Zifahamu aina 9 za wateja ili ukuze biashara yako

Zifahamu aina 9 za wateja ili ukuze biashara yako

Ben Zen Tarot

JF-Expert Member
Joined
Dec 13, 2014
Posts
4,298
Reaction score
7,612
: Mteja ni nani? Mteja ni mtu yeyote anayenunua bidhaa au huduma inayotolewa na biashara fulani. Mteja ni mtu muhimu sana katika biashara yoyote. Lengo la kuanzisha biashara ni kupata wateja watakaonunua bidhaa au huduma yako. Biashara yoyote isipopata wateja bora na wa uhakika, ni wazi kuwa haiwezi kufanikiwa; itakufa tu. wafanyabiashara wengi hawawafahamu wateja vyema, hivyo kutokuwamudu vyema; jambo ambalo huwakwamisha kufikia malengo yao.

Ikiwa wewe ni mfanya biashara tayari au unataka kuanza kufanya biashara, karibu nikushirikishe aina 9 za wateja unazoweza kuzitumia kukuza biashara yako.

1. Wateja wapya Hawa ni wateja ambao huja kwenye biashara yako kwa mara ya kwanza, mnaweza kuwa mnafahamiana nje ya biashara, lakini hamjawahi kuhudumiana kwenye biashara. Mteja huyu huja kwa lengo la kupata huduma pamoja na kuifahamu biashara husika ili kuona sababu itakayomfanya awe mteja wa biashara hiyo. Wewe kama mfanyabiashara, hutakiwi kufanya kosa kwa aina hii ya mteja; hakikisha mteja huyu anaifahamu biashara yako vyema na anapata sababu za kutosha za kuanza kuwa mteja wako wa kudumu. Unaweza kufanya haya yafuatayo kwa mteja huyu: Mpe maelezo kuhusu bidhaa au huduma unazotoa katika biashara yako. Mpe ofa ya ukaribisho.

Onyesha sura na lugha nzuri itakayo mfanya aone ujio wake mpya umethaminiwa sana. Ikiwa inawezekana au atahitaji, mpe mawasiliano ya biashara yako pamoja na muda wa utoaji wa huduma. Ikiwa mteja huyu amehama kutoka kwenye biashara nyingine, basi dodosa ni sababu gani zimemfanya ahame. Mara nyingi wateja waliohama husema wao wenyewe kuwa kule walikokuwa walipata changamoto kadha wa kadha hivyo sasa wameamua kuwa wateja wako. Mf. Utasikia mteja akisema “Kule kwenye lile duka fulani wanajisikia sana.”, “Yule muuzaji anauza vitu ghali sana.” n.k. Yachukue haya kama somo la kuboresha huduma yako. Soma pia: Mbinu 10 za Kuongeza au Kuvutia Wateja Kwenye Biashara

2. Wateja watafutao punguzo Hii ni aina nyingine ya wateja ambao huja kwenye biashara yako wakiwa katika safari yao ya kutafuta punguzo la bei kwenye huduma au bidhaa wanayoitafuta. Mara nyingi wateja hawa wanaweza kutekwa na punguzo dogo sana ambalo hata wewe mwenyewe usingedhani kama linaweza kumshawishi mteja kununua huduma au bidhaa yako. Jambo muhimu hapa inabidi ujue kucheza na bei za bidhaa vizuri, ni bora ukose hata shilingi hamsini au miamoja kwenye faida yako lakini uwapate wateja wa aina hii. Kwa mfano kuna mteja anaweza kuacha kununua gesi kwenye duka inapouzwa shilingi 20,000 na kwenda kununua wanapouza 19,850 au 19,900. Hivyo, ni muhimu kuwaelewa wateja hawa ili uwapate na ukuze biashara yako.

3. Wateja watiifu au wakudumu Hawa ni wateja ambao uko nao kila mara, hawa ndio wateja wakuu uliowazoea na waliokuzoea wewe. Hawa ni wateja muhimu ambao wanapaswa kuthaminiwa na kuhudumiwa vyema. Mara nyingi wateja hawa wanakuamini na wanaamini huduma na bidhaa ile unayoitoa.

Tabia kuu za wateja wa kudumu: Wateja hawa hawahamishwi kirahisi, hata kunapokuwa na mterereko wa huduma au bei wengi wao huvumilia. Hupenda kutoa ushauri na mapendekezo kuhusu biashara na huduma kwa kuwa hujihisi kuwa nao ni sehemu ya biashara husika. Mara nyingi huwa mabalozi wema wa biashara husika. Hupenda kuacha pesa zao kwako na kukopa. Hivyo basi, wewe kama mjasiriamali hakikisha unaongeza thamani ya huduma kwa wateja hawa ili kujenga msingi imara wa wateja kwa ajili ya biashara yako.

4. Wateja mabalozi Ingawa wateja watiifu au wakudumu wanaweza kuwa mabalozi wa biashara yako; sifa hii hujidhihirisha zaidi kwa wateja wale ambao hasa sifa yao kuu ni ubalozi. Wateja ambao ni mabalozi wanaweza wasiwe ni wateja wa mara kwa mara, lakini wakawa mabalozi wazuri au wabaya wa ile huduma au bidhaa unayouza. Wateja hawa hupenda kuwashirikisha watu wengine sifa za biashara yako ikiwa ni nzuri au ni mbaya. Wateja hawa huleta marafiki, majirani au hata wanafamilia wao kwenye biashara yako ikiwa wameridhishwa na huduma unayotoa. Vivyo hivyo, ikiwa wateja hawa hawakuhudumiwa vizuri, wataeneza sifa mbaya ya huduma au bidhaa unazouza. Hivyo, ni muhimu kuwabaini wateja hawa na kuhakikisha tabia yao ya ubalozi inabeba mbegu au sifa njema kutoka kwenye biashara yako. Mambo unayoweza kufanya ili kuhimiza wateja kuwa mabalozi wa biashara yako: Toa huduma nzuri ambayo mteja hataisahau au kuona aibu kuitaja kwa mtu mwingine. Toa ofa na punguzo. Mshukuru mteja pale anapokuletea mteja mpya. Tumia lugha nzuri itakayo kufanya uwe mfano. Kumbuka! Inawezekana kumfanya kila mteja awe balozi mwema wa biashara yako.

5. Wateja watafiti Hii ni aina ya wateja ambao hufanya manunuzi baada ya kupata taarifa za kina kuhusu bidhaa au huduma ile wanayoitaka. Hebu tutazame mfano huu:

(Mteja A na Muuzaji A) Mteja A: “Habari, kuna losheni ya kuondoa chunusi?” Muuzaji A: “Ipo ya Aloe Vera shilingi elfu tano, nikupe ngapi?” (Mteja A na Muuzaji B) Mteja A: “Habari, kuna losheni ya kuondoa chunusi?”

Muuzaji B: “Ndio ipo, unataka ya wanaume au ya wanawake?” Mteja A: “Ya wanawake” Muuzaji B: “Ipo ya Aloe Vera ile OG, hii inaondoa chunusi na haichubui ngozi kabisa, tena nitakushauri jinsi ya kuichanganya ili ikubali zaidi ngozi yako.” Mteja A: “Unauzaje?” Muuzaji B: “Moja ni shilingi elfu tano, ila ninaweza kukupunguzia kidogo….ukinunua nyingi pia nitakupunguzia zaidi.” Kwa kutazama hayo mazungumzo hapo juu unafikiri mteja A atanunua losheni kwa muuzaji A au B? Ni wazi kuwa atanunua kwa muuzaji B kwa sababu anajua kunadi bidhaa yake vyema kwa kuhakikisha mteja anapata maelezo ya kutosha ya bidhaa na bei. Fahamu vyema huduma na bidhaa unazouza, haifai mteja kuja kwako na kukuuliza kuhusu huduma au bidhaa zako ukashindwa kumpa maelezo ya kuridhisha. Kumbuka kuwa wateja watafiti wanataka kupata maelezo ya kina kabla hawajafanya manunuzi.

6. Wateja wapitaji Hawa ni wateja ambao huja kwenye biashara yako mara moja tu, na si rahisi kuja tena mara nyingine au karibuni. Mara nyingi wateja wa aina hii huwa ni wasafiri au watu walioletwa kwenye eneo lako la biashara kutokana na tukio fulani kama vile msiba au sherehe. Ingawa wateja hawa ni wapitaji, unapaswa kuwahudumia vyema kwani hujui kesho itakuwaje. Ili kuwapata wateja hawa ni vizuri kujenga jina jema katika eneo husika ili mteja mgeni afikapo katika eneo unalofanyia biashara akubaini wewe kwanza kabla ya kumbaini mfanyabiashara mwingine.

7. Wateja walalamikaji Hii ni aina ya wateja ambao wanapenda kulalamika na kulaumu sana. Si rahisi kuwaridhisha wateja hawa kwani wao kila kitu kwao ni tatizo. Hata hivyo, pamoja na tabia yao hii, bado utaendelea kuwaona wakija kila mara. Ukimpunguzia bei atasema ni mbinu ya kumvuta umuibie, ukimweleza ubora wa bidhaa atakuambia unamrubuni ili anunue, ukimwambia bei za vitu zimepanda atakuambia unamdanganya…n.k. Wateja hawa kamwe huwezi kuwaridhisha kwani kila mara huona kuwa mfanyabiashara si mwaminifu au anapata faida kubwa sana kwa ujanja ujanja. Kwa kuwa wateja hawa hupenda kuongea sana, ni muhimu ukaangalia jinsi ya kutumia hekima kuwajibu na kuwahudumia ili wasije wakaeneza sifa mbaya kwa wateja wengine.

8. Wateja wasiokuwa na mpango wa manunuzi Je umewahi kununua kitu sokoni au dukani ambacho hakikuwa kwenye mpango wako wa manunuzi kwa kuwa tu umekiona au mtu mwingine amekushawishi kukinunua? Au umewahi

kusikia mtu akisema nimenunua hiki kitu kwa sababu nimekuta kinauzwa bei nzuri nikaona nisikiache? Ikiwa jibu ni ndio, wewe au huyo mtu mwingine wote mlikuwa wateja wasiokuwa na mpango wa manunuzi. Wateja hawa hufanya manunuzi ambayo hawakuyapanga awali; mara nyingi hufanya manunuzi kutokana na tamaa ya macho au ushawishi wa marafiki au muuzaji. Ikiwa wewe ni mfanyabiashara mwenye ushawishi na unayejua kunadi bidhaa zako vyema, ni rahisi sana kuwapata wateja wa aina hii kwani utaweza kuwashawishi wateja ambao hawakuwa na malengo ya kununua bidhaa zako wazinunue. Soma pia: Njia 9 za Kutangaza Biashara Yako Bila Pesa

9. Wateja wanaotafuta ubora Kutokana na hali ya ugumu wa maisha, wateja wa aina hii ni wachache sana. Wateja wanaotafuta ubora ni aina ya wateja ambao wao hawaoni shida kutumia gharama kubwa kutafuta bidhaa yenye ubora wanaouhitaji. Wateja hawa hawatishiwi na bei wala hawapendi kuomba punguzo, wanachozingatia ni ubora wa bidhaa au huduma wanayoitaka. Je, umewahi kujiuliza inakuwaje mtu anaacha kiatu cha ngozi cha shilingi 50,000 na kwenda kununua kiatu cha ngozi cha Italia chenye thamani ya zaidi ya shilingi 650,000? Hii ni kutokana na sababu kuwa mteja huyu anataka ubora wa bidhaa yake. Ikiwa unataka kuwapata wateja wa aina hii, basi zingatia kuweka bidhaa za bei tofautitofauti kwenye biashara yako. Kumbuka, bidhaa za bei ghali zinatakiwa kuwepo kwa uchache na baada ya kufanya tathimini kubwa kwani mzunguko wake ni mdogo sana kutokana na uchache wa wateja wake.

Hitimisho Kwa hakika naamini umejifunza mengi kuhusu aina hizi 9 za wateja nilizozieleza katika makala hii. Bila shaka wateja ni watu muhimu sana kwenye biashara yoyote. Hivyo, kumfahamu mteja ni ufunguo muhimu wa mafanikio ya biashara yako. Je wewe uko kwenye kundi gani la wateja? Je wateja wako wengi wako kwenye kundi gani? Je kuna aina mbayo unaifahamu lakini sijaisema?
 
Aina zote 9 nimezielewa na nimezizingatia vyema, sema hiyo namba 5 ndio nimeipenda na kuvutiwa nayo zaidi. Asante kwa darsa mkuu, nasema ubarikiwe sana kwa haya uliyoandika hapa.
 
Ubarikiwe sana, umeelezea vizuri hizi aina za customers, mimi nandondokea hapo kwa mteja mtafiti. Lakini hizi aina nyingine naona zitanisaidia kwenye shughuli zangu za kila siku.
 
Hapo namba 7,kuna mteja alikuja dukan kwa mara ya kwanza akauliza bei ya kuku wa kisasa nikamwambia 7500 kwa 8000 aliruka almanusuru avunjike kiuno eti ooh mbona wenzio wanauza 6500 kwa 6800. Nikamuonesha kuku akakataa kununua akaondoka,dakika 20 mbele karudi akasema nipo huyo wa 7500. (siku nyingine) kaja tena nipe kuku wa 7500 nikampa basi ndo akaanza kuongea ooh !kule nilienda (huku anajishtukia maana siku ile aliongea sana juu ya biashara na kusema mimi sijui biashara naweka bei za ovyo na bla bla kama hivo) nikakuta kikuku kama njiwa wadogo yaan hata 1kg hawafiki akaenda tena bucha maarufu la kisasa full vioo akakuta kuku 8000 wangu wa kubwa ndo ikabidi arudi kwangu.Mimi nikacheka kidogo na kumwambia karibu sana mteja wangu mpya,mpaka leo ni mteja ila bado kila akija lazima atake kupunguziwa bei yaan wateja wengine ni headache sana
 
Back
Top Bottom