Wzanzbari Wachoshwa na kupotoshwa kiswahili

Wzanzbari Wachoshwa na kupotoshwa kiswahili

Baraghash

JF-Expert Member
Joined
Dec 18, 2012
Posts
2,713
Reaction score
1,790
Kisa cha watu wa pangoni, yaani kwa lugha ya kiarabu ‘ashaabul-kahfi’, ni miongoni mwa visa vikongwe katika historia ya dini na maisha ya mwanadamu. Kisa hiki ambacho ni moja ya visa vingi vinavyoonesha utukufu na uwezo mkubwa wa Mola wetu Muumba, Allah subhaanahu wataala, si maarufu katika uislamu tu, bali hata katika dini na jamii nyengine duniani.
Kwa muhtasari, kisa hiki kinawahusu watu wasiopungua saba, na mbwa wao, waliokimbia mateso ya utawala kandamizi katika nchi yao. Katika kimbia kimbia yao hiyo, walifika pahala wakaingia kwenye pango kujipumzisha. Hapo Mola mtukufu aliwalaza usingizi mrefu zaidi kuliko usingizi wowote aliowahi kulazwa mwanadamu na mola wake, ukitoa maiti waliokwishatangulia mbele ya haki.Watu hawa waliamka baada ya kulala kwa miaka inayosadikiwa kutimu 300 na ushei. Ambapo, walipoamka walikuwa wageni katika ardhi yao waliyozaliwa na kukulia humo. Allah akbar! Nimelazimika kukikumbuka kisa hiki kikongwe kwa kukinasibisha na maisha halisi wanayoishi wazanzibari wakiwa chini ya himaya ya Muungano. Himaya, kwa maana wakiwa chini ya uangalizi na udhibiti wa Muungano huo ambao kwa kughafilika na kulala kwao kwingi wamejikutia au watajikutia wakiamka mbali na zama za siku walizolala.Pia wameamka au wataamka wakiwa wageni katika nchi yao kama walivyokuwa ‘as-haabul-kahfi’.
Ikiwa imepita miaka 48 sasa ya Muungano, huku Zanzibar ikizidi kupoteza himaya yake na kila kitu chake, kuna kila dalili kwamba sehemu kubwa ya wahusika wa kuitetea nchi hii kuwa bado hawajaamka. Wamelala pangoni bila kujitambuwa.
Wazanzibari tumelala usingizi mnene, mzito, uliojaa mkoromo, korozo, na ndoto za mwasande(mwanamke anaemjia mwanamme ndotoni kimapenzi), tena katika bustani za Adeni. Wakati sisi tukistarehe na mwasande, wenzetu hawalali, wanakusanya kila kilicho chetu. Na yule mbwa wetu tuliemchukuwa kule pangoni, katupiwa fupa ambalo hugunya, akichoka nae hulala. Hata habweki, maskini.
Na kwa usingizi huu, tumepoteza utambulisho wetu, utaifa, mila na desturi zetu, na kila kitu. Kwa kulala kwetu huko kusikokwisha, tukipumbazwa na ndoto za mwasande, huku tukiamini mbwa wetu yupo kutulinda, bila kutanabahi hasara inayotukabili. Kumbe vile tunarudi nyuma kiamendelo huku washirika wetu wakikimbia kwa kasi ya ajabu. Kasi ambayo hata siku tukiamka, tutalala tena kwa kukata tamaa kwa walivyotuacha duni na umbali walioko wao.
Kwa sababu ya usingizi wetu mzito, Wazanzinbari ambao kiasili ni magwiji, wazawa na wamiliki halisi wa lugha ya KISWAHILI duniani, leo wanasomeshwa Kiswahili na watu wa bara. Pamoja na kasumba zinazoenezwa na wenzetu wa Kenya na Tanganyika kuwaambia wageni na kuandika vitabuni kuwa Kiswahili hakina wenyewe, ukweli unabaki kuwa wenyewe hasa ni Wazanzibari ambao hawazaliwi na lugha nyengine yoyote ukiacha Kiswahili, seuze wao wanauzungumza Kiswahili kama lugha yao ya tatu au ya nne.
Hata hivyo, sishangai sana kuwasikia wenzetu wa bara na Kenya wakisema Kiswahili hakina wenyewe. Ni kweli kiasi fulani maana kama wapo kweli Waswahili, wangesema, wangejibu, au hata kujitetea kwa njia moja au nyengine. Lakini tupo, tumelala, watu wanajivunia Kiswahili chetu na kujipatia utajiri mkubwa na shahada za juu za Elimu huku sisi tukizidi kutokwa na ‘dovuo’(madenda) kwa usingizi mzito uliotuvaa.
Ni jambo la aibu na fedheha kuona Wizara ya Elimu Zanzibar, ikiwapiga chenga wataalamu wa Kiswahili waliopo taasisi ya Kiswahili na lugha za kigeni (SUZA), na kukimbilia waandishi wa bara kuwatungia vitabu vya kufundishia Kiswahili Zanzibar. Iweje wenzetu wa bara, japo wana shahada kubwa za Kiswahili, lakini ukweli wao sio waswahili, wawe ndio mabingwa wa kutuandikia sisi vitabu vya Kiswahili? Haya sio yale ya ‘kuku kupanda basikeli na bata kuvaa raizoni’?
Ukweli tunaheshimu sana taaluma ya wenzetu na kila mtu, lakini ikumbukwe kwamba zamani vitabu vyetu vya Kiswahili ndivyo vilivyovikitumika Afrika mashariki nzima na duniani kufundishia Kiswahili. Na vilikuwa vizuri na vyenye kufunza Kiswahili cha kikweli.Lakini ukiviangalia vitabu vya Kiswahili tunavyoandikiwa bara na kamusi, ni ‘korogo-vyogo’ tu!
Sambamba na haya, kuna ombwe la vilio juu ya Kiswahili kinavyoharibiwa na wenzetu wa Kenya na Bara. Tena kwa bahati mbaya,kinaharibiwa na wale wanaoitangazia dunia kuwa wao ndio wajuzi wa Kiswahili. Ama kweli, penye vipofu, chongo huwa mfalme. Wakati sisi tumelala, wao wanajichumia na kututungia maneno yasiyokuwa na nyuma wala mbele.
Isitoshe mengi yao maneno hayo, kwa mila na desturi zetu ni matusi ya laana, lakini kwa vile hii si lugha yao hawalijui hilo.Je, tunategemea nini iwapo wao hawatajuwa mipaka, miko na itikadi ya lugha hii ambayo wenyewe wameisahau chini ya vitanda vyao walivyolalia usingizi mzito wa watu wa pangoni?
Kuna wenzetu wa bara na Kenya wametajirika kwa kufundisha Kiswahili nje ya nchi na kuandika vitabu vya Kiswahili. Japo vingi ya vitabu vyao hivyo na hasa kamusi, ni vyenye kiwango duni, lakini madamu hakuna chengine, wao ndio watatambulika. Sisi wazanzibari tupo, hatuandiki, hatuziombi kazi hizo hata zikitangazwa kiasi gani. Letu dharau nyingi tu, tukitajiwa kufundisha Kiswahili.Utasikia ‘ah! Kiswahili kitu gani? Tunawaachia wenzetu wakifaidika bure!
Leo hii kumkuta Mzanzibari anaefundisha Kiswahili nje ya nchi ni nadra. Na sijui hata kama yupo. Na kama wapo, ni mmoja kwa mia. Kiswahili kina wakenya na wabara tu kule Marekani, Uingereza, na kila pahala ni Mkenya, Mbara tu. Zanzibar tumelala, huku tukisondogewa na dume la ng’ombe lililokata kamba liitwalo Muungano bila huruma na wala hatufanyi jitihada ya kujitetea.
Pamoja na yote haya, suali hili linachangiwa na viongozi, taasisi zetu za elimu, na wasomi wa Kizanzibari waliopo. Ambao, wao ni nguvu kazi kubwa na wanaopaswa kusimama na kukikingia kifua Kiswahili, kukitetea na kukirejeashea hadhi yake.
Bahati mbaya hakuna msomi anaeandika tena hapa petu. Ukitoa wale wachache waliowakiandika hadithi na mashairi siku hizo, hakuna mwengine. Na bahati mbaya hawa pia vitabu vyao haviingizwi katika silabasi ya bara kwa madai Kiswahili chao ni kigumu, hakimo katika kamusi zao.
Lakini yote haya ni kwa sababu hapana Kiongozi anaelipa kipaumbele suali hili. Ndio maana ukaona hata ile TAKILUKI pale SUZA, imedorora. Haichapishi, haiandiki kitu, inasubiri tuandikiwe kamusi na vitabu kutoka bara. Kamusi zenye maneno ya kikabila, mengi yakiwa ya matusi, yasiyoingia akilini, tuwafundishe watoto wetu. Kule Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA), japo wametoa kamusi lakini ni la lugha moja tu, halikidhi haja. Pia wanaonekana kufunikwa sana na wenzao wa kule bara.
Kwa kweli, ipo haja kwa Serikali, viongozi, wasomi, na taasisi husika Zanzibar kulivalia njuga suali hili. Kwani Zanzibar kama Zanzibar, tumeshapoteza vingi katika Muungano, na ni vigumu kuvirudisha tena. Basi na hili la Kiswahili kuna dalili ya kukipoteza. Kiswahili, lugha ya mama na baba zetu. Lugha ya wahenga wetu, utu wetu, na utambulisho wetu? Hatuoni hata kimeme, tunakiacha kikifaidisha watu wengine. Bado tumelala tu.
Tuamkeni Wazanzibari, tujiandikie vitabu vyetu, kamusi zetu. Kamusi zinazosawiri muktadha wa mazingira na tamaduni zetu. Vitabu, vyenye kuandika Kiswahili chetu na sio chao. Hili tunaweza na halihitaji, tume ya Warioba kamwe. Hivi hatuoni aibu, hata Kiswahili tufundishwe na bara? Tuamke, Inatosha, kwani ‘Mwana mtambuwa shibae, hashibiwi’.
 
Back
Top Bottom