Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,967
- 32,074
Mwanafunzi mtoto wa Mufti Sheikh Hassan bin Amir, Ali Abbas anakumbuka kuwaona Abdulwahid Sykes, Dossa Aziz na Nyerere mara kadhaa katika miaka ya mwanzoni ya 1950 wakija kuonana na sheikh katika madrassa yake Kariakoo, Amani Street, nyumba nambari 36.
Kwa kawaida Abdulwahid, Dossa Aziz na Nyerere walipokuja kumwona Mufti Sheikh Hassan Bin Amir alikuwa akivunja darsa na kuwapa ruhusa wanafunzi wake ili upatikane utulivu wa maongezi.
Mazungumzo mashauriano yalikuwa yakifanyika mle mle ndani ya madrasa, Abdulwahid, Dossa na Nyerere wakiwa wamekaa chini kwenye jamvi wamekunja miguu.
Wazee wengine mashuhuri waliomuunga mkono Nyerere walikuwa mwanazuoni Sheikh Suleiman Takadir aliyeelimika sana, akijulikana zaidi kwa jina la utani ‘’Makariosí,'' Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa TANU.
Jumbe Tambaza, mzee aliyekuwa akihodhi ardhi kubwa pale mjini.
Mshume Kiyate, dalali na muuza samaki soko la Kariakoo aliyekuwa na kipato kizuri.
Mwinyijuma Mwinyikambi, aliyekuwa na viunga vya minazi na miembe.
Rajabu Diwani, seremala hohehahe aliyekuwa akisumuma randa yake Mtaa wa Congo lakini aliyejaaliwa ufasaha mkubwa wa kuzungumza.
Makisi Mbwana, kiongozi wa Wazaramo rais wa Zaramo Union mjini Dar es Salaam.
Sheikh Haidari Mwinyimvua, fundi cherehani na mtu mwadilifu.
Iddi Faizi Mafungo na Idd Tosiri ndugu wawili Wamanyema na binamu wa Sheikh Mohamed Ramia wa Bagamoyo, Khalifa wa tariqa ya Qadiriya.
Iddi Faizi akiwa mweka hazina wa Al Jamiatul Islamiyya na Iddi Tosiri mwanachama shupavu.
Iddi Tulio, mtu mwenye heshima zake.
Iddi Tulio alishika nafasi ya Sheikh Suleiman Takadir ya uenyekiti wa Baraza la Wazee wa TANU baada ya kutokea sintofahamu kati ya Sheikh Suleiman Takadir Mwenyekti wa Baraza la Wazee wa TANU na Julius Nyerere Rais wa TANU,
kutoelewana kutokana na Uchaguzi wa Kura Tatu mwaka wa 1958.
Ramadhani Mashado Plantan, mhariri na mmiliki wa gazeti la Zuhra na kaka yake Schneider Abdillah Plantan, watoto wa Affande Plantan Mzulu aliyeingia Tanganyika na jeshi la askari mamluki wa Kizulu chini ya kamanda Mjeruami Herman von Wissman kuja kuwasaidia Wajerumani kuitawala Tanganyika chini ya mtutu wa bunduki.
Kwa heshima yake Wajerumani mwaka wa 1914 Vita Kuu ya kwanza wakati wako katika ya mapigano na Waingereza Tanganyika walisimamisha vita kwa juma moja baada ya kifo chake kuomboleza.
Affande Plantan alikuwa ndiye mkuu wa Germany Constabulary Dar es Salaam.
Pamoja na hawa kulikuwa nyuma ya Nyerere wazee wengi ndani ya TANU waliomuunga mkono Julius Nyerere. Hiki kilikuwa kipindi muhimu katika historia ya Tanganyika.
Imekuwaje katika kundi hili la watu maarufu kiasi hiki Mshume Kiyate akatokea juu zaidi kuwashinda hawa wote?
Itaendelea...