengine. Kila msomi chipukizi au mbobezi ajiangalie na kujifanyia tathimini yeye mwenyewe ili awezegundua madhaifu yake na ambayo ataweza kuyafanyia marekebisho kwa maslahi mapana ya nchi yake. Kweli WATANZANIA tubadilike!
 
Upvote 0
Back
Top Bottom