Kuna wakati niliwahi kushiriki katika kampeni ya kitaifa ya kupinga viboko shuleni. Bado nilikuwa sina mtoto. Hivi sasa ninao watoto 2, na nimewahi kumchapa mara moja tu mkubwa wa miaka 8 alipokuwa na umri wa miaka 5. Nilifikia hatua hiyo baada ya kumaliza ushauri nasaha wote. Kosa lilikuwa kumdharau mfanyakazi wa ndani.
Kabla ya kumchapa nilimwambia, masaa 6 kabla ya kumwadhibu, kuwa saa fulani nitakuchapa idadi fulani ya viboko. Nilifikiria kwa kumpa muda angelijirekebisha na pengine kuomba radhi, kinyume chake kabla ya muda nilomwambia, akarudia kosa lile lile. Kwa sababu ninampenda sana, alihisi sitomwamdhibu. Nilimchapa, sio kwa hasira, sio sehemu zinazoweza kumweka alama, na idadi ile ile ya viboko nilivyomwahidi, bila kupunguza wala kuzidisha. Tokea wakati huo amejirekebisha na amekuwa mwalimu mzuri kwa mdogo wake. Nyumbani ipo bakora, pahala pa wazi. Wanajuwa kuwa ninaweza kuitumia wakati wowote ingawa siitumii.
Kwa ufupi, kimsingi ninapinga matumizi ya viboko, (hasa namna ambavyo wazazi na walimu wengine wanatumia, kwa hasira, bila kuweka idadi maalumu ya viboko wala kuchagua wapi pa kupiga), lakini kama mzazi mwenye jukumu la kumlea mtoto wangu, sitosita kuvitumia pale inapobidi.
Kuhusu viboko na nchi za magharibi, nafikiri sasa wanajuta. Uingereza walikuwa na msemo "Spare the rod, spoil the child", lakini kwa kuendekeza haki za binadamu na hasa haki za mtoto, bila ya kuzingatia haki za mzazi, mambo yametoka kwenye udhibiti wao. Ninakubali uwepo wa haki za watoto, ambazo zinapaswa kulindwa kwa kila hali, lakini "haki za mzazi je?". Mtoto kumtukana au hata kumpiga mzazi si kosa, haki zinamlinda, lakini mzazi akijaribu kurekebisha tabia za mwanawe, anaishia korokoroni na pengine hata kunyang'anywa mtoto.