Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 3,984
- 13,760
UCHAGUZI UBATILISHWE NA KUITISHWA UPYA
TAARIFA YA AWALI YA KAMATI YA UONGOZI TAIFA YA CHAMA CHA ACT WAZALENDO KUHUSU UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA, VIJIJI NA VITONGOJI 2024
Kamati ya Uongozi Taifa ya Chama cha ACT Wazalendo imekutana kwenye kikao chake cha dharura jana tarehe 28 Novemba, 2024. Pamoja na mambo mengine, Kamati ya Uongozi imefanya tathmini ya awali ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji uliofanyika tarehe 27 Novemba, 2024.
Msimamo wa ACT Wazalendo ni kuwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji 2024 haukuwa uchaguzi dhidi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) bali ulikuwa uchaguzi dhidi ya dola, hivyo ubatilishwe na kuitishwa upya.
Mchakato mzima wa uchaguzi kuanzia hatua ya utungaji wa kanuni, uandikishaji wa wapigakura, uteuzi wa wagombea, upigaji wa kura na utoaji wa matokeo uliharibiwa na mamlaka ya kusimamia uchaguzi (TAMISEMI) ikisaidiwa na vyombo vyombo vya dola ikiwemo vyombo vya ulinzi na usalama.
Mchaķato wa uchaguzi ulitawaliwa na matukio ya vitisho dhidi ya raia hasa wanaochuķua fomu, ukamataji na utekaji wa raia, kutishwa ķwa mawaķala wetu na ķiwango cha juu cha matumizi ya kura bandia.
Karatasi za kura kuwa kwenye mikono ya wana-CCM na haswa wagombea, kinaonyesha dhahiri kuwa hakuna tena maana (‘credibility’) ya uchaguzi hapa nchini. Vyombo vya dola vilihusika kutumbukiza kura bandia kwenye masanduku ya kura vituoni. Kwa mfano, katika Manisapaa ya Kigoma Ujijij jimbo la Kigoma Mjini, Askari mwenye hadhi ya Inspekta alikamatwa na wananchi akiwa na mamia ya kura akijaribu kuyaingiza kwenye sanduku la kura na kuleta taharuki kubwa.
Viongozi na wanachama wetu waliojaribu kukabiliana na hujuma hizi walishughulikiwa ķwa mkonno wa chuma wa dola kwa vipigo na kukamatwa. Mifano ya hili ni mingi ikiwepo wanachama wetu zaidi ya 30 katika Jimbo la Kigoma Mjini waliokamatwa na Polisi kwa ķudhibiti kura feki; Mwenyekiti wa Jimbo la Tunduru Kaskazini aliyekamatwa kwa kumzuia Msimamizi wa Kituo asimtoe nje wakala wetu, Mwenyeķiti wa Mkoa wa Songwe aliyekamatwa na kupigwa na Polisi, wagombea wetu wawili wilayani Muleba kutekwa, Mwenyeķìti wa Ngome ya Wanawake Jimbo la Mchinga aliyetekwa na vikosi vya CCM n.k
MSIMAMO WA AWALI WA CHAMA
1. ACT Wazalendo hatukubaliani na matokeo yaliyotangazwa na Waziri wa TAMISEMI Ndugu Mohamed Mchengerwa kwani mchakato mzima wa uchaguzi umevurungwa kwa kiwango ambacho kimepora madaraka ya wananchi kuchagua viongozi wao.
2. ACT Wazalendo tunataka uchafuzi huu wote ubatilishwe na uchaguzi mpya wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji ufanyike baada ya kupata sheria mpya ya uchaguzi huo na Tume Huru ya Uchaguzi.
3. ACT Wazalendo tutafanya mawasiliano na Vyama makini vya Siasa na Asasi muhimu za Kiraia ili kuitisha kikao kwa ajili ya kupata mkabala wa pamoja katika kupata ufumbuzi wa uhuni na uchafuzi dhidi ya mifumo ya usimamizi na uendeshaji wa chaguzi na vipi kuihami demokrasia hapa nchini.
Maeneo tunayotaka yafanyiwe kazi kwa pamoja na vyama na asasi makini ni Mabadiliko ya Katiba ili kupata Katiba Mpya, Sheria za Uchaguzi na uundwaji wa Tume Huru ya Uchaguzi pamoja na Sekretarieti Huru ya Tume wakiwemo Wasimamizi wa Uchaguzi na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi na Makarani wa Uchaguzi. Yote haya yakamilike kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
4. ACT Wazalendo tunakusanya taarifa ya matukio yote ya uchafuzi na uhuni uliofanyika na tutatayarisha taarifa kamili ya Chama kuhusu hicho kilichoitwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji.
Aidha, Chama kinasimamia wanachama na viongozi wote waliokamatwa kuweza kutolewa na inapobidi kuwapatia wanasheria. Zaidi ya wanachama wetu 60 walikutwa na kadhia ya kukamatwa na kushikiliwa na Jeshi la Polisi wakipambana kudhibiti uhuni uliofanyika kwenye hicho kinachoitwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji.
Taarifa Kamili ya uhuni na uchafuzi uliofanyika tutaisambaza kwa Jumuiya zote za Kimataifa, Mashirika ya Haki za Binadamu, Taasisi za Fedha Duniani na nchi washirika wa Tanzania duniani kote.
5. Katika hatua ya sasa, tunawataka wanachama wetu ķutotoa ushirikiano kwa viongozi wa Mitaa, Vijiji na Vitongoji kutoka Chama cha Mapinduzì (CCM) ambao wametangazwa kuwa washindi bila uhalali hadi hapo uchaguzi huu utakapoitisha na kufanyika upya kwa kuzingatia misingi ya demokrasia ya uchaguzi huru, wa haki na unaokubalika.
HITIMISHO
Uchaguzi huu umechora picha halisi kwamba CCM bado haiamini katika utawala bora, demokrasia na haki za raia. Imedhihirisha kuwa yote yaliyofanyika tokea kuanza kwa Awamu ya Sita, tokea mikutano ya wadau, Kikosi Kazi, Mikutano ya Maridhiano na baadhi ya vyama, Mikutano ya Baraza na Vyama vya Siasa na kuasisiwa na watu kuaminishwa katika Falsafa ya 4R yalikuwa na madhumuni ya kuwasahaulisha na kuwatuliza Watanzania madhila na udhalimu mkubwa waliopitia chini ya Awamu ya Tano.
Uchaguzi huu wa Serikali za Mitaa, Vìjiji na Vìtongoji umetanabahisha jambo moja la kutia hofu kubwa katika Taifa nalo ni la kukosekana kwa uongozi madhubuti wa kuipeleka nchi katika mageuzi makubwa yanayohitajika.
Imetolewa na;
Dorothy Jonas Semu
Kiongozi wa Chama
ACT Wazalendo
29 Novemba, 2024.