beth
JF-Expert Member
- Aug 19, 2012
- 3,880
- 6,368
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amefuta mnada wa nafaka, ulioendeshwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Januari 7 mwaka huu. Ameagiza uongozi wa mamlaka hiyo, kutangaza upya zabuni, baada ya kutoridhishwa na taratibu zilizofanyika awali.
Mnada huo unahusisha mahindi tani 5,000 na ngano tani 460.12, unafanyika baada ya wahusika kushindwa kutimiza masharti ya kiforodha, hivyo serikali imeamua kuuza ili kufidia gharama zake.
Nafaka hizo ziliingia nchini Machi 2017. Waziri Mkuu alisitisha mnada huo, wakati akizungumza na Kamishna wa Forodha na Ushuru wa Bidhaa wa TRA, Ben Asubisye, jijini Dar es Salaam jana.
Waziri Mkuu aliagiza kutangazwa upya kwa mnada mwingine wa kuuza mahindi hayo, sambamba na ngano. Aliitaka TRA ihakikishe masuala yote kuhusu mnada huo, yanakamilika ndani ya siku tatu kuanzia jana.
“Mahindi yameuzwa kwa bei ya shilingi 340 kwa kilo moja ambayo ni chini na bei ya soko kwa sababu bei ya mahindi sokoni kwa sasa ni shilingi 800. Zabuni imetangazwa kwa muda mfupi, watu wameshindwa kushiriki. Ilifunguliwa saa 8:00 mchana na imefungwa saa 5:00 usiku”, alisema.
Pia, Waziri Mkuu aliutaka uongozi wa TRA, uhakikishe mnada unaofuata unakuwa wa wazi, huru na kutoa muda wa kutosha kwa wananchi wote kushiriki ili kuondoa malalamiko.
“Kwa kuwa mnada unafanyika kwa njia ya mtandao, hakikisheni matumizi ya mtandao yanakuwa rafiki kwa wananchi wote watakaovutiwa kuwasilisha zabuni zao,”aliagiza.
Hata hivyo, Waziri Mkuu alisitiza kuwa TRA ishirikiane na mamlaka nyingine za serikali, kuhakikisha wanunuzi wa nafaka hizo, hawaziingizi sokoni kwa ajili ya matumizi ya binadamu. Nafaka hizo zimepimwa na kuthibitika kuwa zinafaa kwa matumizi ya wanyama.