Sina hakika "usafi" wa lugha ni kitu gani. Nilipata kusoma makala moja juu ya Kiingereza cha Marekani. Mtafiti alikuwa na ramani ya Marekani, akazunguka Marekani nzima kuuliza: Kiingereza kibaya kinasemwa wapi na Kiingereza kizuri kinasemwa wapi Marekani. Wa New York na mashariki walisema watu wa kusini wa Kiingereza kibaya. Watu wa kusini walisema watu wa pwani ya mashariki na magharibi wana Kiingereza kibaya. Watu wa sehemu za nyanda za kati walisema watu wa kusini wanasema Kiingereza kibaya. Kila mmoja alikuwa na MAONI tofauti juu ya ubora wa lugha au lahaja mbalimbali.
Kwa hivyo basi, usafi wa lugha au ubora wa lahaji si sifa ya lugha yenyewe, bali ni maoni ya watu. Maoni hutofautiana kulingana na vigezo. Yumkini mtaalamu isimu atakwepa kutoa sifa ya "usafi" wa lugha kwa sababu kila lahaja inafuata kanuni fulani. Lahaja kama Kisanifu ni lahaja zilizoteuliwa tu, na jambo hili lisidhaniwe kuwa ni ubora wa lahaja.