Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 3,984
- 13,760
Chama cha ACT Wazalendo, tumepokea kwa masikitiko na huzuni kubwa taarifa ya kuuliwa kwa watu wawili na Kikosi cha KVZ cha Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na mtu mmoja ambae hajuilikani alipo mpaka sasa, huko katika Kijiji cha Kiungoni, Jimbo la Pandani, Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Waliouliwa ni Athumani Hamad Athumani na Amour Khamis Salim. Mtu mwengine wa tatu ambaye hajuilikani yupo wapi pamoja na hali yake ni Ndugu Mbarouk Abdalla Khamis. Watu hawa walichukuliwa usiku wa tarehe tarehe 23 kuamkia tarehe 24/12/2024, mnamo saa 7 za usiku, wakiwa wazima wa afya na kutokuwa na ugonjwa wa aina yoyote ile.
Mnamo majira ya saa 1:30 usiku wa tarehe 24/12/2024, maiti za watu wawili zilipelekwa kwa familia zao kwa kutumia gari la KVZ kwa ajili ya taratibu za mazishi bila ya maelezo yoyote yale.
Pia soma: Pemba: Polisi wachunguza vifo vya watu wawili waliofariki dunia wakipatiwa matibabu hospitali ya Ali Khamis Camp
Tukio hili linafanana na tukio la mauaji lililowahi kutokea hivi karibuni huko Kidoti, Mkoa wa Kaskazini Unguja, ambalo limebakia kuwa doa katika Zanzibar. Matukio haya yanazidi kudhoofisha na kutia wasiwasi kuhusu uslama wa maisha na amani ya wananchi wa Zanzibar.
Chama Cha ACT Wazalendo, tunaitaka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi kuchukua hatua zifuatazo ili kukomesha mauaji haya:-
1. Amuwajibishe kwa kutengua haraka uteuzi wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Serikali za Mitaa, Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ kwa kushindwa kuzisimamia ipasavyo Idara hizi Maalum za SMZ na badala yake kutumika kama ni vyombo vya kukatisha uhai wa watu.
2. Aunde Tume huru ya Kijaji kuchunguuza Mauaji yote yaliyotokea hivi karibuni hapa Zanzibar ambayo yanahusisha Vikosi vya Ulinzi na Usalama.
3. Tunalitaka Jeshi la Polisi kuhakikisha wanatimiza wajibu wao wa kulinda raia na mali zao, kwa kuhakikisha usalama na raia wanaishi katika nchi yao bila ya khofu.
Pia soma: CCM Zanzibar yataka chama cha ACT Wazalendo kuacha kuingilia kazi za Polisi
4. Tunalitaka Jeshi la Polisi kuhakikisha wanawakamata wote waliohusika na mauaji haya na mengine na kuwafikisha mahakamani haraka iwezekanavyo.
5. Tunalitaka Jeshi la Polisi kuweka wazi Ripoti ya Tume waliounda ya mauaji yaliyotokea Kidoti tarehe 09/11/2024.
Imetolewa leo, tarehe 25/12/2024 na,
Hamad Mussa Yussuf,
Msemaji wa Ofisi, Kamati ya Wasemaji wa Kisekta - Zanzibar