TANZIA Abdulkarim Shah, umekuja Saigon Sports Club umechelewa na umeondoka kwa haraka

TANZIA Abdulkarim Shah, umekuja Saigon Sports Club umechelewa na umeondoka kwa haraka

Mohamed Said

JF-Expert Member
Joined
Nov 2, 2008
Posts
21,967
Reaction score
32,074
Nimemjua Abdulkarim maarufu kwa jina la Bujji kwa kumsikia kwa muda mrefu kabla ya kukutananae uso kwa macho na sababu ya kumsikia kwa muda mrefu ni kuwa nilikuwa nikifuatilia siasa za Mafia katika chaguzi za vyama vya siasa mpashaji wangu mkubwa akiwa rafiki yangu Baku, mtu maarufu kisiwani Mafia yeye akiwa mwanachama shupavu wa CUF kama Abdulkarim alivyokuwa CCM hadi kufikia kuwa Mbunge.

Baku akinieleza miamba ya siasa za Mafia na jina la Bujji lilikuwa akilitaja mara nyingi pamoja na jina la Omar Kimbau na Mbaraka Dau.

Lakini kubwa ni kuwa binafsi nina maslahi na siasa za Mafia kwa kuwa mke wangu ni kutoka Mafia na alikuwa anataka kugombea nafasi mojawapo katika nafasi za juu kisiwani.

Kwa ajili hii basi nikipokea wageni wengi nyumbani wakitokea Mafia na nikajifunza historia ya watu wa Mafia na utamaduni wao.

Kitu cha kwanza watu wa Mafia takriban wote wanahusiana kwa njia moja au nyingine.
Wote ndugu ukuachilia mbali ule udugu wa Kiislam.

Pili Mafia hakuna mjinga.

Kila utakaemgusa hata akiwa mwanamke basi tambua kuwa kahifadhi. Lakini nililolipenda sana kwa watu hawa ni kuwa hawana makuu.

Akikufikia mgeni kutoka Mafia labda ghafla usiku wala usihangaike tenga kilichopo.
Jambo lingine watu wa Mafia fasaha sana.

Wana kipaji cha kuzungumza.
Mimi nafurahi kuwasikiliza kwa ile lafidh yao ya Kimafia kwani hakika inavutia.

Bujji akiniita ‘’Mwamu,’’ kwa Kimafia maana yake, ‘’Shemeji ’’ na hivi ndivyo Abdulkarim alivyopenda kuniita kila tukikutana na ilikuwa kupitia mke wangu, dada yake, ndipo Abdulkarim akafika nyumbani tukafahamiana na tukawa marafiki.

Hawa wanasiasa hata wakiwa wapinzani wana namna fulani ya ‘’urafiki,’’ tabu kwa sie wachezea pembeni kuelewa.
Hii kwa lugha ya kitaalamu wanaita, ‘’horse trading.’’

Lakini Bujji kama mwanasiasa alikuwa kabla hata ya kukutana na mimi akinisoma na kufuatilia kila nilikoandika na kuweka mtandaoni.
Nilifurahi sana pale Bujji alipojiunga na Saigon Club.

Abdulkarim hakupoteza muda mara moja Saigon ikatambua kuwa kama ni mchezo wa karata Saigon Club imelamba dume.
Kipi kitakachotatiza club Bujji asitoe suluhisho lake kwa kila hali utakayoifikiria?

Siku moja Bujji kaniandikia na akainipigia simu baada ya kusoma historia niliyoandika jinsi TANU ilivyoingia Southern Province (Jimbo la Kusini) kupitia wazalendo ambao yeye wengine amewaona akiwa mtoto na akacheza na watoto wao.

Alishangaa vipi sijataja mchango wa Kilwa.

Abdulkarim akaniambia, ‘’Mwamu babu yangu Abdulkarim Hajj Mussa Jamadar ambae mimi nimepewa jina lake akifahamiana vyema na Mwalimu Nyerere na ni mmoja kati ya watu waliomuunga mkono na kasaidia sana katika kuiingiza TANU Kilwa Mtoni na akimpakiza Mwalimu kwenye pikipiki yake BSA 500 wakienda kote sehemu za Kilwa kuhamasisha watu kujiunga na TANU na kudai uhuru wa Tanganyika.’’

Haukupita muda mrefu Bujji akanirushia picha ya pikipiki ya babu yake aliyokuwa akimchukua Nyerere, kijiji hadi kijiji, katika miaka ile ya 1950 pamoja na picha ya nyumba ambayo Nyerere alikuwa akifikia na kulala.

Bujji akaniletea na picha ya nyumba ya Mwinyi Mcheni Omari ambae mikutano yote ya ndani ya TANU ikifanyika.

Nilimshauri Abdulkarim kuwa tupate wasaa tukae kitako tuiandike historia hii kwa utulivu na yeye awasilaine na Makumbusho ya Taifa ili ile pikipiki ya somo yake Abdulkarim Hajj Mussa Jamadar ihifadhiwe kama kumbukumbu ya taifa.

Nilimweleza Bujji kuwa hivi tukifanya tutakuwa na kumbukumbu ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na pia tutakuwa na kumbukumbu ya babu yetu Abdulkarim Hajj Mussa Jamadar na kila atakaeiangalia pikipiki ile na akasoma maelezo yake ataona juu au chini yake picha ya wazalendo hawa wawili zimewekwa ubavu kwa ubavu.

Abdulkarim kwa muda mfupi tuliofahamiana niligundua kuwa si mru wa maneno matupu haraka hili alilifanya na watu wa Makumbusho wakanipigia simu kutaka kujua habari zaidi.

Nami nikawaambia kuwa mtu wa kumshika ni Abdulkarim Shah.
Miezi sita iliyopita Bujji alikuja nyumbani na kamati yake ya kuitangaza Kilwa kama moja ya vivutio vya utalii Tanzania na tukafanya mazungumzo.

Abdulkarim alinitaka aniingize katika kamati ile ili nitoe mchango wangu kwa kile ninachokifahamu katika historia ya Tanganyika.

Hakika Saigon tumeondokewa lakini Abdukarim katuachia mengi sana ya kumkumbuka inagwa Allah hakujaalia sisi kuwa na yeye kwa muda mrefu.

Mwenyezi Mungu amfanyie wepesi ndugu yetu katika safari yake hii na amtie Firdaus.

Amin.


PICHA: Abdulkarim Shah akiwa katika Khitma ya Saigon 2019 hii ilikuwa khitma yake ya kwanza kuhudhuria kama mwanachama picha inayofuatia ni pikipiki ya babu yake Abdulkarim Hajj Mussa Jamadar na picha ya tatu ni nyumba ya babu yake ambayo Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akifikia na kulala wakati wa kupigania uhuru wa Tanganyika.

ABDULKARIM SHAH KHITMA SAIGON.jpeg

PIKIPIKI YA MZEE ABDULKARIM.jpg

NYUMBA YA MZEE ABDULKARIM HAJJ MUSSA JAMADAR.jpeg
 
'Kitu cha kwanza watu wa Mafia takriban wote wanahusiana kwa njia moja au nyingine.
Wote ndugu ukuachilia mbali ule udugu wa Kiislam.'

Kama kawaida.
 
'Kitu cha kwanza watu wa Mafia takriban wote wanahusiana kwa njia moja au nyingine.
Wote ndugu ukuachilia mbali ule udugu wa Kiislam.'

Kama kawaida.
Mnga'ato,
Allah ndiyo kauli yake katika Qur'an kuwa Muislam nduguye Muislam.

Aya inaendelea kueleza kupatanisha baina ya ndugu waliogombana.

Sent using Jamii Forums mobile app
 
'Kitu cha kwanza watu wa Mafia takriban wote wanahusiana kwa njia moja au nyingine.
Wote ndugu ukuachilia mbali ule udugu wa Kiislam.'

Kama kawaida.

Huyu Ustadhi wa Tandamti inabidi kuzoea mambo yake
 
Umenikumbusha Mafia. Watu waungwana kweli. Na ni kweli wana undugu karibu wote. Wanatofauti sana na waislam wa bara. Wachache hawa walofanikiwa hawawekezi kwao mji na wengi wakikua wanahamka huku bara kwa hiyo mji haundelei.

Siasa za Mafia zimetawaliwa na hizo familia tatu.

Visiwa vizuri na utajiri wa samaki unaneemesha Dar es salaam.

Poleni wana Mafia.

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Ungeandika Eulogy kama hii kwa Mama Rwakatare kwa makubwa aliyofanya ila Udini sasa

Sent using Jamii Forums mobile app
Mtochoro,
Unamwandikia taazia mtu unayemfahamu.

Mama Rwakatare nikimfahamu katika miaka ya 1970s tukiwa wote ni watumishi wa East African Cargo Handling Services (EACHS)enzi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki ofisi zetu zikiwa Kilwa Road.

Tukapoteana kwa miaka lakini nilisikia kuwa amekwenda Amerika.

Sina zaidi niyajuayo katika maisha yake.

Pole sana ndugu yangu si kama sikumuandikia taazia kwa kuwa si Muislam.



Sent using Jamii Forums mobile app
 
Huyu Ustadhi wa Tandamti inabidi kuzoea mambo yake
Ngongo,
Mimi si ustadhi wala sina uhusiano wowote na Mtaa wa Tandamti.

Nimeishi miaka mingi ya maisha yangu Masaki, Msasani Peninsular na anuani yangu ya Dar es Salaam ndivyo inavyoonyesha hadi sasa.

Hapo ndipo kwetu.

Ningeshukuru sana kama ningejaaliwa nikawa ustadh lakini kuwa ustadh kunahitaji ilm ambayo mie sina.

Mwanangu sasa mtu mzima ananambia,"Baba nikiona tabu sana kukuona wewe unasali nyuma yangu mie mwanao ndiyo imam naongoza sala."

Mie humjibu nikamwambia, "Ndiyo ujue faida ya ilm mimi baba yako nimekuwa chini wewe umekuwa juu sababu ni hiyo ilm ambayo mimi sina; ni hiyo Qur'an uliyohifadhi ndiyo imekunyanyua wewe. Hawawi sawa mwenye kujua na asiyejua."

Ningependa sana kuwa ustadh lakini kunahitaji ilm kuwa ustadh hakuji kirahisi upinde mgongo kwa walimu usomeshwe vitabu na vitabu.

Hakika ningependa kuwa ustadh.

Nilichoambulia ni passages and passages za William Shakespeare, Charles Dickens...

Ngongo unaponiita ustadh ilm niitakayo lakini sina unatonesha kidonda.




Sent using Jamii Forums mobile app
 
Mohamed Said nashukuru kwa bandiko mujarab lenye kuelimisha.

Kuwaridhisha binadam wote kwa wakati mmoja ni kazi sana na huenda isiwezekane. Hilo lisikuvunje moyo wa kuendelea kuandika.

Kila mtu ana uhuru wa kuamua achukulie vipi jambo, akijikita kwenye udini, atakosa vitu vya msingi.

Ifike mahali tuzingatie kwanza kitu gani kimeandikwa kisha nani kaandika ikiwa kuna ulazima.

Mfungo mwema Ustaadh.
 
Mohamed Said nashukuru kwa bandiko mujarab lenye kuelimisha.

Kuwaridhisha binadam wote kwa wakati mmoja kazi sana. Hilo lisikuvunje moyo wa kuendelea kuandika.

Kila mtu anauhuru wa kuamua achukulie vipi jambo, akijikita kwenye udini, atakosa vitu vya msingi.

Ifike mahali tuzingatie kwanza kitu gani kimeandikwa kisha nani kaandika ikiwa kuna ulazima.

Mfungo mwema Ustaadh.
The Monk,
Amin.

Sent using Jamii Forums mobile app
 
Pili Mafia hakuna mjinga. Kila utakaemgusa hata akiwa mwanamke basi tambua kuwa kahifadhi.

..hizo sentensi mbili kwa kweli zimenifurahisha sana.

..zimenifurahisha kwasababu umeweza kueleza jambo kubwa kwa maneno machache, lakini kwa msisitizo mkubwa.

..nimerudia kusoma sentensi hizo tena na tena nikifurahia umahiri wako wa kucheza na maneno.

..THANK YOU!!
 
Ulipozungumzia mafia nilikuwa nasubiri kusikia historia yao maana Zanzibar wanadai ile nisehemu yao
 
Back
Top Bottom