MasterKey1
New Member
- Sep 2, 2022
- 1
- 1
AFRIKA USISAFIRI, TANZANIA USIHAME
Kwanza nilishtuka kwa mshangao wa bashasha baada ya kuona maneno ya Kiswahili katika ardhi ya Korea, “Afrika Safari” ndivyo yalivyosomeka huku yakipambwa na picha za wanyama wa aina mbalimbali kama vile Simba, Chui, Twiga, na Tembo. Furaha yangu ilianza kupotea na uso wangu kujawa na huzuni iliyoambatana na machungu dhidi ya viongozi wa Afrika wasio wazalendo kadri nilivyozidi kuingia kwenye eneo hilo la kivutio lililokua na wanyama wa aina mbalimbali wenye asili ya Afrika, badala ya kufurahia utalii huo, rafiki yangu kutoka Misri niliyembatana naye alinishangaa na kuhoji kwa nini furaha yangu ilitoweka ghafla.
Zikiwa zimebaki siku tatu kabla ya tarehe ya mwisho, nikasema mimi ngoja niombe, bosi wangu alinisihi niache kwa sababu ya tishio la janga la UVIKO 19 kwa wakati huo, huku akisema nifikirie zaidi kujenga familia yangu. Lakini dhamira yangu ilinihimiza kuendelea na mchakato huo wa ushindani, kwani niliamini Mungu Ataamua. Hakika, penye nia pana njia, nikawa miongoni mwa waafrika wachache waliobahatika kupata udhamini huo uliogharamia sio masomo pekee bali hadi nauli ya kwenda na kurudi.
Siku yangu ya safari, Agosti 30, 2020 ndipo niliamini changamoto yaweza kuwa ni sehemu ya safari yoyote ya mafanikio, ni baada ya kukutana na kikwazo katika uwanja wa ndege wa Mwalimu J.K. Nyerere. Kama mtumishi wa umma, nilipaswa niwe na kibali kutoka Ikulu ili kuruhusiwa kwenda nje ya nchi, ila kibali kilichelewa, na tarehe ya safari ikafika. Hadi nusu saa kabla ya safari nilikuwa sijaruhusiwa kupita kwenye lango la uhamiaji, nilimpigia waziri hakuweza kunisaidia, nilimshukuru sana Katibu Mkuu wa TAMISEMI wakati huo kwa kunipa ushirikiano ndani ya muda mfupi sana uliokua umebaki, huyu ni miongoni mwa viongozi ambao tunawahitaji kushughulikia changamoto za wananchi, hatuhitaji viongozi wanaoweka tabaka kati yao na watu wa chini yao, hatuhitaji viongozi wanaojali maslahi yao pasi kutanguliza maslahi ya taifa mbele, Afrika, hatuhitaji viongozi kama hawa wanaohamisha vivutio vya utalii na mbuga zetu kwa kuuza wanyama nje ya nchi. Basi hatimaye simu kutoka Ikulu ikawa sababu ya mimi kuruhusiwa kuingia kukaguliwa kwa ajili ya kuendelea na safari huku nikiwa nasubiriwa kama mtu aliyepotea na wahudumu wa ndege, nilimshukuru Mungu.
Nilipoingia Korea ndipo nikagundua kuwa kuna tofauti kubwa sana kati ya nchi ‘zinazoendelea’ na zile ‘zilizoendelea’. Miundombinu ni ya hadhi ya juu na bora kila mahali, elimu ni bora kwa ukweli na ubora huo unachagizwa na mazingira ya utoaji elimu, lakini pia hadhi ya mwalimu. Kwa uzoefu nilioupata kutoka darasani na uraiani, Korea ni nchi ambayo ilikua masikini kupindukia hadi kufikia miaka ya 1950, ikiwa imepishana kidogo tu na tarehe za uhuru wa nchi zetu nyingi za Afrika, Korea iliweza kupiga hatua za maendeleo kwa kasi sana baada ya kufanya mapinduzi ya Kielimu, kuipa elimu kipaombele, kutoa watu kwenda kusoma kwenye nchi zilioendelea za Ulaya na kisha kuja kuleta mabadiliko ndani ya nchi yao.
Leo hii ndani ya nchi yetu sina uhakika kama kuna mpango wowote wa kubainisha raia waliosoma nje ya nchi, kujua wamesoma nchi gani, wamesomea nini, na wanawezaje au wanawezeshwaje ili kile walichosomea kilete tija katika taifa. Lakini si elimu pekee iliyoiwezesha Korea kufika hapo, uongozi ni jambo jingine, na si uongozi tu bali uongozi wenye uadilifu. Marais wastaafu wawili walishafungwa jela kwa tuhuma za rushwa, ufisadi, na matumizi mabaya ya madaraka nchini Korea. Uwazi na Uwajibikaji ni msingi katika serikali ya Korea. Siku moja katika semina moja baada ya waziri wa Elimu wa Korea kuwasilisha mada yake, nikapata nafasi ya kumuuliza swali: “Tumeona Mapinduzi ya Kielimu yaliisaidia Korea kupiga hatua ya maendeleo kwa kasi sana, je, nini kifanyike katika nchi zinazoendelea hususani Afrika ili kuboresha elimu na kuleta mabadiliko chanya?”. Pamoja na urefu wa swali nililouliza, Daktari huyo wa Elimu alijibu kwa kifupi sana kabla ya kudadavua: “RUSHWA/UFISADI, bila shaka huyo ndio adui namba moja wa Afrika. Kabla ya kufikiria kuboresha elimu lazima kuhakikisha uongozi bora, unaweza wekeza fedha nyingi kwenye elimu lakini kama hakuna usimamizi madhubuti itakua ni bure, rushwa/ufisadi ni adui mkuu wa maendeleo ya Afrika.”
View attachment SNPT5440.jpg
Ndipo nikahusianisha na kile nilichokiona ndani ya “Afrika Safari”, wanyama hao wamefikaje nchini humo, kutoka nchi gani, ni nani aliyeuza, alikua na nia gani?. Shauku ya watu ni kushuhudia kwa macho, ndio maana wanalipa pesa kwa ajili ya kuweza kupata nafasi ya kuona. Pamoja na michezo mingine ya watoto iliyopo hapo, nilipofuatilia niliambiwa sehemu hiyo watu hufurika mara zote zaidi kwa ajili ya kuangalia wanyama, ni pesa nyingi mno zinazopatikana kwa watu kufika kuona wanyama. Hivyo nilipokasirika ni kwa sababu nilianza kuwaza ni pesa kiasi gani tumepoteza kama taifa/Afrika kwa kuhamisha wanyama hao iwe kwa njia halali au njia haramu, ni sehemu ngapi kama hizo zipo katika nchi nyingine zilizoendelea ambao pia walinunua/kuhamisha wanyama kutoka Afrika, ni watalii wangapi wanapotea baada ya shauku na kiu yao ya kushuhudia wanyama fulani kwa macho kukatikia ndani ya nchi zao?. Siku moja rafiki yangu mmoja aliyekua mwanafunzi katika shule moja Sekondari katika chuo nilichokua nasoma hapo Korea, akawa akiniuliza maswali mbalimbali kuhusu Tanzania, mojawapo ni kuwa akifika Tanzania ataweza kuona wanyama kama Simba, Chui, na Tembo kwa macho, ndipo nilipomuhakikishia hilo na kumuelezea zaidi kuhusu vivutio mbalimbali vilivyopo nchini mwetu. Lakini vipi akishapata kuwaona ndani ya nchi yake, atakua na shauku tena?.
Tunaweza ona kawaida lakini ni hatari kwa ustawi wa nchi yetu, o Afrika, yaani kuna viongozi wa hovyo sana ambao wangekua na uwezo wa kuhamisha Mlima Kilimanjaro, kuuza Mto Naili, kuliuza Ziwa Victoria, na hata kuihamisha Serengeti, wangefanya hivyo, ili mradi tu kujinufaisha nafsi zao, na matumbo yao bila kujali kesho yao na ndugu zao, inaumiza. Niliporudi nchini 2022 nilisikia habari iliyosema kuwa Serikali imeruhusu usafirishaji wa wanyama pori nje ya nchi, nilishtuka sana na kuumia mno ila wapi ningetoa maoni yangu, ni kabaki tu kulia na Mungu wangu nikijua athari zake kwa taifa letu, ila kesho yake nikasikia waziri mwenye dhamana kazuia tena hadi pale yatakapotoka maelekezo mengine, nilifarijika, japo ukweli halisi wanaujua wao huko kwenye sekta husika. Kwa maoni yangu na ningekua nina mamlaka, hakuna kuuza wala kusafirisha wanyama pori nje ya nchi. Simulizi yangu ni ndefu, ila kwa kikwazo cha idadi ya maneno, haya yametosha, ahsanteni sana.
Afrika usisafiri, Tanzania usihame
Ulipo ni kuzuri, waingie wakusome,
Serengeti usisafiri, Kilimanjaro usihame,
Royo Tua ni sahili, watalii wasikwame,
Tanzania ukisafiri, utawafanya wakuhame
Ngorongoro subiri, wafike wakuone,
Usijitie ngulumbili, kujipeleka wakuchune,
Mikumi mara mbili, nakusihi utulizane,
Mueleze na Naili, rafikie Viktorine,
Watulie wanawili, hawahitaji mashine,
Afrika usisafiri, Tanzania usihame
Ulipo ni kuzuri, waingie wakusome,
Serengeti usisafiri, Kilimanjaro usihame,
Royo Tua ni sahili, watalii wasikwame,
Tanzania ukisafiri, utawafanya wakuhame
Ngorongoro subiri, wafike wakuone,
Usijitie ngulumbili, kujipeleka wakuchune,
Mikumi mara mbili, nakusihi utulizane,
Mueleze na Naili, rafikie Viktorine,
Watulie wanawili, hawahitaji mashine,
Afrika usisafiri, Tanzania usihame
Attachments
Upvote
1