Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 5,352
- 15,876
Kwanza, Serikali inayotuhumiwa kwa kushindwa kuzuia au kuhusika na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu haiwezi kuwa ndiyo inayounda, kuelekeza na kusimamia chombo cha kuchunguza tuhuma zinazoihusu. Kanuni za haki zinataka mtuhumiwa achunguzwe na chombo huru, si kujichunguza mwenyewe. Aidha, muundo wa Tume uliotangazwa haujengi imani kwa waathirika, wananchi na Jumuiya ya Kimataifa kwamba uchunguzi huo utakuwa huru na usio na upendeleo.
Pili, hadidu rejea za Tume zinaonyesha wazi kuwa lengo lake kuu si kulinda haki za waathirika wala kubaini ukweli wa matukio ya Oktoba 29, 2025. Badala yake, zinaelekeza nguvu katika kuwatafuta na kuwachunguza wanaodaiwa kuhusika na vurugu, bila kuweka uzito unaostahili katika kuchunguza mauaji, majeruhi, upotevu wa watu na ukiukwaji mwingine wa haki za binadamu unaodaiwa kufanywa na vyombo vya dola. Kwa msingi huo, Tume hii inaonekana zaidi kuwa chombo cha kuilinda Serikali dhidi ya tuhuma zinazoikabili kuliko kuwa chombo cha kutafuta ukweli, kutenda haki na kuhakikisha uwajibikaji.
Kwa sababu hizo, ACT Wazalendo haitambui Tume hii kama chombo kinachoweza kutoa uchunguzi unaoaminika. Tunarudia wito wetu wa kuundwa kwa uchunguzi huru wa kimataifa utakaoendeshwa au kusimamiwa na taasisi huru zinazotambulika kimataifa, ikiwemo Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Afrika (AU) au Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), ili kubaini ukweli, kuwawajibisha wote waliohusika bila upendeleo na kuhakikisha waathirika wanapata haki.
Tunaitaka pia Serikali kuwaachia huru wafungwa na watuhumiwa wote wa kesi zenye muktadha wa kisiasa, kuwapatia waathirika msaada wa kitabibu, kisheria, kisaikolojia na kifedha, na kuanza kwa dhati mchakato wa Katiba Mpya pamoja na mageuzi ya kisiasa yatakayojenga taasisi huru na kuzuia matukio ya aina hii kujirudia.
ACT Wazalendo itaendelea kusimama katika misingi ya Ukweli, Haki na Uwajibikaji, kwa kuamini kuwa amani ya kudumu haiwezi kujengwa kwa kuficha ukweli bali kwa kuuweka wazi na kuhakikisha sheria inachukua mkondo wake bila upendeleo.
ACT Wazalendo: Taifa Kwanza, Leo na Kesho!
Imetolewa tarehe 08 Agosti, 2026.
Isihaka Rashid Mchinjita
Makamu Mwenyekiti Bara
ACT Wazalendo