Stephano Mgendanyi
JF-Expert Member
- May 16, 2020
- 2,833
- 1,301
WAZIRI BASHUNGWA AKUTANA NA UJUMBE KUTOKA KOREA KUSINI, WAJADILI NAMNA YA KUBORESHA MIUNDOMBINU NCHINI
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe kutoka nchi ya Korea Kusini ulioongozwa na Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Fedha ya Korea kwa ajili ya Ujenzi (K-Finco), Dkt. Lee Eun Jae pamoja na Balozi wa Tanzania nchini humo, Togolani Mavura, leo Ijumaa Julai 26, 2024 jijini Dar es Salaam.
Mazungumzo hayo yamehusisha maeneo ya ushirikiano, ubia na kuangalia fursa za uwekezaji zilizopo katika sekta ya miundombinu hususan barabara na madaraja.
Akiongea baada ya mkutano huo, Waziri Bashungwa amesema Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) itaangalia namna bora ya kushirikiana na sekta binafsi katika ujenzi ili kuipunguzia Serikali mzigo wa gharama pamoja na kuondoa utegemezi wa serikali pekee katika ujenzi wa miundombinu ya barabara nchini.
"Kwa upande wa TANROADS tutaendelea kujipanga ili kuhakikisha kwamba, maeneo ambayo tunaweza kujenga barabara kwa kushirikiana na sekta binafsi. Toll Road System (Barabara za mfumo wa kulipia) , Express High Ways ndio mambo ya karne ya 21, na itaondoa ule utegemezi wa serikali peke yake katika ujenzi wa miundombinu ya barabara." amesema Waziri Bashungwa.
Aidha, Waziri Bashungwa amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kukuza diplomasia na kuitangaza vyema nchi ya Tanzania duniani.
Ameeleza kuwa ujio wa ujumbe huo umechangiwa na kuvutiwa na tunu nyingi zinazopatikana nchini ikiwemo utulivu, amani, umoja, mshikamano pamoja na utawala wa sheria, tunu ambazo wawekezaji huvutiwa nazo na kufikia hatua ya kuweka mitaji yao na kuwekeza.
Kikao hicho kati ya ujumbe kutoka Korea Kusini na Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Innocent Bashungwa kilichoangazia fursa za uwekezaji katika sekta ya miundombinu nchini kilihudhuriwa na, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi Balozi Mhandisi Aisha Amour, Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi Mohamed Besta pamoja Watendaji Wakuu kutoka TEMESA, TBA, ERB, AQRB na NCC.