ACT Wazalendo yafanya Uchambuzi wa Ripoti ya CAG 2023/2024, leo Mei 10, 2025

ACT Wazalendo yafanya Uchambuzi wa Ripoti ya CAG 2023/2024, leo Mei 10, 2025

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Joined
Apr 18, 2017
Posts
5,352
Reaction score
15,876
ACT Wazalendo wanafanya Uchambuzi wa Ripoti ya CAG 2023/2024 Mei 10, 2025


UCHAMBUZI WA ACT WAZALENDO RIPOTI YA MDHIBITI NA MKAGUZI MKUU WA HESABU ZA SERIKALI KWA MWAKA WA FEDHA UNAOISHIA MWEZI JUNI 2024

“Ubadhirifu, Uozo na Ufisadi wa Mama”

UTANGULIZI

Jumatano tarehe 16 April 2025 Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Bw. Charles Kichere alitoa taarifa yake ya Ukaguzi wa Mapato na Matumizi ya Fedha za Umma kwa mwaka wa fedha wa 2023/24 Bungeni baada ya kuikabidhi kwa Rais mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu.

Sisi, ACT Wazalendo tumeisoma, kuipitia na kuichambua taarifa husika, kwa lengo la kuitumia ili itusaidie kutimiza wajibu wetu wa kuisimamia Serikali kama chama mbadala nchini. Katika uchambuzi wetu, tumeona zipo hoja nyingi za ukaguzi zinajirudiarudia mwaka hadi mwaka.

Aidha, katika uchambuzi wa miaka mitatu 2020/21, 2021/22, 2022/23 na 2023/24 tuliibua hoja 40 kutoka katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi tumeona hoja nyingi zikijirudia na hakua natua za msingi zinafanywa kuwawajibisha wahusika.

Wakati ambao bunge la CCM limehalalisha ndoa yake na serikali; na kuamua kusaliti majukumu yake ya kikatiba: ya uwakilishi wa wananchi na kuisimamia serikali, ACT Wazalendo tunaendeleza wajibu wetu wa kuwawakilisha wananchi kwa kuitumia Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuanika uozo, ubadhirifu na uzembe.

Uchambuzi wa Ripoti ya CAG mwaka 2023/24
ACT Wazalendo, kupitia uchambuzi wetu wa ripoti ya CAG mwaka 2023/24, tumebaini hoja/ mambo kumi (10) muhimu ambayo tumekusudia kuwaeleza Watanzania na kuyatolea mapendekezo na miongozo kwa ajili ya kuchukuliwa hatua.

Ubadhirifu na Upotevu wa Fedha za Umma

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwa mwaka wa fedha 2023/24, imebainisha hoja za ubadhirifu unaotokana na upotevu ma fedha, ufisadi na ukiukwaji wa sheria za manunuzi zenye thamani ya shilingi trilioni 2.56

Ripoti ya CAG imeainisha ubadhirifu wa wazi na dhahiri uliofanywa na serikali ya CCM kuwa ni Trilioni 1.116:

  • Ubadhirifu katika Serikali Kuu – Bilioni 141.95
  • Ubadhirifu katika Miradi ya Maendeleo – Bilioni 190.00
  • Ubadhirifu katika Serikali za Mitaa – Bilioni 134.36
  • Ubadhirifu katika Mashirika ya Umma – Bilioni 650.02
Katika ubadhirifu huu, ripoti ya CAG inaonesha ya kwamba takribani Bilioni 506 pekee ya ubadhirifu unatokana na matumizi yasiyo na tija na ukusanyaji wa mapato nje ya mfumo wa kielektroniki.

Kwa mara nyingine tena tunaona tija ya serikali ya CCM ni kuendeleza ufujaji na upigaji; tija ya CCM sio ustawi wa wananchi; tija ya CCM ni kutufanya tuendelee kuwa mateja wa mikopo huku tukipoteza kiasi kikubwa cha mapato yetu ya ndani.

Ripoti ya CAG inaendelea kubaini kwamba, jumla ya kiasi cha Trilioni 1.446 kinatokana na upotevu wa fedha za umma; ambapo Trilioni 1.34 pekee zinatokana na madeni ya mapato yasiyokusanywa [ada, faini na gharama za huduma] na hivyo kuwa sehemu ya fedha za umma zinazopotea.
WhatsApp Image 2025-05-10 at 16.09.25_2c971353.jpg
Pamoja na kuainisha ubadhirifu na upotevu wa fedha za umma wa kiasi cha Trilioni 2.56, vivyo hivyo, ripoti ya CAG imeonesha upotevu mkubwa wa mapato kwa kutokukusanywa kwa ushuru wa huduma kutoka taasisi 29,432; ambapo kati ya taasisi hizo, taasisi 27,663 (asilimia 93.98) zinapatikana katika Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni pekee.

Inastaajabisha kwamba badala ya kuhakikisha ufanisi katika ukusanyaji wa mapato, katika wakati ambao nchi inaupungufu wa makusanyo ya Trilioni1.45, CCM imeamua kukumbatia ubadhirifu. Ni ubadhirifu kwenye mauzo, manunuzi, mikataba, makusanyo, ruzuku, matumizi, malipo; ni ubadhirifu kila kona. CCM inafanya maksudi kukuhakikisha kunakosekana ufanisi katika ukusanyaji wa mapato haya, ili mradi kujitengenezea mianya ya rushwa, upigaji na ufisadi, unaolenga kuwaneemesha wao na kuwafukarisha Watanzania wengi.
WhatsApp Image 2025-05-10 at 16.09.26_078fd260.jpg
Pamoja na kumulika na kuainisha ubadhirifu na upotevu, ACT Wazalendo tunasisitiza mambo yafuatayo:

  • Tunasisitiza kwamba watumishi wote wanaohusika na kuwezesha kuwepo na kushamiri kwa vitendo vya ubadhirifu na upotevu wa mapato wakamatwe na hatua kali za kisheria na kiutawala zichukuliwe.
  • Tunatoa rai kwa vyombo vya habari na TAKUKURU kutekeleza wajibu wao wa kiukombozi kuangazia, kumulika na kuweka hadharani vitendo vya ubadhirifu na upotevu wa mapato.
  • Tunasisitiza kwamba serikali ihakikishe kwamba mfumo wake wa kielektroniki unafanya kazi kwa wakati wote na maeneo yote na kuweka utaratibu wa kutokuruhusu miamala kufanyika nje ya mifumo hiyo.
  • Tunasisitiza kwamba viongozi, wawakilishi, vyama vya siasa, wadau wa maendeleo pamoja na wananchi kuhakikisha tunakata mirija ya ubadhirifu ili kuhakikisha kunakuwepo na ustawi wa kweli wa watu.
ACT Wazalendo tunatamka kwamba hatuwezi kuendelea kukaa tu na kubaki kuwa mashuhuda tu wakati fedha za umma zinaliwa, miradi ya maendeleo inatelekezwa na Watanzania wanaumia na kuteketea.

Ucheleweshwaji na Kutelekezwa Kwa Miradi ya Maendeleo
Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2023/2024 imebainisha uwepo wa miradi iliyotelekezwa, kusimama au kuchelewa kutekelezwa, hali inayosababisha hasara kubwa kwa serikali na kuchelewesha maendeleo ya wananchi.

CAG ameonesha jumla ya miradi 136 yenye thamani ya Shilingi Trilioni 1.34 imesuasua huku baadhi ya miradi ikiathiriwa kwa kucheleweshwa hadi asilimia 92. Hii inaonyesha udhaifu mkubwa wa usimamizi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Hali hii inatia hasira kali kuona kwa taifa maskini kama Tanzania, ambalo linapaswa kuhakikisha kila shilingi inayotengwa kwa maendeleo ya wananchi badala yake inaishia kupotea kwenye matumbo ya wachache.
WhatsApp Image 2025-05-10 at 16.09.23_cd377f0e.jpg
Aidha, CAG ameonesha utekelekezwaji wa miradi wenye mamilioni ya fedha. Katika sekta za barabara, afya, maji na miundombinu, ripoti inaonyesha miradi mingi imetelekezwa, ikiwemo miradi 41 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 558.63 ambayo ilitelekezwa kwa sababu ya ukosefu wa fedha na mipango duni.
  • Miradi 22 ya Miundombinu ya Barabara yenye thamani ya shilingi bilioni 507.6
  • Miradi 6 ya Afya yenye thamani ya shilingi 35.75
  • Miradi 12 sekta ya maji- shilingi bilioni 13.8
  • Huduma za magereza- shilingi bilioni 1.44
Serikali ya CCM haijali wala kutoa thamani ya kila shilingi inayokusanya. Inakopa matrilioni ya shilingi kwa jina la maendeleo, halafu inatelekeza miradi au inaisimamia kwa kiwango cha aibu. Matokeo yake ni wananchi kuendelea kutaabika bila huduma za msingi huku viongozi wakiendelea kuishi maisha ya kifahari. Tunaitaka serikali iwajibike kwa kila senti iliyotumika kwenye miradi iliyokwama. Tunataka uchunguzi huru, kufutwa kwa mikataba mibovu, na hatua kali kwa waliohusika na utelekezwaji wa miradi hii.

Hatari ya kasi ya Kuongezeka kwa Deni la Taifa
Katika ripoti ya mwaka 2023/24, Deni la taifa limepanda hadi kufikia Shilingi Trilioni 97.35 kutoka Trilioni 82.25 mwaka uliopita. Hili ni ongezeko la zaidi ya Shilingi Trilioni 15 kwa mwaka mmoja pekee. Hali hii inaweka hatari mustakabali wa taifa kwani baadhi ya viashiria kama “uwiano wa kulipa deni kwa mapato’’ vinakaribia ukomo wa hatari uliowekwa na taasisi za kimataifa.

Kasi ya ukuaji wa Deni la Serikali ya awamu wa Sita chini ya Rais Samia kwa miaka minne imekuwa kubwa sana. Ongezeko hili halijawahi kutokea tangu nchi yetu ipate uhuru. Amekopa kiasi cha shilingi trilioni 33.18 ikijumuisha shilingi trilioni 17.7 (mtaji) na shilingi trilioni 9.48 (riba).

CAG ameonesha kuwa uwiano wa kulipa deni kwa mapato ya ndani umefikia asilimia 14.5, ukikaribia kikomo cha tahadhari cha asilimia 18. Aidha, uwiano wa kulipa deni kwa mauzo ya nje ni asilimia 11.7, ukielekea ukomo wa hatari wa asilimia 15.

Maana yake, sehemu kubwa ya mapato ya serikali inaishia kulipa madeni badala ya kuendeleza huduma kwa wananchi. Mapato ya serikali kwa mwezi Januari 2025, kwa Mfano ilikusanya trilioni 2.63 katika makusanyo hayo serikali ilitumia shilingi trilioni 1.2 kulipia huduma ya deni. Uchambuzi wetu unaonesha kuwa Serikali ya Tanzania inalipa kati ya shilingi bilioni 900 hadi shilingi trilioni 1.3 kwa mwezi kwa ajili ya huduma za deni. Hii inaonyesha mzigo mkubwa wa deni kwa Serikali, ambao unaathiri uwezo wa kutoa huduma muhimu kwa wananchi kama afya, elimu, na miundombinu.

Aidha, Uchambuzi wetu wa matumizi ya serikali kwa mwaka wa ukaguzi 2023/24 unaonesha kuwa fedha za makusanyo ya ndani yalikuwa trilioni 29.99. Mgawanyo wa matumizi ni kuwa trilioni 10.35 zilitumika kwa ajili ya kulipa mishahara, shilingi trilioni 18 zilitumika kuhudumia deni la serikali na matumizi mengineyo. Huku miradi ya maendeleo ilipangiwa shilingi trilioni 15.1 ambayo yote hii ilitegemea mikopo.

Yaani kila kila shilingi 100 inayokusanywa shilingi 65 inaenda kulipia mshahara wa Rais na watu wake, posho, masurufu na chai huku shilingi 35 ndio inawekezwa kwa maendeleo ambayo yote inategemea mikopo. Ndio maana wananchi wakiuliza maswali kuhusu deni, Serikali imekuwa ikijitetea kuwa Deni ni himilivu, maana yake wao ndio wananufaika.

Lakini, ukweli ni kuwa athari za mzigo huu wa madeni ni kubwa kwa wananchi wa kawaida; Fedha zinazopaswa kwenda kujenga shule, hospitali, maji safi na barabara zinamezwa na kulipa riba ya madeni. Serikali kwa kutumia sehemu kubwa ya mapato kulipa madeni, inashindwa kuwekeza katika huduma za kijamii zinazogusa maisha ya kila Mtanzania. Badala ya kutoa huduma bora, tunajikuta tukilipa kwa makosa ya sera za kifisadi na matumizi holela ya serikali iliyopo madarakani.

Katika uchambuzi wetu wa ripoti ya CAG 2023/24 mwaka huu hapo juu tumeonesha ubadhirifu wa fedha za umma katika utekelezaji wa miradi na majukumu mbalimbali ya wizara, taasisi za Serikali na Mashirika ya umma bila kuchukuliwa hatua za uwajibikaji. Jumla ya hoja zenye thamani ya shilingi trilioni 2.56 zilihusishwa na ubadhirifu.

Kutokana na uchambuzi wetu kwenye sehemu na suala hili nyeti, ACT Wazalendo tunasisitiza yafuatayo:

  • Serikali iache kuhadaa wananchi kuhusiana na hali halisi ya kitaifa, kwa kuwa deni la taifa halitoshi kutazamwa katika jicho la kiuchumi wa jumla jumla pasipo kuangalia hoja za kina siasa-uchumi na kijamii.
  • Serikali inapaswa kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha ufanisi katika makusanyo ya ndani, ili kujiwekeza zaidi katika uchumi unaojitegemea.
  • Serikali inapaswa kuzingatia mipango yake na kujiepushia na mienendo ya ulafi wa mikopo isiyokuwa na mipangilio.
ACT Wazalendo tunasisitiza kwamba serikali ya CCM imeshindwa kutoa suluhu na mbadala wa kiuchumi.

Madai ya Wazabuni na Wakandarasi Yenye Thamani ya Trilioni 4.5

Ripoti ya CAG ya mwaka 2023/24 imeendelea kuonesha kuwa suala la madai ya wazabuni na wakandarasi limekuwa tatizo sugu. CAG amebaini serikali kuwa na madai yasiyolipwa ya Shilingi Trilioni 4.56, ambapo Shilingi Trilioni 3.53 hazijalipwa kwa zaidi ya mwaka mmoja. Hiki ni kiwango kikubwa sana cha Fedha za watu ambazo Serikali inazishikilia mkononi baada ya kupokea huduma za Wazabuni hao.

Hali hii inasababisha mdororo wa uchumi, kwani Serikali inashikilia Fedha za wakandarasi, wafanyabiashara na watoa huduma na hivyo kudumaza shughuli za uzalishaji mali na wakati mwingine kufukarisha wananchi. Kushikiria fedha hizi pia serikali imeshikilia mamilioni ya ajira ya vijana. Wakandarasi wakikosa malipo ya kazi walizotekeleza, hawana uwezo wa kulipa wafanyakazi wao wala kuajiri zaidi. Katika sekta ya ujenzi, hasa wa barabara, sehemu kubwa ya ajira hutolewa kwa vijana wa maeneo husika. Miradi inapokwama, vijana hukosa chanzo cha kipato, hali inayoongeza tatizo la ukosefu wa ajira na umasikini katika jamii.

Mbali na athari za kiajira lakini pia madai ya muda mrefu yanazalisha riba na kuongeza mzigo wa madeni kwa Serikali na kulitia hasara Taifa. Kwa Mwaka 2023/24 pekee imesababisha wakandarasi kudai riba ya zaidi ya Shilingi Bilioni 55.55, pesa ambazo zingetumika kwa huduma muhimu kwa wananchi kama afya, elimu na maji.

Vile vile, kushindwa kwa Serikali kulipa madeni ya wakandarasi na watoa huduma kumechangia kudorora kwa kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa barabara, hospitali, shule na miundombinu ya maji. Ndio maana tunaona barabara maeneo mbalimbali nchini zimesimama (hakuna ujenzi unaendelea), hazifanyiwi matengenezo, ukarabati au kuendelea kujengwa mathalani barabara ya Rufiji – Mtwara.

Mwenendo wa madai ya Wazaburi na Watoa Huduma kwa Serikali kwa miaka mitatu kuanzia 2021/22 hadi 2023/24 ni kama ifuatavyo;

​
NaMwaka wa FedhaDeni (Trilioni za Shilingi)
2021/223.62
2022/234.4
2023/244.56



Tunarudia tena mwaka huu 2025 Serikali illipe madeni yote ya wazabuni na wakandarasi kwa mkupuo, ili kufufua miradi iliyosimama na kuchochea mzunguko wa fedha katika uchumi.

Pia, tunaitaka Serikali iweke mpango mahsusi wa kulipa madeni ya nyuma kupitia Hati Fungani, ili yasikwepe kwenye mipango ya bajeti kila mwaka.

Mwisho, Serikali iweke mfumo mzuri wa kulipa watoa huduma kwa wakati ili kuwasaidia kukuza shughuli zao na hivyo kuongeza ajira na kuondoa umasikini wa Wananchi.

Serikali imeendelea kutokulipa malimbikizo ya wafanyakazi na pensheni

Uchambuzi wetu katika ripoti ya CAG 2023/24 imeonesha kuwa Serikali inaendelea kukalia fedha za malimbikizo mbalimbali ya wafanyakazi na fedha za pensheni hazipelekwi kwenye mifuko,

Serikali haijalipa malimbikizo ya Bilioni 299.3

CAG ameeleza mamlaka za serikali za mitaa na Serikali kuu zimekua zikizuia fedha halali za watumishi walizotakiwa kuzipata kama malimbikizo ya mishahara ya wafanyakazi, kupandishwa madaraja, stahiki za wastaafu na posho za kisheria kama vile likizo, kujikimu, safari, uhamisho.

Serikali ya CCM haijali kuhusu haki, stahiki na maslahi ya watumishi wa umma wa ngazi za chini, watumishi wengine kama Rais, mawaziri, wabunge, makatibu wakuu, wakurugenzi na wakuu wa mashirika wamekua wakijipendelea kupata posho, takrima za ofisi na kupandishana vyeo huku watumishi wengine wakiendelea kfatilia malimbikizo yao kwenye ofisi za maafisa utumishi bila majawabi yoyote.

Kutolipwa fedha hizo ni kinyume na kanuni ya utumishi wa umma inayoelekeza mfanyakazi yeyote wa Serikali pale anapopandishwa daraja au kuteuliwa kwenye nafasi ya kiwango cha juu au kuhamishwa, alipwe malipo yanayostahili. Kuacha kulipa madai yao inapelekea kushusha morali ya watumishi na kuondoa ufanisi katika utendaji na kuwahudumia wananchi.

Bilioni 4.73 za wafanyakazi kutopelekwa kwenye mifuko ya Pensheni.

Licha ya serikali kutolipa malimbikizo na stahiki nyengine za wafanyakazi CAG ameendelea kuthibitisha nia ya CCM na serikali yake kutopeleka fedha za wafanyakazi kwenye mifuko ya pensheni. Kutopeleka fedha kwenye mifuko ya pensheni ni jitihada ya serikali ya kutaka Kuua mifuko ya hifadhi ya jamii na kukandamiza wastaafu kwa kuwakata makato makubwa kupitia kikokotoo na kuwacheleweshea kiinua mgongo. Kuchelewa kupeleka fedha hizo kwenye mifuko stahiki kunapelekea kuongezeka kwa gharama zinazotokana na adhabu, mathalan mamlaka za serikali za mitaa zilitakiwa kupeleka Bilioni 3.39 lakini kutokana na ucheleweshaji wamepigwa adhabu ya kulipa Bilioni 10.

Madai haya ya wafanyakazi na kutopeleka michango kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii kunaongeza ugumu wa maisha wakiwa wafanyakazi na kunahatarisha haki zao wakati wa ustaafu na kutishia uhimilivu wa mifuko ya pensheni. CAG anathibitisha jinsi ambavyo Serikali ya Chama cha Mapinduzi imeshindwa kuwathamini wafanyakazi wa umma nchini.
WhatsApp Image 2025-05-10 at 16.09.33_7a9a62da.jpg
ACT Wazalendo; tunaona kuwa Serikali imeendelea kuwatupa na kuwapuuza wafayakazi wake, tunaitaka serikali kuchukua hatua zifuatazo;

Mosi, tunataka serikali iwaheshimu watumishi na wastaafu kwa kuwatendea haki, iwalipe malimbikizo na stahiki zao zote kwa wakati na ipeleke fedha za watumishi zinazokwenda kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii haraka.

Pili, tunataka wafanyakazi watumie vyama vya wafanyakazi kudai haki zao, wasikubali vyama vya kutetea haki na maslahi yao vitafune pesa zao huku vikifumbia macho kusiginwa kwa haki zao, wafanyakazi, msikubali vyama vyenu kugeuzwa vijiwe vya machawa

Hujuma na usimamizi mbovu wa mashirika ya Umma.

Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kila mwaka imekua ikibaini mapungufu makubwa katika mashirika ya Umma, ikiwa ni pamoja na hasara, ubadhirifu katika manunuzi, usimamizi wa mapato, matumizi, mikataba na uendeshaji mbovu. Kwa sehemu kubwa watumishi katika mashirika haya wanakosa weledi na utaalamu kwakua watendaji wakuu na wenyeviti wa bodi wamekua wakipatikana kwa kujuana na kuteuliwa na waziri au Rais.

Serikali ya CCM imeshindwa kuendesha hata mashirika ya Umma ambayo hayana haja yoyote ya kupata hasara, kitu pekee inachoweza na kukiwaza ni kuyauza na kuyabinafsisha mashirika hayo. Kushindwa kuendesha mashirika haya ni kielelezo cha Kushindwa kwa kuendesha Serikali, kwa taarifa hii ya CAG katika mashirika ya Umma tunauambia Umma kuwa CCM imechoka na inapaswa kuondolewa.

Katika ripoti yake CAG ya 2023/24 anatoa mfano wa Masirika ya Umma 11 tu yamerikodi hasara ya Bilioni 403.06, mashirika hayo ni;

Shirika la Reli Tanzania Bilioni 224.59

Kampuni ya Ndege Tanzania Bilioni 91.8

Shirika la Mawasiliano la Tanzania Bilioni 27.78

Shirika la Posta Tanzania Bilioni 23.63

Kampuni ya Mkulazi Bilioni 19.04

Kiwanda cha Kuzalisha Bidhaa za Kibiolojia Tanzania Bilioni 4.3

Kiwanda cha Dawa Keko bilioni 1.84

Shirika la Masoko ya Kariakoo billion 1.45

Kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi Tanzania bilioni 1.34

Katika kituo cha uwekezaji cha APC bilioni 6.73

Soko la Bidhaa Tanzania Milioni 561.92

Hasara hizi zinatokana na kukosa weledi, uzembe, hujuma, na ukosefu wa mifumo madhubuti ya uwajibikaji, mfano mmoja wa hujuma ambao CAG ameonesha ni matumizi yasiyo na tija ya shilingi bilioni 371.42 pamoja na matumizi yasiyostahili ya shilingi bilioni 6.75 katika mashirika ya umma. Hiki ni kiashiria cha uhujumu wa mashirika ya Umma unaofanywa na watumishi wasio na weledi na uzalendo, waliojawa tamaa na ufisadi.

Ni jambo la kusikitisha kuwa licha ya hasara yote hii na kuwa wazi na kurudiwa kila mwaka, hatua madhubuti hazichukuliwi. Viongozi wa mashirika haya pamoja na bodi zao wanaendelea kubaki madarakani licha ya kuhusishwa na ubadhirifu mkubwa. Badala ya kushughulikia kiini cha tatizo ambacho ni usimamizi mbovu na ukosefu wa uwajibikaji, viongozi wa serikali wamekuwa wakitoa mapendekezo ya kuyavunja mashirika haya au kuyabinafsisha, kana kwamba ubinafsishaji ndiyo tiba pekee ya matatizo yao.

Tuna mifano mingi duniani ya mashirika ya umma yanayofanya vizuri kwa sababu yanasimamiwa kitaalamu na kwa uwazi. Shirika kama Ethiopian airways, Huawei, ni mfano wa mashirika ya umma yaliyopata mafanikio makubwa duniani kote kwa sababu ya weledi wa usimamizi, si kwa sababu ya kubinafsishwa kuimarisha utendaji, kuongeza uwajibikaji, na kuhakikisha usimamizi wa kitaalamu.

Kwa msingi huo, ACT Wazalendo inasisitiza kuwa mashirika ya umma yanaweza kuwa imara, ya kisasa na yenye tija ikiwa yatasimamiwa vizuri. Kufuatia changamoto zilizojitokeza kwenye mashirika ya umma tunataka hatua zifuatazo zichukuliwe,

Mosi, Msajili wa Hazina atoe taarifa ya hatua zilizochukuliwa dhidi ya ubadhirifu, na iwapo hakuna hatua yoyote aliyochukua, awajibishwe na mamlaka zake za uteuzi.

Pili, Bodi na Menejimenti za mashirika yenye hoja za wazi za kiukaguzi zivunjwe mara moja, na wahusika wawajibishwe kwa kufilisiwa mali zao na kurejesha fedha za umma.

Tatu, Uongozi wa mashirika ya umma upatikane kwa njia ya ushindani, si kwa upendeleo wa kisiasa, upendeeleo au undugu.

Kiburi cha serikali kinaiTia hasara ATCL

Ripoti ya CAG Imeonesha kuwa Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL) inaendelea kupata hasara kwa miaka saba mfululizo, na hasara hii imefia shilingi biioni 534. Licha ya kupokea ruzuku kutoka serikalini kila mwaka, Mwaka 2023/24, ilipokea shilingi bilioni 70 kwa ajili ya mishahara ya wafanyakazi na gharama zingine za wafanyakazi, pamoja na shilingi bilioni 57 kama ruzuku ya maendeleo kwa miradi ya uwekezaji. Licha ya kupokea fedha nyingi za ruzuku, hasara halisi ya Kampuni ya Ndege Tanzania ni shilingi bilioni 91.8 mwaka 2023/24.

Hasara yote hii haitokani na kukosa faida katika uendeshaji bali inatokana na gharama kubwa za kukodi ndege kwa TGFA, pamoja na kodi na matengenezo ya ndege mpya zilizonunuliwa, ambazo ziliongeza gharama kwa Kampuni. Tumekuwa tukirudia hoja hii kila mwaka, kuiambia serikali inacheza sarakasi isiyo na maana yoyote na kuigharimu nchi, utaratibu wa TGFA kumiliki ndege sio endelevu kwa ATCL.

TGFA tangu 2016 ilipowekwa ofisi ya Rais imekua ikinunua ndege mbovu, zilizopitwa na wakati na hasara za matengenezo na bima zinaachwa mabegani mwa ATCL, Hii ndio kusema kuwa Ikulu ya Magufuli ililifanya hili kwa siri na sasa Rais Samia anaendelea na jambo hili linaloathiri uendelevu wa ATCL na kusababisha kutumika kwa Fedha za Umma kama ruzuku kwa shirika lenye uwezo wa kupata faida.

Kuhusu TGFA kununua ndege mbovu CAG anasema “nilibaini kuwa jumla ya shilingi bilioni 20.63 zilitumika kwa ajili ya matengenezo na bima ya ndege aina ya DASH 8 Q300 (5H-MWF) tangu ilipopelekwa Malta kwa ajili ya matengenezo Novemba 2020 …Sababu kuu zilizoainishwa ni pamoja na kupitwa na wakati kwa muundo wa ndege”

Iwapo ATCL itamiliki ndege, gharama za ukodishaji zisingekuwepo kwenye vitabu vyake vya mahesabu hata hivyo kama ATCL ingemiliki ndege isingenunua ndege chakavu na mbovu na kama ingeharibika ingeshughulikia kwa wakati suala la ubovu wa ndege na CAG angeikagua.

ACT Wazalendo tunaendelea kuitaka Serikali iimilikishe ATCL ndege zote inazokodishiwa, ifute madeni ya kukodi ndege na kuirejesha TGFA chini ya Wizara ya Uchukuzi.

Tunamtaka CAG Kufanya ukaguzi maalum wa manunuzi ya ndege tangu tulipoanza kununua ndege 2016 hadi sasa, kwenye manunuzi ya ndege kuna madudu makubwa yanafichwa, kwakua ni fedha za Umma tunataka ufanyike ukaguzi maalum.

Hatari ya Upigaji wa Bilioni 262.34 za CSR za Mradi wa Bwawa la Mwl. Nyerere

Wakati mradi wa ujenzi wa bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere ukiwa umekamilika kwa zaidi ya asilimia 99, CAG ameeleza na kuibua hoja ya kutokutolewa kwa fedha za miradi ya huduma kwa jamii (CSR) zenye thamani ya shilingi bilioni 262.34. Taarifa na hoja hii ya CAG imeendelea kujitokeza kwa takribani miaka sita, ambapo, ripoti za CAG zimekuwa zikisisitiza kwamba fedha hizi zilitakiwa kuanza kutolewa tangu tarehe 13 Januari 2019.

Kwa miaka sita, serikali ya CCM imeendelea sio tu kupuuza hoja za CAG, bali imeendelea kuwadhihirishia watu wa Rufiji, Kibiti, Mkuranga, Liwale na maeneo mengine yanayoathiriwa na mradi wa kufua umeme wa bwawa la Mwalimu Nyerere kwamba haiwajali wala kuwazingatia. Muendeo huu wa serikali unatoa tafsiri moja tu kwamba genge la watu wachache wa TANESCO na TAMISEMI na viongozi wengine wa serikali na CCM wanataka kuzipiga fedha hizi ili kujinufaisha wao wenyewe.

Inasikitisha na inashangaza kwamba fedha hizi [bilioni 262.34] ambazo zimeshasainiwa, na hivyo zipo au zinapaswa kuwepo, zinafanywa kama hisani na zinatengezewa mazingira ya upigaji, licha ya kwamba ni haki halali ya jamii zinazoathirika na mradi, pamoja na Watanzania kwa ujumla. Tabia hii ni muendelezo wa ulafi na vitendo haramia vya CCM katika kutafuna na kufanya ubadhirifu kwa fedha za miradi mbali mbali mikubwa inayojengwa nchini.

Pamoja na ufisadi huu wa fedha za miradi ya huduma kwa jamii (CSR), CAG amebaini kuwa mradi wa ujenzi wa bwawa la mwalim Nyerere, haukua na mpango wowote wa dharura na usalama wa kukabiliana na majanga. Athari yake ni kwamba inapotokea dharura yoyote madhara makubwa yanaweza kuikumba jamii inayozunguka mradi huo au hata kuathiri mradi wenyewe. Kielelezo tosha ni tukio la mwaka 2024 ambapo TANESCO ilifungulia maji na kusababisha maafa katika maeneo ya Rufiji na Kibiti lilikuwa kielelezo cha kutokuwepo kwa maandalizi ya usalama.

Maafa haya na upigaji huu unatoa picha moja tu, kwamba serikali ya CCM haijali na wala haina nia yeyote ya kuhakikisha ustawi na maendeleo ya wananchi. Kwa mantiki hii, ACT Wazalendo tunasisitiza mambo yafuatayo kufanyika:

  • Tunasisitiza wananchi wa Rufiji, Kibiti, Mkuranga, Liwale na maeneo mengine yanayoathiriwa na mradi kuwashinikiza madiwani na wabunge wao kuwajibika kusimamia na kuhakikisha fedha hizo, bilioni 262.34, zinatolewa na kuhudumia jamii zao husika.
  • Tunapinga na kukemea janja janja zinazofanywa za kutaka kuchepusha fedha, bilioni 262.34, hizo kuhudumia jamii nyingine huku zikipuuza na kutokutoa kipaumbele kwa watu wa Rufiji, Kibiti, Mkuranga, Liwale na maeneo mengine yanayoathiriwa na mradi.
  • Tunaitaka serikali iweke na kutekeleza mipango madhubuti ya dharura na usalama ili kuiwezesha jamii zinazoathiriwa na mradi kukabiliana na madhara na majanga.
  • Tunasisitiza wananchi na wadau wa mazingira na maendeleo kuunganisha nguvu kuishinikiza serikali kuweka na kutekeleza mpango wa dharura na usalama ili kuziepusha jamii zinazoathiriwa na mradi kupata madhara, kama yaliyopatikana mwaka 2024.
  • Mwisho, tunaitaka wizara ya nishati, na serikali kwa ujumla, kuhakikisha mradi huu unakamilika na unasaidia katika kupunguza gharama za umeme nchini; na vivyo hivyo unatuepushia na kuondoshea kabisa adha ya umeme kukatika katika.
Ukosefu wa mabasi ya Mwendokasi umeleta adha ya usafiri Dar es salaam

Kwa zaidi ya ripoti tatu 2020/21/ 2022/23 ma sasa 2023/24 tumekua tukieleza kuhusu mradi wa mwendokasi, mradi ambao badala ya kuwa faraja umegeuka adha kubwa ndani ya Jiji la daer es salaam.

Mradi huu ambao unajengwa kwa fedha za mkopo wa Benki ya Dunia na wadau wengine wa maendeleo umeendelea kusuasua kukamilika, kujengwa chini ya kiwango kutokana na usimamizi usimamizi mbovu kwa wakala wamabasi yaendayo haraka (DART)ambayo ipo chini ya OR-TAMISEMI, katika ripoti ya Mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali CAG ameoesha sababu kuu ya adha ya usafiri dar es salaam ni;

Upungufu wa mabasi ya UDART

Uchambuzi wetu wa ripoti hii ya CAG umebaini kuwa bado mradi huu una upungufu mkubwa wa mabasi yanayofanyakazi, Mkaguzi anabainisha kuwa DART na UDART waliingia mkataba wa kuwa na mabasi 210 lakini hadi anafanya ukaguzi Novemba 2024 ni mabasi 111 pekee ndio yalikua yanatoa huduma huku mabasi 99 yakiwa hayafanyi kazi kwa uchakavu na kuhitaji matengenezo, huu ni upunufu wa asilimia 49.

Kukosekana kwa mabasi kunaongeza adha ya msongamano wa abiria, kuchelewa kwa huduma kwa wateja na kuchelewesha mzunguko wa Uchumi. Kwa upande mwengine, Mpaka sasa barabara ya Mbagala – Mjini, Mjini - Gongolamboto, keko - Mjini hakuna kabisa magari hayo licha ya mradi kukamilika kwa kiasi kikubwa. Hata barabara ya Morogoro inayokwenda Kivukoni na kariakoo haina magari yakutosheleza abiria. Hii inasababisha kukosekana kwa thamani halisi ya fedha na kutotatua tatizo la usafiri jijini Dar es salaam.

Huu ni uthibitisho kuwa Serikali ya CCM ilianzisha mradi huu kwa kukurupuka, haikua na mipango thabiti ya kuutekeleza matokeo yake badala ya mradi huu kuwa msaada kwa umma umegeuka kuwa mzigo.

Tumemsikia waziri wa Ofisi ya Rais TAMISEMI ndg. Mohammed Mchengerwa akilieleza bunge kuwa jambo hili sasa linapata ufumbuzi na kwamba wamepata wawekezaji watatu, hii si mara ya kwanza kwa waziri huyu kusema maneno hayo, wakati huu ameongeza madoido tu lakini maneno ni yaleyale lakini hayatekelezwi, mradi umkamilika kwa zaidi ya m,iaka miwili hauna hata gari moja. Tunataka atambue jambo moja tu. wananchi wamechoka maneno yake ya hadaa.

ACT Wazalendo Tunapendekeza yafuatayo;

Tuna mashaka kuna mtu au kikundi cha watu kinaihujumu DART, Hivyo Mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali CAG afanye uchunguzi wa zabuni ya hao wawekezaji waliotangazwa na waziri, CAG achunguze wawekezaji hawa wamepatikanaje.

Tunataka mamlaka ya serikali za mitaa dar es salaam (ilala, kinondoni, temeke, ubungo, temeke na kigamboni) waendeshe mradi wa mabasi yaendayo haraka.

Tunataka mabasi mapya yote yafungwe mitambo ya gesi asilia (CNG) na mabasi yote yatumie gesi asilia.

Uwekezaji kiduchu kwenye miundombinu ya barabara

Uchambuzi wetu wa ripoti ya CAG 2023/24 tumebainikuwa Serikali inatenga fedha kiduchu kwa ajili ya ujenzi wa barabara. Katika fedha inayotengwa sehemu kubwa ni kwa ajili ya kulipa madeni ya wakandarasi na kufanya maboresho ya barabara. Jambo hili linafanya Tanzania kwa zaidi ya miaka 63 tangu uhuru kubaki na barabara zisizopitika au kupitika kwa shida. Isivyo bahati Serikali ya CCM haijali kabisa hali na maisha ya wananchi hasa wazalisahaji wadogo vijijini ambao wananshindwa kupata tija ya mazao yao kwa kushindwa gharama za kuyafikisha sokoni. CAG anaonesha mgawanyo wa bajeti za barabara kama ifuatavyo.

TANROADS imepata bilioni 11.71 tu kwa ajili ya ujenzi wa barabara mpya.
Kwa mujibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali imeendelea kukumbatia mtindo wa kupanga bajeti kwa maneno bila dhamira ya utekelezaji. Katika sekta muhimu kama ya barabara, CAG amebainisha kuwa Bajeti iliyoidhinishwa kwa ajili ya kazi za barabara ilikuwa Sh. trilioni 1.05 hata hivyo katika fedha hizo fedha iliyotolewa ni shilingi Bilioni 684 tu, katika fedha hizi Bilioni 672.16 zimetolewa kwa ajili ya maboresho ya barabara zilizoharibika na Kimbunga Hidaya na janga la EL nino na malipo ya madai ya wakandarasi na ni shilingi Bilioni 11.71 ambayo ni sawa na 3% tu ndio ilibaki kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za bajeti za mwaka 2023/24

Wakala wa barabara vijijini (TARURA) imepata bilioni 99.8
CAG amebaini kuwa wakala wa barabara vijijini (TARURA) Ilitengewa kiasi cha Sh. bilioni 251.50 kutoka kwa Bodi ya Mfuko wa Barabara, ambapo Sh. bilioni 229.14 zilitengwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara na Sh. bilioni 22.36 kwa ajili ya ujenzi barabara mpya, Hata hivyo, kufikia Juni 2024, ni 40% sawa na Sh. Bilioni 99.84 tu ya kiasi kilichotengwa kilitolewa.

Hivi ndio namna ambavyo serikali inawekeza kwenye miundombinu, kwa mwendo huu kama CCM isipodhitiwa na kuondolewa madarakani basin chi hii itachukua miaka zaidi ya mianne kuwa na mitandao kamili ya barabara nchini.

Bilioni 648.38 kutopelekwa kwenye mfuko wa barabara (RFB)

Wakati TANROADS na TARURA zinapokea bajeti chini ya 50% Fedha zinazokusanywa kwa ajili ya maendeleo ya barabara hazipelekwi kwenye mfuko wa maendeleo ya barabara. Leo hii kila mtu anaponunua petrol au diesel anakatwa fedha ya ushuru wa barabara. Fedha hii kwa mujibu wa sheria haipaswi kupelekwa kwenye mfuko mkuu wa Serikali bali kwenye mfuko husika. Lakini serikali ya CCM katika Trilioni 1.4 zilizokusanywa walipeleka kwnye mfuko wa barabara Bilioni 836.7 na kuzitokomeza bilioni 648.38 kwenye mambo yasiyohusika.

Serikali ya CCM imekuwa ikijinasibu kwa ujenzi wa barabara huku ikishindwa kufanikisha hata kile inachokiahidi kwenye vitabu vya bajeti, hata fedha inayotokana na barabara zenyewe haitumiki kuendeleza barabara hizo. Kila mwaka Serikali inatengeneza bajeti hewa. Inatoa ahadi za kiinimacho kwenye sekta ya barabara, lakini hakuna dhamira ya kweli ya kuzitekeleza. Upungufu huu ni ushahidi wa kushindwa kwa Serikali kupanga kipaumbele kwa maendeleo ya watu.

ACT Wazalendo, tunataka Serikali ifuate sheria, Fedha zote zinazokusanywa kwa ajili ya ujenzi wa barabara zitumike kwenye ujenzi wa barabara na si vinginevyo.

Pili, Serikali kupitia bajeti ya seikali itenge fedha za kutosha kwenye ujenzi wa barabara za vijijini zinazosimamiwa na TARURA na barabara zinazounganisha mikoa.

HITIMISHO
Uchambuzi wa ripoti ya CAG kwa miaka minne kuanzia mwaka 2020/21 hadi 2023/24 tumeona kuna hoja kubwa zinazojirudia rudia.

Mathalani hoja ya ubadhirifu kwa miaka yote minne CAG ameibua hoja zenye jumla ya thamani ya shilingi trilioni …… Hizi ni pesa zilizopotea, kuliwa au zimetumika bila tija kwa Watanzania walio wengi. Tumeeleza kwa undani, kama fedha hizi zingesimamiwa vizuri, tungepunguza kasi ya mwenendo wa deni la taifa na kuondokana na mikopo humiza inayotishia nchi yetu pigwa mnada. Watanzania wanataka kuona hatua zikichukuliwa dhidi ya ubadhirifu unaotolewa taarifa na CAG, lakini hakuna yeyote aliyechukuliwa hatua.

Kwa miaka minne tumekutana na hoja za kutelekezwa au kusua sua kwa miradi ya afya, maji na barabara nchini. Hakuna hatua zilizochukuliwa dhidi ya uzembe.

Vile vile, tumekutana na hoja ya kuachiliwa kwa shilingi bilioni 262.73 za Wajibu wa Kampuni kwa Jamii (CSR). Hakuna sababu kwanini hoja za fedha kwa ajili ya jamii inayozunguka mradi wa Bwawa la Nyerere na utekelezaji wa Mradi mzima tangu ulipoanza hazichukuliwa kwa ajili kuendeleza jamii husika mpaka mwaka 2024;

Pia, hoja za hasara za ATCL. Hakuna sababu kwanini makosa ya mchakato wa manunuzi ya Ndege, uamuzi wa kuhamishia Ikulu Wakala wa Ndege za Serikali na Mfumo wa Umiliki wa Ndege bado kurekebishwa mpaka sasa ilhali CAG anaonyesha madhara ya maamuzi hayo kila mwaka.

Majawabu tunayoyapata, katika eneo hili la usimamizi wa Fedha za Umma, ni kwamba fedha za Watanzania zinaliwa, miradi imetelekezwa na Watanzania wanaumia chini ya Serikali ya CCM. Hii inaonesha kuwa Serikali yote ni ya kifisadi, haijali wananchi na taifa letu limeendelea kuwa shamba la bibi.

Ni wakati sasa kwa Watanzania kupambana kuindoa Serikali ya CCM madarakani na kuipa dhamana ACT Wazalendo ili ihakikishe kila shilingi inayokusanywa inatumika kutoa huduma bora za jamii, ijenge uchumi imara wenye kuzalisha ajira nyingi na bora na ipambane na ufisadi na ubadhirifu wa mali za umma bila ya woga wala upendeleo.

Mwaka 2025 lazima tutumie ripoti za CAG kuwaonesha kwamba tumechoka kuona fedha za umma zinaenda kuwanufaisha watu wachache waliopo madarakani, tumechoka kuona miradi inaendelea kulala huku deni la taifa linaendelea kupaa, tumechoka kuona madai ya wafanyakazi nawakandarasi yakipewa ngonjera huku posho za chai, magari ya kifahari na matumizi ya anasa ya viongozi yakipewa kipaumbele. Tumechoka kuona shilingi zinapoaswa kwenda kubora huduma za afya na elimu zinaishia kwenye matumbo ya viongozi.

Miaka minne ya Rais Samia ni miaka ya fungulia mbwa. Tunapaswa kutumia mwa 2025, kuonesha hasira zetu dhidi ya wazembe, mafisadi na wababaishaji wa taifa letu, ambao ni CCM.

Ahsante sana.

Tunawataka wananchi kuitafakari kwa kina hali hii ya ubadhirifu na upotevu wa mapato kwa kuchukua hatua ya kuikataa CCM. Tumeshuhudia licha ya kueleza kwamba kumekuwa na ubadhirifu na upotevu wa mapato kwa zaidi ya Trilioni 2.56, serikali ya CCM haijaipa uzito unaostahili ripoti hii ya CAG, kwa kuwa wao sio wahanga wa huduma mbovu za afya, elimu, miundombinu na umasikini uliokithiri.
 
Abdul Nondo simsikii siku hizi tokea atekwe na kupigwa na kuvunjwa mguu.
Hata humu jukwaani haposti tena zile mada zake motomoto.
 
Hao hawajitambui kabisa,ukiwaambia tudai Katiba na mabadiliko ya sheria za uchaguzi na tume hawataki wanakaa pembeni.
😅😅😅😅😅..ukiwaambia habari ya reforms kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu, siku ya pili wanaenda kuchukua fomu ya kugombea kabisa. Imagine! Afu ndo watupotezee muda ati wanachambua hoja za CAG?
 
😅😅😅😅😅..ukiwaambia habari ya reforms kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu, siku ya pili wanaenda kuchukua fomu ya kugombea kabisa. Imagine! Afu ndo watupotezee muda ati wanachambua hoja za CAG?
kwa akili yako zitto asapport cdm? makalio yako yatakuwa na shida
 
Kuna vitu viwili tafauti maelezo CGA na kuchukuwa form za Ubunge
 
Back
Top Bottom