Hivi karibuni, rais wa Marekani Donald Trump alitangaza nyongeza ya ushuru kwa nchi kadhaa, zikiwemo nyingi kutoka bara la Afrika, na hivyo kuvuruga utaratibu wa biashara ya kimataifa. Wakati Marekani imetoa siku 90 za nyongeza kabla ya ushuru huo kuanza kutekelezwa katika nchi nyingi, wachambuzi wanaamini kuwa kipindi hicho ni cha muda tu, na wala si cha kudumu.
Kutokana na hilo, Mkataba wa Fursa na Ukuaji wa Afrika (AGOA), ambao ni makubaliano ya biashara yaliyoanzishwa mwaka 2000 na yanatarajiwa kukamilika mwezi Septemba mwaka huu, huenda ukashindwa kuendelea. Wachumi na wataalamu wa sera wanasema, nchi za Dunia ya Kusini zinapaswa kuimarisha kujitegemea na kuboresha ushirikiano wa Kusini na Kusini ili kukabiliana na kuongezeka kwa vitendo vya kujilinda na upande mmoja vya Marekani.
Mapema mwezi April, Marekani ilitangaza wimbi jipya la ushuru unaozilenga nchi nyingi, ambapo nchi kadhaa za Afrika zimeathirika sana na sera hiyo. Bidhaa kutoka Lesotho zimeongezewa ushuru wa hadi asilimia 50, Madagascar asilimia 47, Mauritius asilimia 40, na Botswana asilimia 37.
Celestin Monga, mchumi kutoka Cameroon ambaye pia aliwahi kuwa makamu wa rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, anasema, madhara yasiyo ya moja kwa moja ya kuvurugika kwa biashara, vita ya kibiashara duniani, na kufungwa kwa masoko ya Magharibi kunaweza kuwa na changamoto kubwa kwa nchi za Afrika, ambazo zinategemea sana uagizaji wa bidhaa kama chanzo cha mzingi cha kipato na biashara ya nje. Anasisitiza kuwa, kushuka kwa uchumi wa dunia kunamaanisha kupungua kwa mahitaji ya mafuta na bidhaa nyingine ghafi, ambavyo vinasababisha kushuka kwa bei ya mafuta ghafi na bidhaa ghafi zinazotoka barani Afrika.
Monga amependekeza kwa nchi za Afrika kuanzisha benki za kitaifa za maendeleo na kukusanya ufadhili kutoka kwa umma, sekta binafsi na taasisi za fedha ili kuanzisha maeneo ya viwanda yanayojikita katika uzalishaji na utengenezaji wa maeneo husika. Anasema hatua hiyo itatumika kama masoko yanayoibuka yenye shauku ya bidhaa zilizotengenezwa Afrika ambazo zinakidhi vigezo vya kimataifa.
Kwa upande wake, mhadhiri wa zamani katika Chuo Kikuu cha Yaounde, Profesa Nkolo Foe, anasisitiza ushirikiano wa dharura wa Kusini na Kusini. Anasema hatua zinazochukuliwa na rais wa Marekani Donald Trump zinaathiti moja kwa moja Dunia ya Kusini na pia zinavuruga utaratibu wa kimataifa na kuishi pamoja kwa masikilizano.
Naye Profesa Humphrey Moshi, Mkurugenzi wa Taasisi ya Maendeleo ya Jamii na Uchumi kati ya Afrika na China katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam nchini Tanzania, ametoa wito wa mtazamo wa kimkakati na kivitendo katika hali inayobadilika ya kimataifa. Amesema badala ya kujaribu kuendana na hali hiyo, nchi za Afrika zinapaswa kuwekeza katika unymbufu, maingiliano ya kikanda, na uhusiano wenye manufaa. Anasema Marekani inaweza kujaribu kuleta mvurugano, lakini ni ushirikiano pekee, na wala sio malumbano, ambao unaunga mkono maendeleo.
Kwa Dunia ya Kusini, hususan Afrika, hii ni fursa kubwa ya kutafakari tena kuhusu uhusiano, kuimarisha uhusiano wa kikanda, na kushirikiana kwa usawa na nchi zinazoibuka kiuchumi, kama vile China.