Zombe kuachiwa...

Inavyojulikana Judge Masati si mchezo. Yuko strict sana. Ningeshangaa kama Zombe angeachiwa!!!!! Katika hao 9 ni lazima pia kila mtuhumiwa apate hukumu kulingana na ushiriki wake. Japo mlenga shabaha bado hajapatikana but naamini siku ya hukumu mambo yatakuwa mazito. Tusubiri utetezi wao.
 
*Zombe akutwa na Tuhuma za Kujibu
*Wenzake wa Tatu Waachiwa Huru Leo

Habari zilizofikia blog hii hivi punde kutoka mahakama kuu ya Tanzania zinasema,Kesi ya mauaji ya kukusudia,inayomkabaili aliyekuwa mkuu wa upelelezi mkoani Dar es salaam,RCO, Abdallah Zombe(Pichani Juu)na askari wenzake 12 imeendelea leo mahakama kuu jijini Dar es Salaam ambapo Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Abdallah Zombe na wenzake wamekutwa na Mashtaka ya kujibu ambapo watuhumiwa wengine watatu katika kesi hiyo wameachiwa huru leo baada ya kutokutwa na Mashtaka ya kujibu..

Source: Hakingowi blog!
 
 

Wandugu kesho ya jana si ndio leo, mbona no updates? nini kimejiri hapo Kisutu?
 
Kama shitaka ni moja tu la murder, ushahidi hauonyeshi muuaji ni nani kati ya watuhumiwa. Inavyoonyesha ushahidi wa kwamba waliouawa walikamatwa na wahusika, na wakapatikana wameuawa. Hilo tuiachie Jury. Walioachiwa inaonekana ni madreva ambao gari yao iliharibika kwa hiyo hawakufika huko....
 
Wakuu ksei ipo mahakamani,na mahakam ni moja ya miimili ya dola Tanzania, ni chombo huru katika utendaji wake na maamuzi.

Na mahakama inafuata na kutekeleza kanuni,sheria na taratibu za nchi yetu kwa dhana ya kutekeleza utawala bora na utawala wa sheria ambapo Tanzania iko juu katika kutekeleza haya.

Sasa si vyema kuingilia huru huu wa mahakama na ni kosa kisheria kfanya hivyo.

watanzania tuwe na subira kwa masuala yote ambayo yapo mahakamani kwani sheria itachukua mkondo wake bila kujali rangi,cheo,dini wala uvigogo n.k.

i always emphasize speed in wroung direction is irrelevant.

Thx
 
Zombe alia kortini Dar


na Happiness Katabazi




KATIKA hali isiyotarajiwa aliyekuwa Kamanda wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Abdallah Zombe (55), jana aliangua kilio mara kadhaa kizimbani wakati akijitetea dhidi ya kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu na dereva teksi mmoja.

Licha ya Zombe kumwaga chozi mara nne akiwa kizimbani, pia alikuwa akitoa utetezi wake akionyesha kujiamini na kunukuu baadhi ya vifungu vya Sheria ya Jeshi la Polisi (PGO), Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya 1985 na Sheria ya Ushahidi.

Akitoa utetezi wake kwa zaidi ya saa nne (saa 4:28 hadi saa 8:06 mchana), Zombe alidai kushangazwa na shahidi wa 36, SACP Sidney Mkumbi, kuidanganya mahakama kuwa alikataa kuhojiwa.

Alidai Mei 29 mwaka 2006, aliitwa ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) na Mkumbi na kuelezwa aandike maelezo na kudai alihoji ni kwa nini aandike maelezo mara ya pili. Alidai alijibiwa kuwa maelezo ya awali hayakuwapo kwenye jalada.

“Napingana na Mkumbi kuniambia nilikataa kuchukuliwa maelezo, kwani mara ya kwanza ilikuwa ni Machi 3, mwaka 2006, niliandika maelezo yangu kwenda kwa IGP kuhusu tukio hilo la mauaji,” alidai Zombe na kuwasilisha nyaraka hizo mbili za maelezo yake, ili zitumike mahakamani kama kielezo.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya wakili Jerome Msemwa na Zombe.

Wakili: Shahidi unatambua unakabiliwa na kosa gani?

Shahidi: Natambua, ninakabiliwa na kesi ya mauaji ya watu wanne, ila marehemu siwafahamu kabla, wakati na baada ya vifo vyao.

Wakili: Hebu tuambie ilikuwaje?

Shahidi: Juni 6 mwaka 2006 nikiwa ofisini Makao Makuu ya Polisi niliitwa kwa IGP Said Mwema ambaye alikuwa na makamishna wawili, Kamishna wa Mafunzo, Paul Chagonja na Tweve.

Wakili: Baada ya hapo ilifuata nini?

Shahidi: IGP Mwema aliniambia siku hiyo ningeunganishwa kwenye kesi ya mauaji ya watu wanne. Na wakati akinieleza hayo aliniambia DPP amemwandikia barua kwamba mimi natakiwa kushitakiwa.

Mwema alinipa hiyo barua ya DDP ilikuwa ni barua ya Juni 6 mwaka 2006 ikiwa na kumbukumbu namba DAC/C180/3/DAR/1565/11/2006 ambayo iliandikwa kwa DCI na kwamba DDP alifikia uamuzi huo kwa sababu ushahidi uliopo kwenye jalada unanigusa moja kwa moja mimi.

Wakili: Unakubaliana na yaliyoandikwa kwenye barua hiyo?

Shahidi: Sikubaliani nayo, kwani yamepangwa, kwani huyu DPP aliandika barua kwa mshitakiwa wa 3, 4, 7, 9 na 10 tuliokuwa nao gereza la Ukonga na hawa ndio walimuandikia barua DPP.

Wakili: Una ushahidi wa hizo barua za washtakiwa walizomwandikia DPP?

Shahidi: Ndiyo, hizi hapa (anaonyesha). Ziliandikwa Juni 3 mwaka 2006, ikiwa ni miezi sita tangu washtakiwa hao wakamatwe na kuwekwa rumande.

Wakili: Hizo barua za watuhumiwa wenzako kabla ya kwenda kwa DPP zilipitia kwa mkuu wa gereza?

Shahidi: Zilipitia kwa mlango wa panya, yaani hazikupitia kwa mkuu wa gereza.

Wakili: Kwa ufahamu wako barua za mahabusu zinapaswa zipitie wapi?

Shahidi: Kwa mkuu wa gereza.

Wakili: Connection ya barua za DPP na washtakiwa wenzako katika kesi hii ikoje?

Shahidi: Wakati nikiwa RCO nilifungua kesi za madai ya kashfa dhidi ya magazeti sita mahakamani na hadi sasa hazijaanza kusikilizwa.

Wakili: Unazikumbuka kesi hizo na namba zake na magazeti uliyoyafungulia?

Shahidi: Ndiyo, nilifungua kesi dhidi ya gazeti la Alasiri, Tanzania Daima, Halihalisi sasa Mwanahalisi, Mwananchi, Mzalendo na Dar Leo. Nadai jumla ya sh bilioni moja kwa kila gazeti.

Wakili: Ulisema hao marehemu walifariki lini?

Shahidi: Januari 16 mwaka 2006, saa 12 jioni.

Wakili: Wakati huo ukiwa na wadhifa gani?

Shahidi: Kaimu RPC na RCO, ila nilikuwa na wasaidizi sita katika nyadhifa hizo.

Wakili: Kwa upande wa cheo chako cha RCO ulikuwa ukisaidiwa na maofisa gani?

Shahidi: Kwa sasa amepanda cheo ni ACP Charles Mkumbo ambaye alikuwa ni Kiongozi wa Kudhibiti Ujambazi jijini, SSP Nyanda, SP Lulu, ASP Kisai hawa wote walikuwa wakinisaidia.

Wakili: Ulikuwa na kazi maalumu wakati unakaimu cheo cha RPC?

Shahidi: Kwa kipindi hicho, nilikuwa nikiongoza msafara wa Rais Jakaya Kikwete katika Pilot Car, ambapo rais alipoingia madarakani alikuwa na ziara ya kutembelea wizara zote. Nilikuwa nikiongoza msafara kuanzia Januari mosi hadi 30 mwaka 2006 nilipomkabidhi ofisi Kamanda Alfred Tibaigana na kwenda Rukwa kwenye ofisi yangu mpya.

Wakili: Majukumu ya kila siku alikuwa anatekeleza nani wakati upo kwenye ziara ya Rais Kikwete?

Shahidi: Upande wa ofisi ya RPC ni SSP Mafie na wenzake watano ambao nimewataja na kama jambo limetokea walikuwa wakikabiliana nalo.

Wakili: Kwenye ofisi ya RCO nani anakusaidia wakati haupo?

Shahidi: SSP Mkumbo.

Wakili: Katika wadhifa huo ulikuwa unapata taarifa za uhalifu kutoka kwa wasaidizi wako?

Shahidi: Walikuwa wananipa taarifa ingawa si zote, kwani nyingine walikuwa wakinijulisha.

Wakili: Kipolisi Mkoa wa Dar es Salaam una wilaya ngapi?

Shahidi: Wilaya tano za kipolisi.

Wakili: Wilaya ya Kinondoni ilikuwa inaongozwa na nani?

Shahidi: Edward Maro.

Wakili: Hao viongozi wa wilaya kipolisi wanawajibika kwa nani?

Shahidi: Kwangu.

Wakili: Kuna sheria yoyote inamzuia RPC kwenda vituo vya polisi?

Shahidi: Hakuna, kwani vituo hivyo ni nyumba za serikali.

Wakili: Turudi kwenye tukio lililopo mahakamani, kuna ushahidi ulitolewa kwamba siku hiyo ulikwenda Kituo cha Urafiki, ulikwenda kufanya nini?

Shahidi: Siku hiyo mke wangu ambaye yupo hapa mahakamani alikuwa anaumwa tumbo na alikwenda Hospitali ya TMJ kwa kutumia teksi kutoka Mtoni Kijichi hadi hospitalini na alipofika alinipigia simu nikamchukue. Ilipofika saa 1:30 jioni nilikwenda hospitalini hapo na dereva wangu Station Sergeant Alifa, ambaye alibaki ndani ya gari na simu ya upepo (Radio Call).

Ghafla dereva alinifuata na kuniambia OCD wa Magomeni, Mentare ananiita kwenye Radio call. Nilipozungumza naye alinitaka niende Kituo cha Polisi Urafiki, ili nikamsaidie kutatua tatizo. Nilipofika Urafiki nilimkuta Mkumbo, Bageni, Ndani na Ahmed Makele.

Wakili: Walikuambia nini?

Shahidi: Mantare aliniambia Bageni na Makele walikuwa wametoka kwenye tukio la wizi la BIDCO ambapo zimeporwa sh 5,750,000 na walikuwa na sh milioni tano, hivyo kama milioni moja haipo. Akaniambia kuwa ni maofisa wakubwa, nimsaidie jinsi ya kupata fedha zilizosalia.

Hata hivyo, nilimweleza nina mgonjwa na nilishangaa kuniambia nimsaidie wakati wamesema wameishapata fedha na inakuwaje viongozi wa polisi waibe vielelezo. Ndipo mtukufu jaji, nilipokasirika.

Wakili: Eeh nini kilifuata?

Shahidi: Nikamweleza OCD Mantare kama ameshindwa kutatua hilo tatizo, basi ameshindwa kazi na nikamwambia mpaka kufika asubuhi fedha hizo zikiwa hazijapatikana watawajibishwa. Kesho yake Bageni alikuwa na fedha ambazo jana yake walisema hazionekani na walieleza zilikuwa ndani ya gari.

Wakili: Uliviita vyombo vya habari kuvieleza hilo?

Shahidi: Niliviita na wakaja na miongoni mwao ni mwandishi wa Tanzania Daima, Happiness Katabazi na Faustine Kapama wa Daily News, na nikawaeleza kazi nzuri iliyofanywa na polisi ya kukamata majambazi ya BIDCO.

Wakili: Taarifa za mapambano ya askari wako na majambazi ulizipata wapi?

Shahidi: Ni OCD ndiye aliyeniambia majambazi hao wameuawa, kwani walipambana na polisi na miili ilikuwa imepekekwa Muhimbili.

Na baada ya kelele nyingi kupigwa na wananchi IGP aliunda tume iliyoongozwa na Mgawe.

Wakili: Lini tume hiyo ilienda eneo la tukio?

Shahidi: Januari 19 mwaka 2006. Mimi na tume hiyo tulikwenda Sinza kukagua. Katika ripoti yake, Mgawe alisema haijakamilika, lakini nimetumia ukachero wangu nimeipata ripoti ya tume hiyo mwisho imeandikwa ‘Hitimisho’. Naomba maneno yaliyopo kwenye ripoti hiyo yatafsiriwe kama yalivyo.

Wakili: Kwenye tume ya Mgawe uliambiwa ufanye nini baada ya ripoti?

Shahidi: Haikuniambia nifanye nini. (Zombe alianza kububujikwa machozi). Tume haikunigusa, mimi nimeguswa na Tume ya Mkumbi. Na ninashangazwa Rais Kikwete kuingizwa katika kesi hii, kwani alisema ni askari 15 ndio wachukuliwe hatua na katika hao jina langu halikuwepo.

Wakili: Mama Mkumbi alisema wewe ulikataa kutoa maelezo ni kweli?

Shahidi: Si kweli, ila ilikuwa ni njia ya kutapatapa kwani nilikuwa nimewashika pabaya.

Wakili: Ni hatua zipi zinachukuliwa kwa mtu ambaye hataki kuchukuliwa maelezo yake na polisi?

Shahidi: Mtuhumiwa anayekataa kutoa maelezo mbele ya askari, Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai inamruhusu askari kuandika jina la mtuhumiwa na anwani yake, kisha naandika Question Statement, halafu naandika tarehe na saini yangu na ya mtuhumiwa.

Wakili: Yote hayo Mkumbi aliyafanya kwako?

Shahidi: Alipoulizwa na wakili wangu Moses Maira mahakamani hapa alisema mimi nimekataa na alipoulizwa alifuata taratibu, alisema hakuzifuata. Mimi ni mpelelezi mkubwa nimesomea ukachero zaidi ya nchi tatu, pia sheria naifahamu, DPP akiona kuna dosari katika ushahidi aliopelekewa anarudisha faili polisi lifanyiwe marekebisho. DPP hakufanya hivyo, alifungua kesi kwa kutumia statement za polisi kwamba mimi nina kesi ya kujibu.

Hii inaonyesha Polisi na DPP walivyokiuka taratibu dhidi yangu.

Wakili: Kuna ushahidi umesema wewe ulionekana Muhimbili, ulikwenda kufanya nini?

Shahidi: Nilienda huko kwani mke wangu alifanyiwa upasuaji.

Wakili: Uliwahi kukutana na baadhi ya mashahidi watatu ambao walikutaja kwamba ulivaa ninja na mwingine alisema alikukuta ofisini, mwingine alisema ulivaa sare za kazi?

Shahidi: Hivi inawezekana vipi mtu mmoja akavaa nguo mbili tofauti kwa wakati mmoja? Si kweli mashahidi hao wameidanganya mahakama.

Wakili: Katika maelezo ya mshitakiwa wa 11 (Rashid Lema) alisema wewe ndiye ulitoa amri watu hao wanne wachinjwe. Unasemaje?

Shahidi: Hakuna kitu chochote kinachonigusa mimi. Machi 6 mwaka 2006, Lema alitoa maelezo kwa mlinzi wa amani na akadai alimsikia Bageni akisema mimi nimesema watu hao wakachinjwe.

Wakili: Unaweza kusema Lema alikuwa ana nia gani?

Shahidi: Huyu Lema alipangwa animalize, kwani mtu mmoja anaandika statement mbili zenye maelezo tofauti. (Zombe akatoa machozi tena).

Wakili: Katika maelezo ya mshitakiwa wa 12, Bakari alikuwa akimsikia Bageni akisema ‘ndiyo afande, ndiyo afande’ kwa sababu walikuwa wote kwenye gari aina ya Pajero, huyo ndiyo afande ni nani?

Shahidi: Alinitaja mimi.

Wakili: Kwanini Lema alikutaja wewe?

Shahidi: Sijui, lakini chanzo cha mimi kuunganishwa kwenye kesi hii nasema wazi ni magazeti yalipoanza kuandikwa ‘Zombe kakamatwa.’ Huu ni mtandao tu. Haiingii akilini mshitakiwa mmoja Lema anitaje kati ya washtakiwa 15. Kuna kitu hapa (Zombe alimwaga machozi).

Wakili: Baada ya tukio lile la mauaji kuna taarifa kwamba ulifanya sherehe na kusema utawapandisha vyeo askari. Ni kweli?

Shahidi: Jamani si kweli. Ukisoma PGO kifungu cha 37 utaona jinsi gani vyeo vinavyopandishwa. Kuna sifa na zawadi katika PGO. Mimi nikiwa Kaimu RPC sijawahi na siwezi kutoa vyeo, anayepaswa kutoa vyeo ni IGP peke yake, tena kwa utaratibu maalumu.

Sina mamlaka ya kupandisha askari vyeo hayo ni majungu.

Wakili: Uliwahi kuulizwa na mpelelezi yeyote kuhusu matumizi yako ya simu ya mkononi?

Shahidi: Sijawahi.

Wakili: Ungependa kuiomba nini mahakama ikufanyie?

Shahidi: Naomba mahakama hii tukufu itoe haki kwa mujibu wa sheria na iangalie ushahidi uliotolewa. Kama nimetenda kosa nihukumiwe kwa kosa nililofanya.

Zombe alimaliza kutoa utetezi wake saa 8: 06 na wakili wake kuomba kesi iahirishwe hadi leo kutokana na hewa nzito iliyokuwapo mahakamani hapo, hoja ambayo iliungwa mkono na mawakili wote.

Leo Zombe ataanza kuhojiwa na mawakili wengine na baadaye wakili wa serikali.

Hata hivyo Zombe wakati anapanda gari kurudi gerezani hakufanya vituko kama ilivyo kawaida yake, bali alipunga mkono na kutabasamu.

Hata hivyo, umati wa watu waliofurika mahakamani hapo kusikiliza ulilalamikia hewa nzito iliyokuwapo mahakamani hapo na kuutupia lawama uongozi wa mahakama kwa kushindwa kudhibiti idadi ya watu na kuonya endapo hali hiyo isipodhibitiwa itaweza kuleta maafa
 

Hakuna kitu muhimu duniani kama kuwa na Public Trust. Kama ni mfanyabiashara ukipoteza Public Trust nobody can buy your products, kama ni kiongozi ukipoteza Public Trust hakuna mtu atakayekusikiliza utang'ang'ania kukaa kwa maslahi yako na si ya Umma. na moja ya dalili hii ni watu kusemasema pembeni na kunung'unikiwa kwa utendaji wako.

UKIONA WATU WANAANZA KUTOA HISIA ZAO KUHUSU MAHAKAMA BASI UJUE HAWAIAMINI KAMA ITATENDA HAKI. MAHAKAMA NA VYOMBO VYETU VYA DOLA VIMEPOTEZA PUBLIC TRUST SIKU NYINGI- KESI KAMA HIZI NDIZO ZA KUONESHA KUWA MAHAKAMA ZINAWEZA TENDA HAKI ZIKIWA MAKINI NA KUANZA KUJENGA UPYA PUBLIC TRUST. Wananchi wanajua kilichotokea msitu wa pande na wengi wanajua yanayotokea kila siku yafanywayo na hawa walinzi wetu wa amani na watoaji wa haki, hivyo matokeo yoyote ya uamuzi wa kesi hii yatakuwa na impact kwa mahakama whether ni negative or positive.

Hakuna kitu kibaya mbele ya jamii kama wewe kuonekana kuwa ni Ndimu - Arkalof
 
Last edited:
Kila kitu siasa mpaka katika uhai wa watu tunaleta siasa,kesi zote sio Zombe tu hata kina mramba,yona na wengineo ni changa la macho tu , CCM inajisafisha na uchaguzi 2010 wanajifanya wako seroius na ma issues kumbe zuga.
For get not: There are only three kind of people in this world.
(a)Those who don’t know what is happening
(b)Those who wondering what is happening
(c)Those who make it happening
Kuna watu hawajui lolote/chochoke kinachoendelea,na kuna watu kazi yao kushangaa tu mambo yanatokea,na kuna watu kazi yao ni kufanya mambo ya tokee.Thus wanachoofanya serekali chini ya CCM nikuwa cheza shere watanzania kwamba wako serious na issues then sisi tunashangilia but mwisho wa siku,workdone ina kuwa zero.Wanatumia kodi zetu wakati wakijua matokea ni ziro.Tujitahidi kuwa kundi la tatu sio la pili na kwanza(Wadanganyika)
 
Huyu Zombe kakata tamaa ya kupona nini?
 
Zombe amekata tamaa. Maji shingoni. Ameamua kubadilisha nguo kila siku ya kesi yake. Naona ANAZIAGA PAMBA zake kidizaini. Amehisi haponi.
 
Duh! huyu Zombe ana majibu ya maudhi na dharau sijapata kuona! haya yangu macho, ndio kibongo bongo tutafika kweli!
 
Zombe amekata tamaa maana anayoyajibu hayaendani kabisa na maswali anayojiuliza ni kama mchezo wa kuigia (pwagu na pwaguzi) nadhani ndio basi tena ngoja tuone
 
Kuwepo gizani kwa shitaka hilo kunatokana na namna ambavyo upande wa utetezi na ule wa serikali unavyoendelea kukabana koo kisheria, kuhusu kuhusika au kutohusika kwa watuhumiwa katika kesi hiyo ya kihistoria.

Akiwa katika siku yake ya pili ya utetezi wake jana (Jumatano) Zombe aliiambia Mhakama Kuu kwamba, wakati mauaji hayo yanatokea alikuwa kwenye ziara ya rais Jakaya Kikwete ambayo ilimchukua siku 30.

Hata hivyo, wakili wa serikali Alexander Mzikila alipinga utetezi huo kwa madai kuwa siku ambazo mtuhumiwa alizitaja zimejumlishwa na za mapumziko na kwamba watuhumiwa waliuawa siku za mapumziko.

Kuhusiana na utetezi wake wa awali wa barua alizodai kuandikwa na watuhumiwa wenzake kwenda kwa DPP kwa lengo la kumhusisha katika kesi hiyo wakili Alexander alidai kwamba, barua hizo ni za kughushi na kwamba isingekuwa rahisi Zombe kuzipata, ingawa mwenyewe alisema alizipata kwa mbinu za kikachero.

Kuhusu bastola iliyokamatwa wakati wa mauaji ambayo inadaiwa kukamatwa eneo la tukio, wakili huyo alisema Zombe hakuifanyia uchunguzi wa kumtambua mmiliki kabla ya kuipeleka kwa waandishi wa habari kuitangaza.

Kesi hiyo inaendelea tena leo (Alhamis), ambapo mshtakiwa wa pili Christopher Bageni anatarajia kutoa ushahidi wake.
 
Wakuu kazi ipo hapa. Mpaka wamalize kujitetea watayaanika yote maana hapa ni ama zangu ama zako. Ukweli wenyewe tutausikia wakianza kujitetea wale wengine, hakuna atakayeficha kitu hapa. Tutajua ukweli wa ni nani aliwakamata??? Nani waliwafunga kamba??? Walikuwa wameuwawa kwa staili ipi?? Ni nani walipewa jukumu la kuzibeba maiti zile? nakadhalika na nakadhalika!!!! Kuna wengine wataachiwa katika mchujo huu wa kujitetea na wengine wataenda na maji. Ni judgement itaamua kunyonga, kifungo cha maisha, au kifungo cha muda maalumu. Na ni nani kati ya hao wataingia kila aina ya kifungo, mahakama itaamua. Kila la heri Zombe na wenzako 9 katika utetezi wenu. Hivi hukumu ni lini??? Mahakamani hapatatosha siku hiyo, maana kwa wakati huu wa utetezi tu watu wanajaa kama utitiri. Sasa sielewi kama wote ni ndugu za marehemu au baadhi ni wale watu ambao wana hobby za kufuatilia kesi maarufu. Yaani kila kesi maarufu ni lazima utamkuta mtanzania huyo anahudhuria, sijui majukumu ya kujenga taifa anayapa priority kiasi gani??? Kazi ipo.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…