Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 5,352
- 15,876
UAMUZI WA EALS KUHAMISHA MKUTANO WAKE KUTOKA ZANZIBAR UTUPE FURSA YA KUJITATHMINI
Tarehe 20 Juni, 2025, Jumuiya ya Wanasheria ya Afrika Mashariki (East Africa Law Society) ambayo inajumuisha vyama vya wanasheria vya nchi nane (8) - Tanganyika, Kenya, Uganda, Zanzibar, Rwanda, Burundi, Sudan ya Kusini, na Ethiopia - ilitangaza uamuzi wa kuhamisha Mkutano wake wa 30 kutoka Zanzibar na kuupeleka Addis Ababa, nchini Ethiopia.
Sababu kubwa zilizotolewa na Jumuiya hiyo katika kufikia maamuzi hayo ni kutokuwa na uhakika wa usalama wa wajumbe wa Mkutano huo ambao ni wanasheria kutoka nchi hizo, wakitaja matukio mabaya ya hivi karibuni ambayo yamewakumba watu mbali mbali hapa Tanzania wakiwemo wanasheria kutoka nchi wanachama wa Jumuiya hiyo. Sababu nyingine ni kuwa tarehe za Mkutano huo ziko katika kipindi cha Uchaguzi Mkuu hapa nchini, kipindi ambacho kutokana na historia ya chaguzi zilizopita hakiwapi uhakikisho wa kuwepo na utulivu.
Soma Pia: Mkutano Mkuu Chama cha wanasheria Afrika mashariki 2025 Kuhamishwa ,Addis Ababa Kutokana na Uchaguzi Tanzania
Sisi ACT Wazalendo tunauona uamuzi huu kuwa ni pigo kubwa sana kwa taswira ya nchi yetu na mifumo yake ya haki na uchaguzi. Uamuzi huo kutoka kwa chombo kinachohusisha wanasheria wa nchi wanachama ikiwemo Zanzibar unaitia doa nchi yetu kuwa si pahala salama na unathibitisha yale ambayo sisi ACT Wazalendo tumekuwa tukiyasimamia kwa miaka mingi - kwamba marekebisho makubwa katika mifumo ya haki na Uchaguzi yanahitajika ili kuzifanya chaguzi zetu kuwa huru na za haki na zinazofanyika katika mazingira ya amani na utulivu.
ACT Wazalendo tunatoa wito kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuuchukulia uamuzi huu kwa uzito wake na kuutumia kama fursa ya kujitathmini na kufanya marekebisho makubwa yanayohitajika katika mifumo ya utoaji haki na uendeshaji wa chaguzi zetu.
Miongoni mwa mambo ya kuzingatiwa katika mfumo wa utoaji wa haki ni marekebisho makubwa ya Jeshi la Polisi, Idara ya Usalama wa Taifa, Vikosi vya SMZ na Mahakama zetu. Katika upande wa mfumo wa uendeshaji chaguzi zetu ni haja ya kuunda Tume Huru za Uchaguzi Tanzania na Zanzibar ikiwa ni pamoja na Sekretarieti huru za Tume hizo, kupitia upya Kanuni zinazosimamia chaguzi zetu, kuondosha kura ya siku mbili Zanzibar ambayo ilikuwa chanzo cha mauaji ya raia 21 wasio na hatia katika Uchaguzi Mkuu wa 2020 na kuhakikisha watu wote wenye haki wanaandikishwa katika Daftari la Wapiga Kura.
Busara na Hekima inatutaka kufanya hivyo. Bado hatujachelewa.
Imetolewa leo, tarehe 26/06/2025 na,
Khalfan Amour Mohammed
Msemaji wa Ofisi, Katiba na Sheria - Zanzibar