Watanzania tutafaidika vipi na uwekezaji wa gesi asilia?

Sword

JF-Expert Member
Joined
Apr 15, 2013
Posts
864
Reaction score
183
Jamani kiukweli kuwekeza kwenye gesi sio lelemama, inahitajika fedha ya kutosha, ni ghali mno. Sielewi mifuko ya watanzania iko vipi lakini mimi nahisi gharama yake ni kubwa sana ni vyema serikali ikawa makini tu hapa ili kuhakikisha sisi watanzania tunafaidika kwa namna moja ama nyingine mathalan kuwekwe sheria makhsus ambayo itatulinda na kuhakikisha tunafaidika pia suala la Corporate Social Responsibility (Uwajibikaji kwa jamii) iwe ni sheria. Ninamaanisha kwamba kabla muwekezaji hajakubaliwa obli lake la kuwekeza aainishe ni nini atafanya kwa watanzania hususan kwa maeneo ambayo uwekezaji unapatikana.

Uwajibikaji ambao ninamaanisha hapa ikiwa ni pamoja na kujenga shule na sio mradi shule lakini naongelea shule ambayo inaenda sambamba na faida inayopatikana, pia kuna suala la barabara, kuhakikisha barabara zinakuwa ni za maana, pia suala la hospitali, kujengwe hospitali na pia vifaa vipatikane vya kisasa.

Mbali na hayo lakini pia muwekezaji huyo kabla ya kuwajibika kwa jamii pia awasiliane na jamii husika kwa kufanya mikutano ama kwa namna nyingine ili kuelewa eneo husika linahitaji kitu gani yani kipaumbele kwa eneo hilo ni nini na akishafahamu basi ndio anawajibika kwa jamii kulingana na mahitaji ambayo yameorodheswhwa na jamii hiyo kwa wakati huo.

Pia uwajibikaji huu hautakiwi ukawa ni wa mara moja inapaswa kuwa ni zoezi endelevu kulingana na vipaumbele hivyo ambavyo wananchi wameorodhesha, kama tatizo ni maji basi yampasa muwekezaji kuhakikisha wananchi wa eneo husika wanakuwa na maji ya kutosha kwa kuanzisha vyanzo ambavyo ni vyakudumu ili hata muda wake utakapokwisha basi faida hii inaendelea kuwepo.

Kwa upande wa serikali inawajibika kuhakikisha inasimamia zoezi hilo kikamilifu huku ikishirikiana na wananchi wa eneo husika. Halmashauri za maeneo husika zinawajibika sana katika mchakato huu.

Hiyo ni uwajibikaji kwa jamii, sasa mbali na hiyo ambayo inawafaidisha wananchi wa maeneo husika tutazame upande mwingine, hususan katika suala la kodi, hapa pia serikali ianishe mapema mchakato wake wa tozo mbalimbali ambazo huyu muwekezaji anapaswa kulipa.

Suala lingine ambalo ninaamini ni muhimu sana ni suala la uwazi, kusiwepo na siri yoyote, wananchi wanapaswa kueleweshwa namna huyo muwekezaji amepatikana ikiwa ni pamoja na mkataba alioingia na serikali ili walau sisi wananchi tuelewe ni vipi muwekezaji amepatikana na ni vipi makubaliano yake na serikali yalivyo ili kukitokea la kutokea basi pia sisi tunakuwa na uelewa mpana zaidi na huenda tukawa na uwezo wa kuishauri serikali juu ya nini kifanyike.

Suala lingine ambalo binafsi naona linaumuhimu ni serikali kuingia ubia, maana serikali kama serikali kwa suala la gesi ninaamini haiwezi vinginevyo kuwepo na PPP (Public-Private-Partnership).

La mwisho kabisa kuwepo na uzalendo katika usimamizi wa haya yote niliyoyaeleza pia maarifa muhimu mathalani wasomi waliobobea katika uchumi hususan uchumi wa gesi watumike hapa. Pia wanahabari hapa wanaumuhimu sana, maana huenda kukawa na ugumu wa kuwasiliana na kila mtanzania yani 'ana kwa ana' (one to one) basi hapa wanahabari watumike kutuelewesha yani wawe ni link kuu baina ya serikali na sisi wananchi.

Kuhusu wanahabari, ushauri wangu kwao ni kuweka maslahi ya taifa kwanza, yani hata kama chombo ni cha mtu binafsi nae ni mtanzania basi ni vyema akaweka utanzania wake mbele na kuhakikisha hakuna upotoshaji, aripoti hivyo hivyo kama serikali inavyosema na pia anweza kutoa maoni yake kama ni kwa gazeti iwe ni sehemu ya maoni ama makala na si sehemu ya habari ili sisi wananchi tuelewe haya ni maoni ambapo na sisi pia tunaweza kutoa hayo maoni kutokana na kusoma habari ambayo inakuwa haijachakachuliwa.

Mungu Ibariki Tanzania
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…