WUkisoma maandiko ya Mohamed Said, references zake ni za akina SYKES na wakina DOSSA mainly. Hivi Leo ukimuuliza atakwambia wazee walioijua TANU kwa kina ni wazee wa kiislam na wote hawapo, wametangulia mbele ya haki!!
Mohamed ukimchungaza utaona kuwa ni very selective katika watu aliowahoji kuhusu TANU nao wengi ni wa dini yake hakupoteza muda kuwahoji wazee waanzilishi ambao wengine wapo ambao sio waislamu!!
Hakupoteza muda kwenda kukaa na Mzee Job Lusinde kabla ya kifo chake bali alipata muda kuongea na ALLY Sykes!! Kuna watu ambao wako hai ambao angeweza, kama angeta kupata unbiased story kuhusu TANU lakini kwa vile hawakidhi matakwa yake hawezi kufanya hivyo!
Mohamed mtafute Katibu mwenezi wa kwanza wa Chama Cha TANU anaitwa ROWLAND MWANJISI ili akurekebishie mapungufu yako kwenye historia unayojaribu kuitengeneza. Huyu Mzee yuko hai somewhere in Tanzania.
Bulesi,
Hakika umesema kweli rejea zangu kubwa ni Nyaraka za Sykes.
Sababu ya kutegemea Nyaraka za Sykes ni kuwa historia niliyoandika inahusu TANU kama chama cha kupigania uhuru wa Tanganyika.
Hii TANU imetokana na African Asociation ambayo iliasisiwa mwaka wa 1929 Kleist Sykes akiwa katibu muasisi na Cecil Matola rais muasisi.
Waasisi wa African Association ni Kleist Sykes, Cecil Matola, Mzee bin Sudi, Ibrahim Hamis, Zibe Kidasi, Ali Said Mpima, Suleiman Majisu, Raikes Kusi na Rawson Watts.
Katika kundi hili ni Kleist peke yake aliyeandika historia ya maisha yake, ''Kleist Sykes The Townsman (1884 - 1949).''
Unaweza kusoma seminar paper (1968) kuhusu maisha ya Kleist Sykes Maktaba ya Chuo Kikuu, East Africana iliyoandikwa na mjukuu wake Aisha ''Daisy'' Sykes.
Unaweza pia ukasoma maisha ya Kleist katika Modern Tanzanians (1973) kitabu alichohariri John Iliffe.
Unaweza pia ukasoma maisha ya Kleist Sykes, ''Kleist Sykes, Pioneer and Man of Ideas,'' katika ''The Life and Times of Abdulwahid Sykes (1924 - 1968) ''The Untold Story of the Muslim Struggle Against British Colonialism in Tanganyika,'' (1998).
Unaweza pia ukasoma, Dictionary of African Biography utakuta historia ya Kleist Sykes (2011).
Ikiwa unatafiti historia ya TANU hizi rejea mbili mswada (baadae kitabu) kuhusu Kleist Sykes na kitabu cha Abdul Sykes na Dictionary of African Biography kitakupa yote kuhusu historia ya AA hadi TANU.
Hicho kitabu cha Abdul Sykes ndiyo nilichoandika kutokana na nyaraka za mbele baada ya kifo cha Kleist Sykes mwaka wa 1949.
Ikiwa wewe unazo rejea ambazo unadhani zina historia ya TAA na TANU zaidi ya hizi za Sykes tafadhali nifahamishe kwani nimezunguka kwingi sikufanikiwa kuzipata.
Rowland Mwanjisi bada ya kusoma kitabu cha Abdul Sykes alikwenda kwa Ally Sykes ili anipatie ''notes,'' zake nisome.
Mzee Mwanjisi anaishi Mikocheni.
Hizi notes ninazo katika Maktaba na hakusahihisha chochote katika kitabu changu ila jina la kaka yake Dr. Wilbard Mwanjisi.
Mimi nilimwandika kama, ''William Mwanjisi.''
Hizi notes zinaeleza ugomvi uliotokea baina ya kaka yake na Julius Nyerere.
Hizi notes nilimwonyesha Prof. Shivji na waandishi wa kitabu cha Julius Nyerere, Prof. Saida Yahya Othman na Dr. Ng'wazi Kamatha.
Kuhusu Job Lusinde.
Huenda hujui.
Pale Dodoma watu waliokuwa mbele katika kuunda TANU ni Haruna Taratibu na Omari Suleiman na hawa nimezungumzanao.
Job Lusinde, Kanyama Chiume na wenzake ''Makererians,'' walimu Kikuyu Secondary School waliogopa kujitokeza wakifikiria kazi zao.
Historia yao hii imo ndani ya kitabu cha Abdul Sykes.
Mzee Lusinde nimempa nakala ya kitabu changu lakini hadi anakufa alikuwa kimya.
Hiyo picha hapo chini niliwapiga siku nilipomkabidhi Mzee Job Lusinde kitabu cha Abdul Sykes.
Nakushukuru kwa ushauri wako.