Stephano Mgendanyi
JF-Expert Member
- May 16, 2020
- 2,833
- 1,301
Waziri Prof. Kitila Mkumbo Azindua Ofisi ya TIC Arusha na Awamu ya Pili ya Uhamasishaji Uwekezaji Kitaifa
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, amefungua rasmi Ofisi ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Arusha iliyopo jengo la Ngorongoro, Arusha. Hafla hiyo pia ilienda sambamba na uzinduzi wa awamu ya pili ya Kampeni ya Kitaifa ya Uhamasishaji Uwekezaji.
Prof. Mkumbo alitangaza kuwa ofisi hiyo sasa itakuwa kituo kikuu cha Kanda ya Kaskazini, akibainisha sababu za kuhamishia ofisi hiyo kutoka Moshi, Kilimanjaro hadi Arusha. Alieleza kuwa Arusha ni kitovu cha utalii Tanzania na hivyo inastahili kuwa na ofisi ya kanda ya TIC. Zaidi ya hayo, alisema Arusha pia ni kitovu cha diplomasia, na kuna haja ya kutumia diplomasia ya uchumi kukuza uwekezaji.
Akizindua awamu ya pili ya Kampeni ya Taifa ya Uhamasishaji Uwekezaji, Prof. Mkumbo alizitaka mamlaka zote za urekebu na udhibiti nchini Tanzania kuhakikisha zinawasaidia na kuwalea wawekezaji na wafanyabiashara ili waweze kufanya shughuli zao kwa uhuru na faida bila usumbufu. Alihimiza umuhimu wa kuunganisha mamlaka hizi kidijitali ili kumwezesha mfanyabiashara na mwekezaji kulipa tozo na kupata leseni moja badala ya utitiri wa leseni.
Katika hotuba yake, Prof. Mkumbo alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Makonda, kwa ubunifu na kasi katika kutekeleza maono na mipango ya serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Alisema, "Kila siku hapa Arusha kuna kitu kipya kinafanyika cha kuleta maendeleo kwa wananchi wa Arusha."
Naye Mhe. Paul Makonda aliishukuru Wizara na TIC kwa kutimiza ahadi yao ya kufungua ofisi Arusha. Alisema maono yake ni kuona TIC inakuwa kituo bora cha kuvutia uwekezaji barani Afrika, na alisisitiza umuhimu wa kuwa na watumishi wenye weledi watakaowahudumia wawekezaji kwa upendo ili waone fahari ya kuwekeza nchini.
Akiongea katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Gilead Teri, alisema uzinduzi huo ni utekelezaji wa maazimio ya kongamano la uwekezaji lililofanyika tarehe 30 Aprili 2024. Azimio kuu mojawapo lilikuwa ni kufungua ofisi ya Kituo cha Uwekezaji Arusha na kuzindua awamu ya pili ya kampeni ya uhamasishaji uwekezaji kitaifa kufuatia mafanikio makubwa ya awamu ya kwanza.
Hafla hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Ngorongoro, jijini Arusha, ilihudhuriwa na wadau mbalimbali wa uwekezaj, viongozi mbalimbali na maafisa kutoka Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji na TIC. Uzinduzi huu unatarajiwa kuleta mapinduzi makubwa katika ya uwekezaji nchini Tanzania, hususan katika kanda ya kaskazini.