Ndagullachrles
JF-Expert Member
- Jun 20, 2023
- 256
- 259
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro limewataka wanachuo wa mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Udaktari na Uuguzi cha KCMC Moshi, kujitambua, kuzingatia maadili mema na kuepuka vishawishi vinavyoweza kuwapeleka katika vitendo vya kihalifu wakati wa masomo yao.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Kilimanjaro ACP Lazaro Mwanyasi wakati akitoa elimu ya ulinzi na usalama kwa wanachuo hao akisisitiza umuhimu wa kuwa na misimamo imara, kuzingatia imani zao za dini na kuepuka kufuata mikumbo ya watu wenye mienendo mibaya.
Mwanyasi amewaonya pia wanachuo hao dhidi ya kujihusisha na uanaharakati usiozingatia taratibu na kanuni za chuo akiwataka kuelekeza nguvu zao katika masomo na kujenga mustakabali mzuri wa maisha yao badala ya kujiingiza katika makundi au shughuli zinazoweza kuvuruga masomo, nidhamu na amani chuoni.
Aidha, amewahimiza kutokubali tamaa ya fedha na ushawishi wa makundi yasiyofaa kuwafanya wajihusishe na vitendo vya uhalifu, akiwakumbusha kuwa fursa ya kupata elimu ya juu ni hatua muhimu inayohitaji uwajibikaji, nidhamu na matumizi sahihi ya muda wao katika kujenga maisha na taaluma zao.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Dawati la Jinsia na Ulinzi wa Mtoto Mkoa wa Kilimanjaro, SSP Asia Matauka, amewataka wanachuo hao kujitambua na kutambua thamani ya fursa waliyoipata ya kusoma katika chuo hicho, huku akiwahimiza kutoa taarifa kwa mamlaka husika wanapobaini matukio ya ukatili ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.
Naye Mkuu wa Polisi Jamii Wilaya ya Moshi, SP Juma Kabelwa, amewasisitiza wanachuo hao kuzingatia usalama wao binafsi kwa kuepuka kutembea peke yao nyakati za usiku bila sababu za msingi, kutunza fedha na mali zao ili kuepuka wizi na utapeli, pamoja na kushirikiana katika kujenga mazingira salama ndani na nje ya chuo.
Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa chuo hicho, matroni wa wanafunzi amelitaka Jeshi la Polisi kuendeleza ushirikiano huo na kulishukuru kwa kutoa elimu iliyogusa nyanja mbalimbali za maisha ya wanachuo, akieleza kuwa elimu hiyo itawasaidia wanafunzi wapya kuanza masomo yao wakiwa na uelewa wa masuala ya ulinzi, usalama na namna ya kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza katika maisha ya chuo.
Elimu hiyo imetolewa kupitia kampeni ya Ongea na Kamanda inayotekelezwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro kwa lengo la kuimarisha mawasiliano na ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na wananchi, kupokea maoni na changamoto zao na kuzifanyia kazi.
Kupitia kampeni hiyo, Jeshi la Polisi linaendelea kuwafikia makundi mbalimbali katika jamii, ikiwemo vijana na wanachuo kwa ajili ya kuhamasisha uzingatiaji wa sheria, maadili mema na ushiriki wa kila mmoja katika kulinda amani na usalama wa jamii