Ni ukweli usiopingika kuwa wafugaji wetu ni muhimu sana katika kutuhakikishia kuwa tunajitosheleza kwa mazao ya mifugo kama, nyama, ngozi na maziwa. Ingekuwa ni busara zaidi kwa wizara ya mifugo kuwaelimisha wafugaji wetu namna ya kuwa na mifugo bora bila kuharibu mazingira kwani kitendo kinachofanywa na Halmashauri ya wilaya ya Kilosa hakiendani na dhana nzima ya kuwaendeleza wafugaji bali ni kuwafilisi na kuwafanya waachane shughuli hii ya kutupatia nyama na mazao mengine. Je hawa wafugaji wakiachana na ufugaji serikali inaweza kufanya kazi inayofanywa na watanzania hawa wasio na elimu na kuadhibiwa kwa kutokuwa na ufahamu?.
soma habari hii ili uone unyanyasaji wanaofanyiwa wafugaji wazalendo katika nchi yao huru chini ya serikali yao walioichagua kwa kishindo ili kuendelea kuwatetea.
soma habari hii ili uone unyanyasaji wanaofanyiwa wafugaji wazalendo katika nchi yao huru chini ya serikali yao walioichagua kwa kishindo ili kuendelea kuwatetea.
Mfugaji atozwa Sh42milioni faini ya mifugo, alipa taslimu
Na Venance George,
MMOJA wa wafugaji wa jamii ya Wasukuma, Dotto Duffu ametozwa faini ya zaidi ya Sh 42.9 milioni baada ya kukamatwa akiwa na mifugo 1,400 katika operesheni inayoendeshwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa ya kuwaondoa wafugaji walioingia wilayani humo, isivyo halali.
Akizungumza na waandishi wa habari katika zizi la serikali lililoko Mikumi wilayani hapa, Duffu alisema tayari amekwishalipa fedha hizo na kupewa stakabadhi namba 0426824.
Alisema mifugo yake mingine 100 ilikamatwa na kuhifadhiwa katika zizi lingine la serikali na kwamba alilipia faini ya Sh 11.9 milioni.
Alisema hadi kufikia juzi jioni, mifugo hiyo ilikuwa bado imezuiliwa huku akitakiwa kukodi gari, ili aisafirishe.
Pamoja na kulipia fedha zote hizo bado wamenizuia kuchukua mifugo yangu na kunitaka nitafute malori ya kusafirishia ambayo pia yataniingiza katika gharama zingine.Lakini pia ngombe hawa wakizidi kukaa hapa, nitatozwa tena faini nyingine ya Sh 5,000 kwa kila mfugo kwa siku, alisema.
Mfugaji mwingine aliyekamatiwa ngombe wake, Shibi Mlelema, alisema operesheni hiyo imemfanya kuwa masikini, baada ya kulazimika kuuza ngombe wake wote 18 waliokuwa wamekamatwa, ili kulipa faini aliyokuwa anadaiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa.
Kwa mujibu wa maelezo yake, halmashauri hiyo ilimtaka kulipa Sh 600,000 kama fidia na kwamba alilipa na kupewa stakabadhi namba 0426820.
Mlelema ambaye ni mwenyekiti wa wafugaji katika Tarafa ya Mikumi, alisema kitendo hicho kilimlazimisha kuuza mifugo yake kwa jumla ya Sh 1.4 milioni na kwamba baada ya kulipa faini hiyo alibakiwa na Sh 800,000.
Operesheni ya kukamata mifugo ya wafugaji waliohamia katika wilaya hiyo na kuhamisha kijiji cha wafugaji kilicho zungukwa na vijiji vya wakulima, inaendelea kulalamikiwa siku hadi na watu wa jamii ya wafugaji na jumuiya mbalimbali kuwa, limetawaliwa na unyanyasaji dhidi ya watu wa kundi hilo.
Wakati huo huo, vurugu zilizoambatana na operesheni inayoendeshwa na Jeshi la Polisi ya kukamata mifugo iliyoingia Kilosa, bila kufuata taratibu, zimesababisha watoto wanne wa familia moja kupotea, baada ya kukimbilia porini kwa kuogopa polisi na bunduki zao.
Akizungumza kwa masikitiko makubwa baba wa watoto hao, Dotto Duffu, alisema watoto wake ambao hawakuwahi kuwaona askari polisi wakiwa na bunduki,walishikwa na hofu na kukimbilia porini na kwamba hadi kufikia juzi, walikuwa hawajarejea.
Aliwataja watoto hao kuwa ni Sengerema, Masanja, Lameki na Shinje na kwamba juhudi za kuwasaka zinaendelea.
Source: Mwananchi