Mdomo umeachama, dafu unalisifiya!
Mbona sina la kusema, macho yananipwaiya,
Yote uwezayo chuma, dafu walikumbatia,
Kamwe dafu sitokula, sababu zangu nakupa.
Mti wake ni mrefu, kukwea mimi siwezi,
Kimo kinanipa hofu, wa kijiji si mkwezi,
Bora ni yale matofu, kufua dafu siwezi,
Kamwe dafu sitokula, sababu zangu nakupa.
Namkumbuka Salumu, ati ataka madafu,
Akajifanya mwalimu, madafu akiyasifu,
Kaukwea kitalaamu, mnazi wa Bwana Sefu,
Kamwe dafu sitokula, sababu zangu nakupa.
Mwisho akafika juu, meno katukenulia,
Akakunjua miguu, huku akishangilia,
Mara chini huyo puu!, wenzake tukakimbia,
Kamwe dafu sitokula, sababu zangu nakupa!
Miguu imevunjika, imetokea begani,
Mbavu zikaparanyika, zimetokea kiunoni,
Damu imetapanyika, kamrudia Manani,
Kamwe dafu sitokula, sababu zangu nakupa!
Sasa yote ni ya nini, madafu kuyatafuta,
Zabibu mbona laini, adhabu hutoipata?
Ukishika vidoleni, mdomoni wazileta,
Kamwe dafu sitokula, sababu nakupa!
Kwanza nina sikitiko, kwa habari ya maziko,
Salumu huko aliko, Mola mpe pumziko,
Nasi tutafika huko, tutote huku tuliko,
Tunda zuri ni lolote, ulilojichagulia.
Pili ninamlaumu, nafsi kuihujumu.
Si mjuzi maalumu, ukwezi haufahamu.
Yeye hakuwa mwalimu, kwa nini kujituhumu?
Tunda zuri ni lolote, ulilojichagulia.
Vipi kukwea minazi, na yeye sio mjuzi?
Alikuwa mwanafunzi, hadi kutokwa pumzi,
Hajaupata ujuzi, aparamia minazi,
Tunda zuri ni lolote, ulilojichagulia.
Lo! Masikini Salumu, fani umeipa doa,
Watu wanakulaumu, kwa ulivyojiondoa,
Hujawa mtaalamu, wala hukupata ndoa,
Tunda zuri ni lolote, ulilojichagulia.
Nikirudi kwenye dafu, nabaki muaminifu,
Kwa mapenzi yakinifu, sitoacha langu dafu,
Wala halitonikifu, sasa na hata halafu,
Tunda zuri ni lolote, ulilojichagulia.
Hapa nimepata funzo, katika hili gumzo,
Kumbe tunda ni matunzo, kila siku tangu mwanzo,
Kwa raha na matatizo, imara weka mawazo,
Tunda zuri ni lolote, ulilojichagulia.
Tunda zuri ni lolote, unalomezea mate,
Bara na pwani upite, kushoto kulia kote,
Kiona wameza mate, tia nanga usisite,
Tunda zuri ni lolote, ulilojichagulia.
Mwingine apenda tende, we waweza usipende,
Neemah ala kwa mbinde, tena kwa shingo upande,
Bora milima apande, akashindie makande,
Tunda zuri ni lolote, ulilojichagulia.
Nyani Ngabu kwa machenza! ala akichezacheza,
Kelly atampokeza, huku akimkonyeza,
Mengine atayasaza, aweke juu ya meza,
Tunda zuri ni lolote, ulilojichagulia.
Mapera atayabeza, eti kula hatoweza,
Kisa yanamtatiza, harufuye yamkwaza,
Tena yanampa giza, ashindwa hata kuwaza,
Tunda zuri ni lolote, ulilojichagulia.
Balantanda na embe, mwenyewe aita dodo,
Atakula na atambe, mbele yake hondohondo,
Ngoja sasa ajilambe, anatia madoido,
Tunda zuri ni lolote, ulilojichagulia.
Suki mpatie ndizi, anageuka mchizi,
Utamu amemaizi, asahau hata kazi,
Usizitaje kunazi, za Kibunango mjuzi,
Tunda zuri ni lolote, ulilojichagulia.
Wewe zako ni zabibu, hupendi kuziharibu,
Zina thamani ajabu, kama ilivyo dhahabu,
Kwa imani yako babu, magonjwa zinayatibu,
Tunda zuri ni lolote, ulilojichagulia.
Salamuni ndugu zangu, wala Sangara na Changu,
Tunda la mtu si langu, nalipa heshima chungu,
Msidharau wanangu, heshimuni walimwengu,
Tunda zuri ni lolote, ulilojichagulia.
JF kuna raha, vipaji twakumbukia,
Twawaona wa madaha, na wale wa kurukia,
Wamakonde pia Waha, wote wote waingia,
Tunda zuri ni lolote, ulilojichagulia.