AFRODAD, SADCOPAC zaungana kuimarisha usimamizi wa Bunge kwa Madeni ya Umma

AFRODAD, SADCOPAC zaungana kuimarisha usimamizi wa Bunge kwa Madeni ya Umma

Elias Msuya

Platinum Member
Joined
Dec 23, 2011
Posts
267
Reaction score
1,014
Afrodad.png


MANZINI, Eswatini. Shirika la African Forum and Network on Debt and Development (AFRODAD) na Jumuiya ya Mashirika ya Kamati za Hesabu za Umma ya Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADCOPAC) zimeingia rasmi katika ushirikiano unaolenga kuimarisha usimamizi wa Bunge, kuhamasisha ukopaji wa umma unaowajibika na kuboresha usimamizi wa fedha za umma katika ukanda wa Kusini mwa Afrika.

Ushirikiano huo unalenga kuzipatia Bunge za Afrika maarifa, uwezo na zana zitakazowasaidia kuchunguza na kusimamia ukopaji wa umma, kuongeza uwajibikaji na kukuza usimamizi endelevu wa madeni na maendeleo.

Makubaliano hayo yamefikiwa wakati AFRODAD ikiadhimisha miaka 30 ya utetezi wake wa haki za madeni, na yanalenga kugeuza kazi yake ya kutetea masuala ya madeni kuwa hatua madhubuti zaidi za kitaasisi, sambamba na kusaidia utekelezaji wa Msimamo wa Pamoja wa Afrika kuhusu Madeni (Africa’s Common Position on Debt).

Mkurugenzi Mtendaji wa AFRODAD, Janet Zhou, amesema ushirikiano huo ni hatua muhimu katika kampeni ya shirika hilo ya miongo mitatu ya kutetea haki za madeni na uwajibikaji.

“Kwa kuimarisha usimamizi wa Bunge, tunabadilisha misingi iliyoandikwa kwenye nyaraka kuwa usimamizi imara katika utekelezaji,” amesema Zhou, akiongeza kuwa ushirikiano huo pia utasaidia juhudi za Afrika za kujenga mfumo wa kimataifa wa madeni ulio wa haki zaidi.

Chini ya ushirikiano huo, AFRODAD na SADCOPAC zitashirikiana katika utetezi, kujenga uwezo na kubadilishana maarifa kuhusu usimamizi wa fedha za umma.

Moja ya maeneo muhimu ya ushirikiano huo itakuwa kuimarisha sheria, ikiwamo kuhamasisha nchi wanachama kurekebisha na kuendana na Sheria Kielelezo ya SADC kuhusu Usimamizi wa Fedha za Umma (SADC Model Law on Public Financial Management) na Sheria Kielelezo ya Ukaguzi wa Umma (Model Public Audit Act).

Mashirika hayo pia yatahamasisha ukopaji unaowajibika kupitia matumizi ya African Borrowing Charter, kwa lengo la kuimarisha usimamizi wa ukopaji wa umma, dhamana zinazotolewa na Serikali na matumizi ya fedha za umma.

Eneo jingine la ushirikiano litakuwa kujenga uwezo wa Kamati za Hesabu za Umma na Bunge katika kuchunguza kwa ufanisi zaidi usimamizi wa madeni na maamuzi yanayohusu fedha za umma.

Ushirikiano huo pia utalenga kuimarisha utetezi wa pamoja kuhusu uwajibikaji katika madeni ya umma na kuchangia utekelezaji wa Msimamo wa Pamoja wa Afrika kuhusu Madeni.

Kwa mujibu wa mashirika hayo, usimamizi madhubuti wa Bunge ni muhimu katika kuhakikisha uwazi katika maamuzi ya ukopaji na kuzifanya Serikali kuwajibika kuhusu namna rasilimali za umma zinavyokopwa na kutumika.

Kwa kuunganisha utaalamu na mitandao yao ya kikanda, AFRODAD na SADCOPAC zinatarajia ushirikiano huo kuimarisha taasisi za kutunga sheria na kukuza usimamizi wa fedha za umma wenye uwajibikaji zaidi katika ukanda wa Kusini mwa Afrika.

AFRODAD ni shirika la kiraia la Afrika linalojikita katika kutetea haki za madeni, ukopaji unaowajibika, maendeleo endelevu na usimamizi wa fedha za umma wenye uwajibikaji.

SADCOPAC ni jukwaa la kikanda linalozileta pamoja Kamati za Hesabu za Umma kwa lengo la kuimarisha usimamizi wa Bunge, uwajibikaji na usimamizi wa fedha za umma.
 
Back
Top Bottom