mkiluvya
JF-Expert Member
- May 23, 2019
- 809
- 729
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameikabidhi Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi nyumba 103 zenye gharama ya zaidi ya sh. bilioni tano kwa ajili ya makazi ya Maafisa na Askari wa Idara ya Uhamiaji nchini zilizojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) katika eneo la Iyumbu jijini Dodoma ikiwa ni utekelezaji wa uamuzi ulitolewa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Baada ya kukabidhi nyumba hizo, Waziri Mkuu amesema kwamba makazi hayo yawe chachu kwa Maafisa na Askari wa Idara ya Uhamiaji nchini katika kutambua wajibu wao wa kutoa huduma iliyobora na inayokidhi matarajio ya wateja ambao ndiyo waajiri wao.
Akikabidhi nyumba hizo leo (Jumanne, Juni 2, 2020), Waziri Mkuu amesema “Uamuzi huu wa Mheshimiwa Rais ambao leo hii tunashuhudia utekelezaji wake kupitia makabidhiano haya, utasaidia kuwafanya Maafisa na Askari wa Uhamiaji kukaa katika makazi yao tofauti na ilivyokuwa hapo awali ambapo waliishi uraiani.”
Ameongeza kuwa “Ni ukweli usiofichika kuwa makabidhiano ya nyumba hizi baina ya Shirika la Nyumba la Taifa na Idara ya Uhamiaji ni moja kati ya vielelezo vya utekelezaji wa ahadi ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya kuwapatia Maafisa na Askari wa Idara ya Uhamiaji nyumba 103.” Pia, Waziri Mkuu amesema “Nyote mtakubaliana nami kwamba leo ni siku muhimu kwa sekta ya nyumba kwani ujenzi wa nyumba za namna hii ni muhimu katika kuimarisha upatikanaji wa huduma bora kwenye Taasisi za Serikali sambamba na kuboresha ufanisi wa wafanyakazi wetu.”
“Vilevile, utekelezaji wa mradi huu umetoa ajira zipatazo 1,000 ikiwa ni sawa na ajira 800 za mafundi na ajira 200 kwa watoa huduma za chakula yaani mama lishe. Upatikanaji wa ajira hizo umechangia kuongeza kipato kwa walengwa na kusaidia kujikwamua dhidi ya umaskini.”
Wakati huo huo, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuipongeza Idara ya Uhamiaji kwa kuimarisha ulinzi na usalama wa mipaka pamoja na kufanikisha maboresho mbalimbali kama vile Uhamiaji Mtandao ambapo sasa huduma za pasipoti, vibali vya ukaazi, viza, usimamizi na udhibiti wa mipaka vinafanyika kwa njia ya kielektroniki. “Utekelezaji mzuri wa mageuzi ya Uhamiaji Mtandao umewezesha idara hii kupata tuzo ya ushindi wa pasipoti yenye ubora duniani kwa mwaka 2019.” Waziri Mkuu amesema ushindi huo, umelipatia sifa na heshima kubwa Taifa Kimataifa. “Halikadhalika, nimefurahishwa na taarifa kuwa ujenzi wa Makao Makuu ya Idara ya Uhamiaji, Dodoma nao unaendelea vizuri. Ninawahimiza endeleeni hivyo kwa mustakabali wa ustawi wa Taifa letu.”
Awali, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala aliishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuwezesha Idara ya Uhamiaji, kupata nyumba 103 za makazi kwa ajili ya Maafisa na Askari wa Uhamiaji kwani hatua hiyo ni kielelezo cha vipaumbele vya Serikali katika kuboresha makazi ya askari wa vyombo vyote vya Ulinzi na Usalama pamoja na wananchi kwa ujumla.