Watetezi TV yapigwa faini ya Tsh. Milioni 3 kwa kosa la kutomiliki na kutochapisha sera na mwongozo kwa watumiaji

Watetezi TV yapigwa faini ya Tsh. Milioni 3 kwa kosa la kutomiliki na kutochapisha sera na mwongozo kwa watumiaji

Influenza

JF-Expert Member
Joined
Jul 1, 2018
Posts
1,509
Reaction score
3,756
Baraza la ushindani wa kibiashara (FTC) jijini Dar es Salaam limeihukumu televisheni ya Watetezi inayotoa maudhui yake kwa njia ya mtandao (Online TV) adhabu ya shilingi milioni 3 kwa kosa la kutokuwa,na kutochapisha sera na mwongozo kwa watumiaji (Online Policy) jambo linalodaiwa kuwa kinyume na kanuni za mawasiliano ya kielektroniki na posta (Maudhui ya mtandaoni) ya mwaka 2018.

Mwezi September mwaka jana,Mamlaka ya mawasiliano Tanzania (TCRA) ilitoa adhabu ya shilingi milioni 5 kwa Watetezi TV kwa kosa la kutokuwa na mwongozo wala sera kwa watumiaji ambapo Watetezi Tv haikuridhishwa na maamuzi hayo na kupelekea kukata rufaa kwenda baraza la ushindani wa kibiashara lililofikia maamuzi hayo leo May 4.

=====

FCT YABADILISHA UAMUZI KATIKA KESI YA TCRA DHIDI YA WATETEZI TV- TCRA HAINA MAMLAKA YA KUTOZA FAINI

Baraza la Ushindani (FCT) limetoa uamuzi wake kwenye rufaa iliyokatwa na Watetezi TV mnamo Septemba 27, 2019, dhidi ya Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania.

Baraza la Ushindani (FCT) limeamua kuwa Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TRCRA) haina mamlaka ya kutoza faini chini ya Kanuni ya 18 ya Kanuni za Mawasiliano ya Kieletroniki na Posta (Maudhui ya Mtandaoni), 2018.

Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania iliwatoza Watetezi TV faini ya Shillingi Millioni Tano za Kitanzania (Tsh 5,000, 000) kwa kutokuweka sera au mwongozo wa watumiaji kinyume na Kanuni ya 5(1)(c) ya Kanuni za Mawasiliano ya Kieletroniki na Posta (Maudhui ya Mtandaoni), 2018.
Kamati ya Maudhui ya TCRA klifikia uamuzi huo kulingana na Kanuni ya 18 ya Kanuni za Mawasiliano ya Kieletroniki na Posta (Maudhui ya Mtandaoni), 2018.

Watetezi TV haikuridhika na uamuzi huo na hivyo wakakata rufaa mbele ya Baraza la Ushindani kwa sababu tatu;

Mosi, kwamba kamati ya Maudhui ilikosea kisheria kwa kutumia kifungu kisichosahihi kufikia uamuzi wake.

Pili, kwamba Kamati ya Maudhui ilitenda bila kuwa na mamlaka.

Tatu, kwamba kamati ilikosea kisheria kwa kushitaki chombo kisichokuwepo.

Dr. Mwenegoha, mwanachama wa Baraza akisoma uamuzi, alikubaliana na sababu ya kwanza ya rufaa kwamba kamati ya Maudhui ilikosea kisheria kwa kutumia kifungu kisichosahihi kufikia uamuzi wake. Kwani Kanuni ya 18 haitoi mamlaka kwa mamlaka kama Kamati ya maudhui kutoza faini. Hivyo, ilikuwa kosa kwa Kamati hiyo kuwatoza faini kulingana na Kanuni ya 18 kwasababu Kanuni hiyo inatumika pale wamekutwa na hatia. Mamlaka ya kumtia mtu hatiani ipo ni ya Mahakama pekee yake. Hivyo kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano haina mamlaka ya kumtia mtu hatiani.

Hata hivyo, Dr. Mwenegoha alisema kuwa Watetezi TV kwa Wakati huo ilikuwa imekiuka Kanuni ya 5(1)(c) ya Kanuni za Mawasiliano ya Kieletroniki na Posta (Maudhui ya Mtandaoni), 2018 kwa kushindwa kufanya sera au mwongozo upatikane na watumiaji.

Hivyo, Baraza limefikia uamuzi wa kuweka kando uamuzi uliotolewa na Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano na kubadilisha adhabu kuwa kulipa faini ya shilingi Millioni Tatu (3,000,000) chini ya kifungu cha 44(2)(b) cha Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano.

Sababu nyingine mbili za rufaa zilikubaliwa kwa sehemu na kukataliwa kwa sehemu.

Mnamo, September 25, 2019 Watetezi TV iliitwa na kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania kujibu juu ya shitaka la kutokuweka sera au mwongozo wa watumiaji wa mitandaoni kwenye mitandao yao ya kijamii kinyume na Kanuni ya 5(1)(c) ya Kanuni za Mawasiliano ya Kieletroniki na Posta ( Maudhui ya Mtandaoni), 2018.

Kanuni ya 5(1)(c) inasema kuwa “Mtoa Maudhui ya mtandaoni atakuwa na jukumu la kutengeneza sera au mwongozo wa mtandaoni na kuufanya upatikane kwa watumiaji.”

Uamuzi uliotolewa na Baraza siku ya leo umeangaza kuwa Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania imeitoza Watetezi TV faini kubwa kinyume na sheria.

Baraza limeeleza kuwa kifungu sahihi cha Sheria lilichopaswa kutumika ni kifungu cha 44(2)(b) cha Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania. Hata hivyo kifungu cha 44 pia kinakosa viungo muhimu vya kuzingatiwa kabla ya kutoza faini.

Uamuzi uliotolewa na baraza leo Katika rufaa ya Watetezi TV imeangaza waendeshaji wa vyombo vya Habari vya Mtandaoni kutetea Haki zao. Poa imejulisha Umma kuwa Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania haina mamlaka ya kutoza faini kulingana na Kanuni ya 18.

Hivyo, faini yoyote iliyotozwa na Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasilano Tanzania haikuwa sahihi kulingana na Kanuni ya 18 na hivyo inapaswa kupingwa mbele ya mamlaka husika kama Baraza la Ushindani.

Zaidi ya hayo, uamuzi wa Baraza umeamsha watunga sheria kufanya mabadiliko husika kwenye Kanuni za Mawasiliano ya Kieletroniki na Posta(Maudhui ya Mtandaoni), 2018.

Kufuatia uamuzi huu wa Baraza, Mtandao utapitia uamuzi uliotolewa ili kujiandaa na kupeleka rufaa kwenye Mahakama ya Rufaa au la.

Mawakili waliosimama badala ya Watetezi TV kwenye rufaa hii mbele ya Baraza la Ushindani ni; Benedict Ishabakaki, Bertha Nanyaro na Rayson Elijah Luka kutoka Kampuni la Mwakili la Victory Attorneys& Consultants .

Imetolewa na;
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC)
4th May 2020.
Dar es Salaam, Tanzania
 
Back
Top Bottom