Afrika haiwezi kupata maendeleo kama itaendelea kuwa chini ya udhibiti wa mfumo wa kimataifa

Afrika haiwezi kupata maendeleo kama itaendelea kuwa chini ya udhibiti wa mfumo wa kimataifa

ldleo

JF-Expert Member
Joined
Jan 9, 2010
Posts
1,116
Reaction score
1,121
1718695551248.png

Kwa muda mrefu sasa suala la maendeleo ya nchi za Afrika limekuwa ni mjadala kwenye majukwaa mengi ya kiuchumi na kisiasa duniani. Licha ya juhudi zinazofanywa na nchi za Afrika, hatua za maendeleo zimekuwa ni polepole sana ikilinganishwa na sehemu nyingine duniani. Kuna wanaosema hali hii inatokana na sababu za ndani za Afrika, lakini kuna ukweli pia kuwa mfumo wa uchumi wa kimataifa, una mirija ya kinyonyaji ambayo inarudisha nyuma kwa makusudi maendeleo ya nchi za Afrika.

Kwa watu waliofuatilia historia ya ukombozi wa bara la Afrika, watakuwa wanakumbuka neno ukoloni mambo leo, ni neno lilioanza kutumika baada ya watu kutambua kuwa juhudi nyingi za ukombozi ziliishia kwenye kupata uhuru wa bendera, lakini mifumo mingi ya kiuchumi na kijamii iliendelea kuwa na mirija ambayo iliendeleza unyonyaji uliokuwa unafanya na tawala za kikoloni. Baadhi ya serikali za nchi za Afrika zilijitahidi kubadilisha hali hiyo, lakini kutokana historia ndefu ya nchi zilizokuwa wakoloni kuweka mifumo ya kinyonyaji, kuondoa mifumo hiyo si jambo rahisi.

Hivi karibuni mtafiti wa muda mrefu wa mambo ya Afrika Profesa Li Anshan wa Chuo Kikuu cha Peking, amesema bara la Afrika haliwezi kupata uhuru kama halitakuwa na uhuru kamili kutoka kwenye mfumo wa kimataifa. Prof. Li Anshan amefanya utafiti wa muda mrefu kuhusu uhusiano kati ya China na nchi za Afrika, na kuangalia hata sababu za kwanini uhusiano kati ya China na nchi za Afrika haujawa na matokeo makubwa zaidi kama China na nchi za Afrika zinavyotaka.

Kumekuwa na nadharia nyingi zinazoongelea hali ya kuwa nyuma kwa maendeleo ya bara la Afrika, baadhi ya nadharia hizo zinataja sababu za ndani na baadhi zinataja sababu za nje, lakini kimsingi sababu zote zinafungamana kwa karibu na kasumba ya ukoloni na mfumo wa kimataifa usio wa haki kwa nchi nyingi zinazoendelea.

Kwenye vikao vingi vya kimataifa China imekuwa ikitaja mara kwa mara kuwa mfumo wa sasa wa kimataifa unatakiwa kufanyiwa marekebisho, ili uendane na hali halisi ya dunia ya sasa na pia uendane na mahitaji halisi ya nchi zinazoendelea. Lakini juhudi za China zimekuwa zikipingwa na kukwamishwa na nchi za magharibi, ambazo zinaona uhuru wa kiuchumi wa nchi za Afrika, utakuwa na maana kuwa ukoloni mambo leo na mirija ya unyonyaji iliyokuwepo kwa muda mrefu itakuwa imekatwa.

Inawezekana kuwa ni vigumu kuelewa kuwa mirija hiyo ni ipi kwa sasa wakati nchi nyingi za Afrika zina uhuru. Tukiangalia mfumo wa biashara kati ya nchi za Afrika na nchi za magharibi, unaweza kuona kuwa biashara ambazo nchi za Afrika zina nguvu kuliko nchi za magharibi, kama vile kilimo, zinadhibitiwa kwa sheria mbalimbali, lakini China kwa upande mwingine imekuwa ikihimiza biashara kati yake na nchi za Afrika kwenye maeneo hayo.

Tukiangalia mifumo ya miamala ya malipo ya kimataifa, tunaweza kuona kuwa ni sarafu za magharibi tu ndio zinaweza kutumika kwenye biashara za kimataifa. Nchi za magharibi zinanufaika kwa kupokea tozo kwenye biashara ambazo hata hazihusiki, na wakati mwingine zinaweza hata kuyumbisha biashara hizo kwa kubadilisha thamani ya safari zao, au hata kuamua kuzuia fedha kwa visingizio mbalimbali kama vile vikwazo na sababu nyingine za kisiasa.

Licha ya ukweli kwamba kuna sababu mbalimbali za ndani ya bara la Afrika zinazofanya bara la Afrika liendelee kuwa nyuma kimaendeleo, kama bara la Afrika halitajikwamua kutoka kwenye mfumo wa kimataifa usio wa haki, itachukua muda mrefu sana kwa bara la Afrika kupata maendeleo.
 
Back
Top Bottom