nngu007
JF-Expert Member
- Aug 2, 2010
- 15,860
- 5,801
JUMAMOSI, FEBRUARI 23, 2013 04:23 NA MWANDISHI WETU
*Dk Kawambwa apata wakati mgumu mbele ya JK
WAZIRI wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Mhandisi Christopher Chiza, amejitosa katika sakata la mitihani na kusema wanafunzi wamefeli kutokana na njaa.
Kauli ya Chiza imekuja wakati ambao, matokeo ya kidato cha nne yaliyotolewa hivi karibuni, yanalalamikiwa kwa sababu ya idadi kubwa ya wanafunzi kufanya vibaya.Chiza alitoa kauli hiyo jana, mbele ya Rais Jakaya Kikwete katika hafla ya uzinduzi wa utaratibu wa mfumo mpya wa usimamizi na ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo, iliyofanyika katika hoteli ya White Sands Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika hafla hiyo, Chiza alisema suala la uzalishaji wa chakula ni muhimu ili kuondokana na matatizo ya njaa shuleni.
Alisema kilimo ni sekta mtambuko, hivyo haina budi kupewa kipaumbele, kwani inapolega athari yake ni kubwa kijamii na hata kiuchumi.
"Wanafunzi wamefeli mitihani kwa sababu ya njaa, hivyo lazima tuongeze uzalishaji wa mazao ya chakula ili kuondokana na tatizo hili," alisema huku wajumbe wakiangua kicheko ukumbini.
Katika hafla hiyo, Waziri wa Elimu na Mfunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa alipata wakati mgumu katika mkutano huo.
Kawambwa alikumbwa na hali hiyo baada ya wajumbe waliohudhuria mkutano huo kucheka kila aliposimama.
Mara ya kwanza, walicheka wakati Rais Kikwete alipokuwa akiwatambulisha Mawaziri na wao kusimama.
Kawambwa alichekwa mara ya pili wakati aliposimama mbele kuelezea suala zima la elimu na changamoto zake kwa wajumbe wa mkutano huo ambao pia ulihudhuriwa na watu wa mataifa ya nje.
Hali hiyo haikumfurahisha Dk Kawambwa, ambapo kabla ya kuzungumza alikaa kipya kidogo kasha kusema.
"Nasononeka sana,mnapocheka najisikia vibaya," alisema Dk Kawambwa kasha kuendelea kueleza juhudi zinazofanywa na wizara yake kuinua elimu nchini.
Kitendo hicho kilimlazimisha Waziri wa Kilimo, Chiza kutafuta namna ya kumnusuru Kawambwa akitumia fursa aliyopewa kuzungumza kwa dakika tatu juu ya sekta ya kilimo mbele ya wajumbe ambao ni watalaamu mbalimbali wa ndani na nje ya nchi.
Chiza badala yake, alianza kwa kusema wakati anakuja kwenye mkutano huo walikuwa wanajadiliana juu ya matatizo ya watoto kufeli mitihani na kugundua kuwa njaa ndiyo kikwazo.
"Watoto wetu hawafaulu kwa sababu ya njaa, na chini ya mfumo huu mpya utakuja na ufumbuzi huo" alisema Chiza ambaye pamoja na mambo mengine alisisitiza kuwa Wizara yake imejidhatiti kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula ifikapo 2015.
Kauli ya Chiza ilitanguliwa na ya Kawambwa ambaye wakati amesimama kuelezea suala zima la elimu mbele ya mkutano huo, alilizamika kueleza wazi kuwa amesononeshwa na kitendo cha kumcheka.
Baada ya kusema hivyo, Kawambwa aliendelea kuzungumza kwa kushukuru suala la elimu kuingizwa kwenye mfumo huo ambao alisema anaamini utakuja na ufumbuzi wa matatizo yanayoikabili sekta hiyo.
Matatizo makubwa yaliyosababisha kidato cha nne kufeli ni upungufu wa walimu wakiwamo wa sayansi, upungufu wa vifaa ambapo alisema, mchakato wa mfumo huo utasaidia kutoa majibu ya hayo yote.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya mkutano huo, Kawambwa alisema semina hiyo ni kama imeota imekuja wakati ambapo matokeo ya kidato cha nne yametoka mabaya.
Hata hivyo Kawambwa alisema kufeli kwa wanafunzi kunatokana na sababu kuongezeka kwa udhibiti wa mitihani.
"Udhibiti umekuwa mkubwa safari hii, husikii mahali popote kama mtihani ulivuja…haya ni mafanikio, miaka ya nyuma watu walikuwa wanajiuliza hata huyu kafaulu?" alisema Kawambwa.
Kawambwa aliitaja sababu nyingine kuwa ni kushuka kwa kiwango cha udanganyifu.
"Mwaka jana tuliwafutia matokeo kwa udanganyifu watoto 3330, mwaka huu idadi imepungua, matokeo haya ni ya kweli" alisisitiza Kawambwa.
Alisema pengine wazazi wanaweza kusema shule za sekondari za serikali zimefanya vibaya jambo ambalo alisema si kweli.
Kawambwa alisema hata shule binafsi na seminari pia zimefanya vibaya katika matokeo hayo kutokana na sababu hizo.
Kawambwa alisema jambo hilo si la kufurahia lakini pia si la kuingiza siasa za bei nafuu ambazo hazitaki.
Kwa karibu wiki sasa, Waziri Kawambwa amekuwa akiandamwa, huku baadhi wakimtaka ajiuzulu, kutokana na sekta ya elimu kufanya vibaya.
Hata hivyo jana gazeti hili lilimkariri Kawambwa akisema hawezi kujiuzulu kwa sababu ya wanafunzi kushindwa mitihani na kwamba hiyo ni lugha ya kisiasa.
Kawambwa alikwenda mbali zaidi na kusema kuwa tatizo si yeye bali ni mfumo wa elimu, hivyo kujiuzulu kwake hakutasaidia lolote.
SOURCE; MTANZANIA