BARD AI
JF-Expert Member
- Jul 24, 2018
- 3,591
- 8,826
Waziri amesema wagonjwa wa saratani wanaopata tiba za mionzi kwa Bima ya NHIF mwaka 2015/16 zilikuwa Tsh. Bilioni 9 na hadi kufikia mwaka 2021/22 gharama za malipo zimefikia Tsh. Bilioni 22.5, ongezeko ambalo haliendani na idadi ya wanachama wa NHIF.
Ameongeza kuwa huduma za matibabu ya figo mwaka 2015/16 ziliigharimu NHIF Tsh. Bilioni 9.5 na hadi kufikia mwaka 2021/22 gharama zimeongezeka na kufikia Tsh. Bilioni 35.44 ambapo wagonjwa wa Figo wameongezeka kutoka 280 hadi 2099.
Kwa upande wa magonjwa ya Moyo Waziri amesema mwaka 2015/16 NHIF ililipa Tsh. Milioni 500 lakini kufikia mwaka 2021/22 gharama za wagonjwa wa Moyo zimefikia Tsh. Bilioni 4.33.
Kuhusu Ongezeko la Wagonjwa Wanaohitaji Vipimo Maalum
Akitolea ufafanuzi kuhusu kuelemewa kwa Bima ya NHIF, Waziri amesema mwaka 2015/16 wagonjwa waliohitaji vipimo vya CT-Scan na MRI waliugharimu mfuko Tsh. Bilioni 5.43 lakini mwaka 2021/22 Mfuko umelipa Tsh. Bilioni 10.89 za vipimo hivyo.
Kutokana na gharama hizo, Waziri amewataka Wananchi kuchukua tahadhari ikiwemo kujua Afya zao mapema, kupunguza unywaji wa pombe, kuzingatia ulaji mzuri kwa kupunguza matumizi ya Sukari, Mafuta na Chumvi na kufanya mazoezi mara kwa mara.
Amekiri kuwa kama ongezeko la Magonjwa hayo litazidi kuwa juu, uwezekano wa Mfuko wa Bima wa Taifa (NHIF) kufa utakua mkubwa.
Chanzo cha kuelemewa kwa Bima Ya Afya
Waziri ameeleza kuwa baada ya Serikali kubadili Sheria na kuruhusu watu ambao sio Watumishi wa Umma kuingia kwenye Bima ya Afya, ndipo mwanzo wa tatizo la kuzidiwa Mfuko lilipotokea.
Amesema kuwa endapo Serikali ingeamua kuwahudumia Watumishi wa Umma pekee kusingekuwa na tatizo linalojitokeza sasa ambapo 99% ya wanaojiunga NHIF kwa hiari ikiwemo Toto Afya tayari ni wagonjwa, na ndio sababu Serikali inakuja na Sheria ya Bima ya Afya kwa wote ili kuongeza wachangiaji.
Ametolea mfano idadi ya Watoto waliojiandikisha kwenye Kadi ya Toto Afya inayogharimu Tsh. 50,400 imefikia watoto 186,000, na inapotokea kuna mgonjwa anayehitaji upasuaji unaogharimu Tsh. Milioni 1, Bima inalipa fedha hiyo bila kujali michango mingapi imelipiwa kupitia kadi hiyo.
PIA SOMA: Waziri Ummy: Bima ya Afya (NHIF) inakaribia kufa