Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 3,984
- 13,760
MKUU WA MKOA WA DAR ES SALAAM AWAJIBISHWE HARAKA KULINDA UTU WA WANANCHI
Chama cha ACT Wazalendo kinalaani vikali kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ndg. Albert Chalamila inayowataka wanawake kujifungua nyumbani kwa kutumia visu na mikasi endapo watakosa fedha za kulipia huduma hospitalini. Kauli hii inashambulia haki za msingi za wananchi kupata huduma bora za afya, hasa huduma za uzazi zilizoahidiwa kutolewa bure.
Kusoma alichokisema Mkuu wa Mkoa ~ RC Chalamila asema mjamzito anayegoma kununua gloves akajifungulie nyumbani. Hafai kuendelea kubaki madarakani
Kauli ya Mkuu wa Mkoa akiwa katika ziara Wilaya ya Temeke, inayosema kwamba mwanamke anayekosa fedha za kujifungua hospitalini ajifungue nyumbani kwa kutumia visu na mikasi. Si tu kwamba ni kinyume na maadili ya kiuongozi, sera ya utoaji wa huduma za bure kwa wajawazito bali ni yanaweka rehani maisha ya mama na mtoto.
Kauli hii ni mwendelezo wa matamko ya Chamilika yasiyo ya kiuongozi, yenye kejeli pindi wananchi wanapokuta naye kueleza matatizo yao au changamoto na huduma.
Tukio hili linadhihirisha kile ambacho Watanzania wengi wanapitia kwenye mfumo wa afya wa sasa unaotegemea uwezo wa kifedha badala ya huduma kwa wote na hivyo kuhatarisha maisha ya wananchi masikini hasa wanawake, watoto na wazee.
Ikiwa kauli hiyo ya kutaka wanawake wasio na uwezo wa kifedha wajifungulie nyumbani haifanywi rasmi kuwa msimamo wa Serikali ya Chama cha Mapinduzi, tunatoa wito wa kuchukuliwa hatua zifuatazo:
Tunamtaka Rais Samia kumwajibisha haraka Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kauli zake zisizo za kiuongozi ambazo zinakiuka misingi ya utoaji haki na huduma za afya kwa wajawazito na watoto.
Tunaitaka Serikali kutekeleza kwa vitendo ahadi yake ya kuhakikisha huduma za uzazi zinapatikana bila gharama, kama ilivyoainishwa katika sera ya afya ya taifa.
Serikali iharakishe utekelezaji wa mfumo wa kuwaunganisha watanzania na Hifadhi ya Jamii na kutoa bima ya afya kwa wote ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za afya bila ubaguzi wa kifedha.
ACT Wazalendo inaendelea kusimama kidete kuhakikisha kuwa huduma za afya si bidhaa ya kibiashara, bali ni haki inayopaswa kutolewa kwa kila mwananchi kwa heshima na utu.
Dkt. Elizabeth Benedict Sanga
Waziri Kivuli wa Afya
ACT Wazalendo
26 Januari, 2024