Magazetini
JF-Expert Member
- Aug 16, 2014
- 593
- 1,712
KAMPUNI ya URSUS ya kutengeneza matrekta ya kutoka Poland, imeonesha nia ya kuja kuwekeza Tanzania na iko tayari kushirikiana na kampuni ya SUMA JKT kutengeneza matrekta hayo.
Hayo yalisemwa na Rais wa Bodi ya Ursus, Karol Zarajczyk wakati akitoa maelezo ya kampuni yake mwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alipokutana na wafanyabiashara wenye nia ya kuwekeza Tanzania jana kwenye hoteli ya Sheraton jijini Warsaw, Poland.
Zarajczyk alisema wanataka kujenga kiwanda hicho nchini Tanzania kwa kutambua nafasi ya kijiografia ya mahali nchi ilipo, kuwa ni fursa ya kufungua milango kwa nchi jirani za Afrika Mashariki na Kati.
"Barani Afrika tulianza kupeleka matrekta Ethiopia, Ghana na Guinea. Sasa hivi tumeamua kuja Tanzania na Zambia. Nia yetu siyo kujenga tu kiwanda bali pia kutoa huduma kwa wakulima juu ya uendeshaji na utunzaji wa hayo matrekta," alisema.
Alisema wako tayari kutoa mafunzo kwa vijana wa Tanzania, kama vile chuo fulani ili waweze kuunganisha matrekta hayo hapa nchini na waweze kuyafanyia ukarabati na kutengeneza vipuri vyake pindi ukitokea ulazima wa kufanya hivyo.
"Tunapenda kujenga kiwanda mahali ambapo itakuwa rahisi kupata vijana wa kuajiriwa au vijana wa kutoka chuoni ili iwe rahisi kuwafundisha pia teknolojia tunayoitumia kutengeneza matreka hayo," aliongeza.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu alisema atawasilisha maelezo yao kwa Waziri anayehusika na sekta hiyo ili mawasiliano rasmi yafanyike.
CHANZO: Habari Leo