JanguKamaJangu
JF-Expert Member
- Feb 7, 2022
- 2,780
- 6,607
Uongozi wa Dodoma Jiji unadai eneo hilo tunaloishi wakazi wa Kata ya Ipala Jijini Dodoma ni mali ya Serikali, wanataka kutuhamisha kwa njia ambayo tunaona siyo sahihi.
Wakati wakitaka kutuhamisha tuliomba zuio na vielelezo vinavyoonesha kwamba ni eneo la Serikali lakini hawatupi, zaidi wamekuwa wakituzungusha.
Kuna wakati kiongozi fulani aliyekuwa anashughulikia mchakato huo alitaka kuwapa Wananchi fedha na makali ili waachanane na eneo hilo, suala hilo halikufanikiwa.
Bada ya hapo, kumekuwa na mchakato wa upimaji wa maeneo wakati sisi tukiwa eneo hili la tukio, wakifuatwa kuulizwa wanaondoka, baada ya siku kadhaa wanarejea tena.
Kuna wakati walikuja Wapimaji kukatokea vurugu kati ya Wananchi na Wapimaji.
Tulivyoita Waandishi wa Habari nao wakadai wamepewa vitisho na Wanausalama, wakati huo wenzetu wakapigwa na wengine kukamatwa.
Kuna Mwananchi mmoja kati ya waliopigwa kwenye sakata hilo alipoteza maisha siku kadhaa baadaye, kuna Mwananchi mwingine naye amepata ulemavu wa kupooza.
Kuna siku Wananchi tulikuwa na kikao pamoja na Mkurugenzi wa Jiji ambaye aliambatana na Askari kadhaa akasema eneo hilo litafanyiwa vipimo lakini baada ya muda wenyeji tutapewa kipaumbele cha kwanza kuuziwa, kilichotushangaza inakuwaje maeneo ni ya Serikali kisha tunauziwa.
Kuna kipindi watangazaji wa Radio Clouds FM walikuja Dodoma, tukaenda kuzungumza nao kuwaelezea changamoto yetu kwa undani, Mkurugenzi wa sasa John Kayombo alipopogiwa simu na Watangazaji wa redio hiyo, akasema yeye haujui huo mgogoro wala hajawahi kuusikia, akaagiza kuwa tukitoka kwenye mahojiano hayo twende ofisini kwake akatusikilize.
Tulipofika akatuambia kwa nini tumeanzia Clouds FM bila kwenda kwake, baada ya hapo hakutaka kuzungumza tena na sisi, hakutupa ushirikiano vizuri.
Baadaye tulipopata nafasi ya kuzungumza naye akaanza kumfokea Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wetu akimwambia na yeye ni Serikali kwa nini anaungana na Wananchi?
Tangu wakati huo hatupati majibu ya kueleweka, wanasema eneo hilo ni la CDA na ni eneo la Misitu lakini hawatupi ufafanuzi wa kueleweka ni kama wanataka kutuhamisha kihuni.
Mpaka sasa hatujui hatima yetu, tunaishia kupata vitisho vya aina mbalimbali. Tunaiomba Wizara ya Ardhi inayoongozwa na Jerry Silaa kuja kutusaidia kwani inavyoonekana kuna watu wachache wanataka kutumia mgongo wa Serikali kutukandamiza na kuchukua haki zetu.
Tunachotaka watuambie eneo letu ni huru na tunaweza kupimiwa ili maisha yetu yaendelee.
Ramani ya Mipango Miji haioneshi eneo letu ni Msitu, ni Green Belt inaonesha kustawisha maeneo ambayo tayari yanaonekana na siyo kwamba yanachukuliwa na Serikali.
Kuna siku sikufanikiwa kumrekodi lakini kuna Kiongozi mmoja alisema “Hata huyo Waziri tunayemtaka, naye anahusika katika eneo hilo kwa namna fulani.”
Maafisa wa huku wamekuwa na mtindo wa kwenda sehemu kupima wakidai ni maeneo ya Serikali, ukipisha wanayachukuwa watu binafsi na kufanya biashara.
Mfano kuna Mzee tupo naye katika hili Sakata, alizungumza mbele ya Mkurugenzi hadi akatoa machozi, alisema alinunua eneo maeneo ya Kikombo, wapimaji walivyokuja wakasema ni eneo la Serikali tukapisha.
Miezi mitatu baadaye akiwa anatafuta kiwanja akapelekwa katika eneo lilelile alilolicha yeye akiambiwa ni eneo la Serikali.
Pia soma ~ Waziri wa Ardhi, Jerry Silaa apiga marufuku uuzaji wa viwanja mitaani