Kiongozi mstaafu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, ameendelea kufuatilia mwenendo wa kesi zinazopinga matokeo ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji, ambazo chama hicho kimefungua katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumza katika Mahakama ya Wilaya ya Hakimu Mkazi Kigoma, tarehe 10 Februari 2025 Zitto ameituhumu serikali kwa kuweka mapingamizi yasiyo na msingi ili kuchelewesha mchakato wa kusikilizwa kwa mashauri ya msingi.
"Kuna vipingamizi vya ajabu vinavyowekwa kwenye kesi hizi kwa makusudi ili kuzuia haki ya wananchi kutendeka. Tunaitaka Mahakama Kuu kuhakikisha kuwa haki inatendeka bila kuingiliwa," amesema Zitto.
Katika mkoa wa Kigoma, ACT Wazalendo imefungua kesi 13 kupinga matokeo ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa, huku hadi sasa chama hicho kikiwa kimeshinda mapingamizi katika kesi moja, huku kesi nyingine zikiendelea kusikilizwa.
Zitto amesisitiza kuwa chama hicho hakitosita kufuata haki hadi ngazi za juu za mahakama ikiwa haki haitapatikana katika mahakama za ngazi za chini.
"Tutahakikisha tunasimamia haki za wananchi, kurudisha heshima ya kura zao, na hatutakubali kuona haki inapotewa au kupuuzwa," ameongeza.
Aidha, amesema ACT Wazalendo itaendelea kupambana kulinda demokrasia nchini na haitarudi nyuma katika kuhakikisha kuwa matokeo halali ya uchaguzi yanaheshimiwa.