BAK
JF-Expert Member
- Feb 11, 2007
- 124,790
- 288,165
Date::2/2/2009
Waziri atetea matumizi ya magari ya kifahari serikalini
Na Mwandishi Wetu
Mwananchi
Waziri atetea matumizi ya magari ya kifahari serikalini
Na Mwandishi Wetu
Mwananchi
SERIKALI imezitaja zababu za kununua magari ya kifahari na ya bei kubwa ya aina ya "mashangingi" kwa ajili ya wizara na idara zake.
Naibu Waziri wa Miundombinu, Hezekiah Chibulunje alielezea aina hiyo ya magari kuwa ni imara na yanayoweza kuhimili safari ndefu vijijini.
"Kigezo kinachotumika kununua magari aina ya ‘Four wheel drive' maarufu kama 'mashangingi' kwa Wizara na idara zake ni ubora, uimara na usalama wa magari hayo, kuweza kuhimili safari ndefu katika barabara za vijijini ambako viongozi na watumishi wengi wa umma hulazimika kwenda kuwahudumia wananchi," alisema Chibulunje.
Alisema tangu magari hayo yaanze kutumika nchini mwishoni mwa miaka ya 1980, serikali imekuwa ikitathmini mwenendo wa gharama za matumizi ya magari hayo.
Alifafanua kuwa katika tathmini hiyo, ilibaini kuwa maghari hayo yanapoanza kuchakaa, gharama za kukarabati zinapanda maradufu.
"Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kupunguza gharama za matumizi ya magari hayo, ikiwa ni pamoja na kufuta magari yaliyochakaa kila baada ya miaka mitano," alisema Chibulunje.
Vile vile, alisema serikali imekuwa ikihakikisha kuwa, magari hayo yanatumika inapolazimu, ili kupunguza gharama na matumizi yasiyo ya lazima.
Pamoja na uzuri wa magari hayo, Chibulunje alisema kuwa serikali inao mkakati wa kupunguza wingi wa magari hayo nchini kwa kubana ununuzi wake.
Katika mpango mpya ambao unaandaliwa na wizara yake, alisema utaweka utaratibu wa matumizi ya serikali kufuatana na wadhifa wa viongozi.
"Wizara yangu, hivi sasa inaandaa waraka wa baraza la mawaziri juu ya utaratibu wa matumizi ya magari ya serikali kufuatana na wadhifa wa viongozi wa serikali," alibainisha Chibulunje.
Alisema mpango huo wenye lengo la kupunguza matumizi ya mashangingi ukikamilika, utapelekwa kwenye baraza la mawaziri, ili kupata baraka zake kabla ya kuanza kutumika.
Maelezo ya serikali yalitokana na swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Lucy Owenya (Chadema) aliyeeleza kuwa matumizi ya magari ya kifahari aina ya mashangingi, yamekuwa yakiongeza matumizi yasiyo ya lazima serikalini.
Owenya alitaka kujua kigezo kinachotumika katika kununua magari hayo, pamoja na mipango ya serikali kwa siku za baadaye.
Rais Jakaya Kikwete hivi karibuni alitangaza kuwa serikali yake ina mpango wa kupunguza matumizi ya magari ya kifahari na ya bei kubwa, ili kubana matumizi.