4.0 MAREKEBISHO YA SHERIA YA MIFUKO YA HIFADHI YA JAMII
Mheshimiwa Spika,
Baada ya kutapanya fedha za wafanyakazi kwa kuwekeza katika grandiose projects isiyokuwa na manufaa ya kiuchumi kwa wafanyakazi wanachama na hata kwa Mifuko yenyewe, sasa Serikali hii ya CCM imeamua kuwadhulumu wafanyakazi fedha zinazotokana na makato ya mishahara yao. Vile vile, inaelekea Serikali hii ya CCM inataka kuficha uchafu ilioufanya katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa kutunga Sheria inayowazuia wafanyakazi kupata fedha zao wakati wanapozihitaji zaidi, yaani wanapokuwa hawana ajira.
Hii imefanyika kwa Serikali kupenyeza kinyemela, na kinyume cha Kanuni za Kudumu, masharti yanayowazuia wafanyakazi wote wanachama wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii Tanzania kuchukua mafao ya kujitoa uanachama wa Mfuko husika kabla ya kufikisha umri wa miaka hamsini na tano au sitini. Kisheria, umri wa kustaafu kwa hiari ni miaka hamsini na tano wakati umri wa kustaafu kwa lazima ni miaka sitini. Kwa masharti haya, mfanyakazi hana haki au namna nyingine yoyote ya kupata fedha za makato yake ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii hata akiachishwa kazi na mwajiri wake bila kosa lolote, hadi atakapofikisha umri huo wa kustaafu kwa hiari au kwa lazima.
Mheshimiwa Spika,
Muswada wa Marekebisho ya Sheria za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, 2012 ulichapishwa katika Gazeti la Serikali la tarehe 12 Januari, 2012. Hakukuwa na masharti ya kuzuia mafao ya kujitoa uanachama wa Mfuko. Tarehe 1 Februari, 2012, Muswada huu uliletwa Bungeni kwa ajili ya Kusomwa kwa Mara ya Kwanza chini ya kanuni ya 83(1) ya Kanuni za Kudumu. Hapa pia hakukuwa na masharti ya kuzuia mafao ya kujitoa. Baada ya hapo, Muswada ulipelekwa kwenye Kamati ya Huduma za Jamii kwa ajili ya kuujadili kwa mujibu wa kanuni ya 84(1) ya Kanuni za Kudumu. Masharti hayo hayakujadiliwa wala kupendekezwa na Kamati ya Huduma za Jamii. Ingekuwa hivyo, kwa mujibu wa kanuni ya 84(3) na (4)ya Kanuni za Kudumu, masharti hayo yangeletwa Bungeni wakati wa Muswada kusomwa kwa Mara ya Pili. Hilo halikufanyika.
Kutoka kwenye Kamati, Muswada huu ulirudishwa Bungeni tarehe 13 Aprili, 2012 kwa ajili ya Kusomwa kwa Mara ya Pili na kujadiliwa na Bunge lako tukufu chini ya kanuni ya 86 ya Kanuni. Hotuba yote ya Waziri haina mstari hata mmoja unaoonyesha nia ya Serikali ya kufuta mafao ya kujitoa kwa wanachama ambao hawajafikisha umri wa kustaafu kwa hiari au kwa lazima. Aidha, hotuba za Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii na Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni nazo ziko kimya juu ya kufutwa kwa mafao ya kujitoa uanachama. Ukimya huu unatokana na ukweli kwamba hadi kufikia hatua hiyo hakukuwa na jambo lolote la kuashiria nia ya Serikali kufuta mafao ya kujitoa.
Aidha, sio Mwenyekiti wa Kamati au Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani pekee waliokuwa kimya kuhusu masharti haya. Kwa mujibu wa Taarifa Rasmi ya Majadiliano ya Bunge ya Mkutano wa Saba, Kikao cha Nne cha tarehe 13 Aprili, 2012, hakuna hata mmoja wa Wabunge wote thelathini na nane waliochangia mjadala wa Muswada aliyezungumzia suala la kufuta mafao ya kujitoa uanachama wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Suala hilo halikuzungumziwa katika michango ya Wabunge kwa sababu halikuwepo kwenye mjadala. Na wala halikuingizwa kwenye mjadala na Wabunge wengine watano waliowasilisha Majedwali ya Marekebisho ya vifungu mbali mbali vya Muswada.
Mheshimiwa Spika,
Kwa kutumia udhaifu wa uongozi wa Bunge katika kusimamia Kanuni za Kudumu, na upungufu wa muda wa mjadala Bungeni ambao ni matokeo ya kuvurugwa kwa Kanuni za Kudumu zinazohusu muda wa Wabunge kujadili hoja za Serikali, Waziri aliwasilisha Jedwali la Marekebisho lililopendekeza marekebisho ya vifungu vipatavyo 45 na vifungu vidogo karibu 70 vya Muswada. Ni katika msitu huo wa Jedwali la Marekebisho ndiko Serikali ilikochomeka masharti ya kufuta mafao ya kujitoa kwa wafanyakazi wasiofikisha umri wa kustaafu kwa hiari au kwa lazima. Kwa sababu ya urefu wa Jedwali na uchache wa muda wa kulichunguza na kujadili, inaelekea hakuna Mbunge hata mmoja aliyeona mapendekezo hayo ya kufuta mafao ya kujitoa. Hansard inaonyesha kwamba ibara za 9, 10 na 11
zilipitishwa na Kamati ya Bungeni Zima pamoja na marekebisho yake. Ibara ya 11 ndio iliyobadilishwa na Jedwali la Marekebisho la Waziri kwa kuweka masharti kwamba mfanyakazi atapata mafao ya kujitoa pale tu atakapofikisha umri wa miaka 55 au miaka 60.
Mheshimiwa Spika,
Mara nyingi Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imelalamikia ukiukwaji wa kanuni zinazohusu muda wa mjadala Bungeni. Tumelalamika kwamba uongozi wa Bunge umeshiriki katika kupunguza muda wa mjadala kinyume cha Kanuni za Kudumu. Hatukusikilizwa. Tumepigia kelele kupunguzwa kwa muda wa mjadala wakati wa kupitisha vifungu vya Miswada ya Sheria na mafungu ya bajeti.
Hakuna aliyetaka kuelewa kelele zetu. Tumepaza sauti zetu kwamba Bunge lako tukufu linageuzwa kuwa muhuri wa kuhalalisha maamuzi ya Serikali tunayotakiwa kuisimamia na kuishauri. Tumepuuzwa. Haya ndio matokeo ya kuruhusu kanuni za mjadala kukanyagwa jinsi zilivyokanyagwa. Sheria hii inayodhulumu wafanyakazi kwa kuzuia mafao yao ya kujitoa katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii sio tu ni matokeo ya hila za Serikali, bali pia ni uthibitisho wa ulegevu wa uongozi wa Bunge na udhaifu wa Bunge lenyewe katika kusimamia Kanuni za Kudumu za Bunge lako tukufu.
Mheshimiwa Spika,
Kwa mujibu wa Kumbu Kumbu Rasmi, kifungu pekee kilichofanyiwa marekebisho ya kuzuia fao la kujitoa ni kifungu cha 21 cha Sheria ya Mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma. Hata hivyo, SSRA imedai kwamba Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii yanahusu Mifuko yote na wafanyakazi wote. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulieleza Bunge lako tukufu kama Sheria hii mpya imerekebisha vifungu vya Sheria nyingine by implication, kama inavyoelekea kuwa tafsiri ya SSRA. Kama Sheria mpya haijabadilisha vifungu vya Sheria za Mifuko mingine, ni kwa nini SSRA inangangania kwamba marekebisho ya Sheria ya PPF
yanawahusu wafanyakazi wote nchini mwetu bila kubagua sekta yoyote ile.
Mheshimiwa Spika,
Aidha tunaelewa kuwa Pensheni ni suala la msingi sana na hatuwezi kuwaacha wazee wetu waishi bila Pensheni. Vile vile tunatambua kuwa kuna mahitaji ya sasa ambayo hayasubiri mpaka mtu azeeke ndipo aweze kuyatatua ndio maana tunaunga mkono wafanyakazi katika kupata fao la kujitoa na tunapendekeza sheria irekebishwe na kuzingatia yafuatayo;
i. Uanzishwe utaratibu wa kuwa na mafao kwa wanachama ambao ama wamekosa kazi kutokana na sababu mbalimbali (Unemployment benefits) kama vile kumalizika kwa mkataba , kuachishwa kazi,kufukuzwa kazi nk kwa kipindi cha miezi sita mwanachama wa mfuko husika aweze kulipwa kiasi cha mshahara kamili na miezi sita mingine kama hajapata kazi alipwe nusu mshahara na mfuko na baada ya mwaka mmoja kama atakuwa hajapata kazi basi mfuko uache kuendelea kumlipa mwanachama huyo. Mifuko itenge fungu maalum kwa ajili ya kulipia mafao hayo.
ii. Mifuko itenge fedha kwa ajili ya masomo (Education fund) kwa ajili ya wanachama wake pindi watakapokuwa wanaenda masomoni wakiwa ni wanachama wa mfuko ,hii itawafanya wanachama kuweza kujiendeleza kielimu na hivyo itapunguza idadi ya wanachama ambao wanajitoa kwa ajili ya kupata fedha za kusoma.
Mheshimiwa Spika,
Aidha Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kurejea pendekezo letu tuliloishauri katika bajeti ya Wizara hii ya mwaka 2011/2012 katika kuona umuhimu wa kuiunganisha mifuko yote ya hifadhi za jamii na kubaki katika wizara moja ambayo ni ya Kazi na Ajira. Kambi rasmi ya Upinzani inasisitiza kuwa lengo kuu la kuunganisha mifuko hii ya hifadhi za jamii ni katika kuirahisishia Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Hifadhi za Jamii (SSRA) katika kutekeleza Sheria moja na kuunda vifungu sawa vya kisheria vitakavyosimamia utekelezaji na uendeshaji wa mifuko hii ambapo kwa sasa mifuko hii imekuwa chini ya wizara tofauti na hivyo hata utekelezaji wake unakua mgumu na kuleta ukinzani kwa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Hifadhi za Jamii.
Tunasisitiza kuwa pendekezo letu ni kuifanya PPF na NSSF iunganishwe na kuwa mfuko mmoja kwaajili ya Sekta Binafsi vilevile LAPF, PSPF na GEPF iunganishwe na kuwa mfuko mmoja kwaajili ya Sekta ya Umma. Pia, kambi ya Upinzani inapendekeza mifuko yote isimamiwe chini ya Wizara ya Kazi na Ajira.