Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 5,352
- 15,876
Tunamtaka Rais Mwinyi, kuunda Tume huru kuchunguza matukio ya Mauwaji ya Raia)
ACT Wazalendo tunalaani vikali tukio la mauaji ya kinyama dhidi ya Ndugu Juma Ame Ngwali, mwenye umri wa miaka 58, mkazi wa Kijiji cha Ndooni, Shehia ya Uweleni, Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba. Marehemu alifariki dunia mnamo tarehe 08/03/2025, majira ya saa 7:00 mchana, katika Kijiji cha Manyaga, Shehia ya Mbuguani, Wilaya ya Mkoani, baada ya kushambuliwa na kufanyiwa ukatili mkubwa na kikosi maalum kilicho chini ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar (ZDCEA) kwa kushirikiana na vyombo vyengine vya Ulinzi na Usalama
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa familia na mashuhuda wa tukio, marehemu alikuwa akijishughulisha na kazi zake za kawaida za kupara njiti za mafyagio kabla ya kushambuliwa kwa kupigwa maeneo ya shingo, kuchomwa moto mgongoni, na kukatwa maeneo ya mgongo na mikono kwa vitu vyenye ncha kali. Aidha, waliotekeleza ukatili huu waliripotiwa kuwa na silaha za moto, jambo linaloashiria uwezekano wa matumizi mabaya ya madaraka na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.
ACT Wazalendo tunaamini kwamba, kitendo hichi cha kikatili na kinyama, kilichofanywa kwa mwananchi huyu, ni uvunjifu wa katiba ya Zanzibar na Ukiukwaji wa Haki ya Kuishi Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, ibara ya 13, inatamka wazi kuwa kila mtu ana haki ya kuishi na kwamba hakuna mtu anayeruhusiwa kunyimwa uhai wake kinyume cha sheria. Mauaji ya Ndugu Juma Ame Ngwali ni kinyume na haki hii ya msingi.
ACT Wazalendo, tumeshitushwa na matumizi mabaya na nguvu yanayoendela kufanywa hivi karibuni na Vyombo vya Ulinzi na Usalama, hivi karibuni kuna matukio kadhaa yaliyotokea kule kidoti, Mkoa wa Kaskazini, Unguja na Kiungoni Mkoa wa Kaskazini Pemba, ambayo yamefanya na vyombo vya ulinzi na usalama na hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa na serikali, hivyo inadhihirisha wazi kabisa, matumizi mabaya ya nguvu dhidi ya raia wasio na hatia. Ni kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ibara ya 15, kwani inatoa ulinzi dhidi ya utekaji, mateso na adhabu za kinyama, kama hizi.
ACT Wazalendo, tunaamini kwamba, matendo yote haya yana baraka za watawala, hakuna Ufuatiliaji wowote unaofanywa na dola, wala hatua walizozichukua, pamoja na raia wema kutoa taarifa na kuonesha mashirikiano ya kina.
Kutokana na uzito wa tukio hili, ACT Wazalendo tunatoa wito kwa hatua zifuatazo kuchukuliwa mara moja:
1. Tunamtaka Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, kuunda Tume huru Uchunguzi wa haraka, ili wahusika wote wa tukio hili na mengine kama haya wafikishwe mbele ya sheria.
2. Tunaitaka Serikali itoe tamko rasmi kueleza mazingira ya tukio hili na hatua inazochukua kulinda maisha ya wananchi dhidi ya matumizi mabaya ya nguvu kutoka kwa vyombo vya dola.
3. Taasisi za Haki za Binadamu, ndani na nje ya nchi, zichukue hatua ya kufuatilia kwa karibu ili haki itendeke kwa familia ya marehemu.
4. Wananchi wasimamie haki na kuhakikisha kuwa matukio kama haya hayaachiwi bila uwajibikaji wa waliohusika.
ACT Wazalendo tunasisitiza kuwa hakuna taifa linaloweza kuendelea ikiwa wananchi wake wanauliwa kwa ukatili mkubwa bila hatua zozote kuchukuliwa. Tunamtaka Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani, kutoa maelezo juu ya tukio hili na mengine yenye mfanano na tukio hili na hatua zinazochukuliwa ili haki ipatikane.
Imetolewa leo, tarehe 19/03/2025 na,
Hamad Mussa Yussuf,
Msemaji wa Ofisi, Kamati ya Wasemaji wa Kisekta - Zanzibar