Wananchi wa Mkoa wa Kagera wamejitokeza kwa wingi katika kliniki ya ardhi iliyofanyika mkoani humo, ambapo huduma mbalimbali za sekta ya ardhi zimetolewa, ikiwemo utoaji wa hati za miliki za ardhi na utatuzi wa migogoro.
Katika kliniki hiyo, zaidi ya hati 100 za miliki za ardhi zimetolewa kwa wananchi waliofika kupata huduma, hatua inayotekelezwa ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kusogeza huduma karibu na wananchi na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili katika sekta ya ardhi.
Akizungumza katika zoezi hilo, Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Kagera, Florida Busheni, amesema kumekuwa na mwitikio mkubwa kutoka kwa wananchi, ambapo kila mmoja amepata fursa ya kuhudumiwa kulingana na mahitaji yake.
“Kwa upande wa Mkoa wa Kagera, mwitikio katika kliniki ya ardhi umekuwa mkubwa na wenye mafanikio. Wananchi wameitikia, wamekuja kwa wingi na tumefanikiwa kutoa hati zaidi ya 100. Pia tumeweza kutoa huduma mbalimbali za ardhi, ikiwemo utatuzi wa migogoro na kuwasikiliza wananchi kuhusu changamoto zao,” amesema Florida.
Mbali na utoaji wa hati na utatuzi wa migogoro, kliniki hiyo imetumika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu masuala mbalimbali ya kisheria na usimamizi wa ardhi, ikiwemo ulipaji wa kodi ya pango la ardhi, huku wananchi wakipata fursa ya kukutana na wataalamu na kupata ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili.
Katika hatua nyingine, Florida amesema kliniki hiyo imekamilika kwa mafanikio makubwa, huku akiwashukuru wananchi wote waliojitokeza kupata huduma pamoja na watumishi walioshiriki katika kufanikisha zoezi hilo, ambalo limechangia kuongeza uelewa na kupunguza kero za ardhi mkoani Kagera.