SoC02 Afya kidijitali, mkombozi utoaji wa huduma za afya nchini

Stories of Change - 2022 Competition

Hadija Mlacha

New Member
Joined
Sep 5, 2022
Posts
1
Reaction score
6

Chanzo picha:TechCrunch

Habari yako, mimi ni Hadija Mlacha, Karibu katika makala haya yanayoangazia umuhimu wa sayansi na teknolojia katika afya ya binadamu, yapo mengi ya kujifunza.

Maendeleo ya sayansi na teknolojia yamekuwa na mchango mkubwa kwa binadamu katika nyanja zote, hapa namaanisha kiuchumi, kijamii, kiutamaduni na kisiasa. Katika zama hizi za kidijitali makampuni, taasisi na mashirika ya umma na yale ya binafsi yamekuwa yakitoa na kuendesha huduma zao kwa njia ya kidijitali hususani katika kukidhi mahitaji ya wateja wao hasa ambao ni watumiaji wazuri wa vifaa vya kidijitali kama vile simu janja, kishikwambi na kompyuta.

Kwa wengi wetu sio jambo geni kupitia changamoto lukuki hasa wakati tunahitaji huduma za vipimo na matibabu katika vituo vya kutolea huduma za afya, hali inayopelekea hali zetu za kiafya kuzorota. Miongoni mwa changamoto hizo zinavumilika lakini zipo zile ambazo hazivumiliki wala kuepukika, hata hivyo bado tumekuwa tukizielekeza fikra zetu katika kupokea matibabu ya maradhi tulionayo kwa vile ni huduma ya msingi.

Changamoto hizi zimekuwa zikijitokeza sana katika vituo vya afya vya umma kwani vituo hivi vinahudhuriwa na idadi kubwa ya wagonjwa iikilinganishwa na idadi ya watoa huduma waliopo katika vituo hivyo jambo ambalo linapelekea kuzorota kwa utoaji wa huduma kutokana na msongamano mkubwa wa wagonjwa wanaohitaji huduma za afya.


Chanzo Picha: Istock

Pia vituo hivi vya afya vinakumbwa na changamoto ya kasumba kwani kuna baadhi hupewa huduma stahiki kwa wakati kwa vile tu wanafahamiana na mtoa huduma wa zamu ama anakipato cha juu kuliko wengine wanaohitaji huduma inayofanana.

Mbali na changamoto hizo, pia hospitali za umma zimekuwa zikilalamikiwa kila kukicha kuwa hazina vifaa toshelevu kwa ajili ya kutoa matibabu kwa wagonjwa hali ambayo ina hatarisha maisha ya wagonjwa hususani wajawazito.

Mara nyingine hospitali hizi zinakuwa mbali kiasi kwamba baadhi ya wanajamii wanashindwa kuzifikia kwa wakati kutokana na ufinyu wa miundombinu.

Lakini pia wagonjwa wamekuwa wakitoa malalamiko yao kuwa vituo ya umma vya utoaji huduma za afya zimekuwa zikikumbwa na changamoto ya vitendea kazi ikiwemo dawa muhimu na badala yake wamekuwa wakishauriwa na watoa huduma kujipatia huduma ya dawa ya wamiliki binafsi maduka ya swala ambalo limekuwa endelevu kwa kipindi kirefu. Kutokana na changamoto hizo wagonjwa wakaamua kujitafutia sululisho la changamoto hizo ili kupata huduma sahihi kuendana na hali ya afya zao na kuepusha usumbufu.

Kwa wakati huo ndipo ongezeko la vituo binafsi vya kutoa huduma za afya vikaongezeka kwa kasi kama namna ya kuteka soko jipya la utoaji huduma na kukuza biashara. Hapo ndipo kundi kubwa la wagonjwa waliohamia katika vituo binafsi vya afya na kwa kiasi fulani kero za wagonjwa hasa ile ya upatikanaji wa dawa ikapungua.

Ongezeko la wagonjwa kupata huduma za afya katika vituo binafsi lilizihirika hasa pale mifumo ya utoaji wa huduma wa afya kupitia mfumo wa bima za afya ulipoanza kutumiwa katika vituo vya afya vya wamiliki binafsi ambavyo hapo awali vilikuwa vikitoza gharama kubwa za matibabu ili kupata huduma.

Hakika huduma zilizokuwa zikitolewa na vituo hivi binafsi ziliwapendeza na kuwavutia wengi kwa vile huduma zilikuwa zikitolewa kwa ubora kama ilvyotarajiwa, hakukuwa na changamoto ya foleni wala changamoto ya dawa, wagonjwa wakasahau haza walizokuwa wakikutana nazo katika vituo vya afya vya umma, lakini kadri siku zinavyosogea tamu inageuka kuwa chungu katika vituo hivi binafsi vya afya kwani idadi ya wagonjwa imekuwa ikiongezeka maradufu kwani zimeonekana kuwa ndio kimbilio lenye kuleta hafueni kwa wagonjwa.

Kitendo cha ongezeko la wagonjwa katika hospitali binafsi kimepelekea kurejea kwa changamoto za awali kama ilivyokuwa kwenye vituo vya afya vya umma, hali ambayo inawaumiza wagonjwa kwani hawana jibu sahihi kutokana na kutofahamu ni wapi wataipata ahueni ya afya zao.

Tatizo la utoaji sahihi wa huduma za afya bado linawaumiza vichwa watumiaji na watoaji wa huduma hii. Lakini Siku ya leo nipo hapa kukupatia ufumbuzi juu wa fumbo ambalo siku zote limekuwa limekuwa likitafutiwa ufumbuzi wa kina.

Ufumbuzi wa fumbo hilo ni matumizi yakinifu ya sayansi na teknolojia katika kuzifikia huduma zote zenye umuhimu kwa biaandamu.. Kama tunavyojua kwa sasa tumetawaliwa na ulimwengu wa kidigitali ambapo vifaa vingi vinavyotumika kwa sasa vinatumia teknolojia ya hali ya juu iliyoifanya dunia kuwa kijiji katika ulimwengu wa biashara na mawasiliano.

Katika ulimwengu wa kitabibu matumizi ya sayansi na teknolojia yamebisha hodi na kushika atamu lengo kuu ni kuboresha afya ya mwanadaamu na kutatua kero zilizokuwa zikivuta shati utoaji wa huduma za afya.

Kama namna ya kutatua kero hiyo wanasayansi wamegundua programu maalum iitwayo Ada app. Programu hii imetengenezwa mahususi kwa ajili ya kutoa huduma za awali za afya kupitia vifaa vya kiteknolojia kama simu janja, kishikwambi na hata kompyuta.

Iwapo programu hii itatumika kwa usahihi itakuwa ni suluhisho la kipekee katika kuboresha utoaji wa huduma za afya kwani inamruhusu mgonjwa kuweka maulizo ya dalili za ugonjwa alionao au vile anavyojisikia na mwisho inauwezo wa kutoa makisio ya ugonjwa husika kulingana na dalili zilizotolewa na mgonjwa na kilicho kizuri zaidi program hii zitaweza kupendekeza dawa ambazo zipo kwa ajili ya kutibu ugonjwa huo.

Huduma hii ni moja wapo wa ukombozi wa sekta ya afya kwa vile ni rahisi katika matumizi na utoaji wa huduma za awali kwa mgonjwa kwani haina foleni lakini pia haina gharama kubwa ikilinganishwa na mchakato mzima wa upatikanaji wa huduma katika kituo cha afya.

Hivyo basi kuwepo huduma hizi za afya kupitia kwenye programu kama hii ni maendeleo muhimu katika sekta ya afya na inaweza kuchukuliwa kama mfano mzuri wa kuigwa kwa wanasayansi na wataalam wa teknolojia nchini, kwani zinaweza kuundwa programu nyingine kama hizi zenye uwezo wa kumruhusu daktari wa kidijitali kumtibu mgonjwa kwa ukaribu zaidi hususani kwa wagonjwa wanaopatiwa huduma za afya wakiwa majumbani, wagonjwa waliopo karantini mfano wagonjwa wa ebola au uviko-19.

Katika hali ya kumhudumia mgonjwa program hizi zinauwezo mkubwa wa kuhifadhi taarifa za mgonjwa hivyo inakuwa rahisi kufuatilia mwenendo wa mgonjwa na kupata taarifa zanmgonjwa wakati wowote ule. Sanjari na haayo program hizi ni za haraka lakini ni salama katika kutunza taarifa binafsi za mgonjwa kwani hazimruhusu mtu mwingine kupata taarifa za mgonjwa bila idhini ya mgonjwa mwenyewe.

Programu hizi husaidia pia wanasayansi na watafiti kupata dalili mpya za ugonjwa na hata katika kutafuta suluhisho jipya katika kutibu dalili mpya za ungonjwa kwani ugonjwa mmoja unaweza kuwa na dalili tofauti kutokana na utofauti wa hali ya hewa na mazingira. Chunguzi zilizofanywa, kukusanywa na kuhifadhiwa na programu hizi kuhusu mgonjwa zinasaidia kutoa dozi kamili ya dawa juu ya ugonjwa husika.

Wataalam wetu wa afya wakishirikiana na wanateknolojia wanaweza kuweka nguvu kwenye teknolojia hizi na zaidi kuboreshwa kwa kurahisisha upatakanaji wa huduma ikionyesha maduka yote ya dawa muhimu za binadamu yalioko sehemu ya mji au kijiji, kuorodhesha dawa zote zilizomo kwenye maduka hayo pamoja na kutoa nafasi ya mawasiliano kati ya wagonjwa na watoa huduma wa maduka ya dawa, zahanati na vituo vya afya vilivyo karibu.

Lakini pia teknolojia hii ikiboreshwa inaweza kurahisisha ufikiwaji wa dawa kwa kusafirisha mahitaji ya dawa muhimu kwa sehemu zinapohitajika.

Kwa kufanya hivyo itapelekea huduma hii kuwa rahisi, na hatimaye itatatua kero ya foleni na kuweza kuwasaidia wagonjwa wasio na ulazima wa kufika katika vituo vya huduma.


Chanzo picha: Bio World Medtech

Matumizi ya teknolojia katika sekta ya afya ni maendeleo yanayopigiwa chapuo kila uchao na kwa kiasi kikubwa yamechangia kuboresha huduma ya afya ulimwenguni kote hivyo ugunduzi na uboreshaji wa teknolojia utasaidia kutoa huduma kwa usalama na itapunguza adha na usumbufu usio wa lazima.
Matumizi ya teknolojia katika ulimwengu huu waa kidijitali hayaepukiki na ndio sululisho pekee la changamoto zinazowakumba.

Wataalam wa afya na teknolojia nchini wananafasi ya kipekee ya kutumia nyenzo hizo muhimu za maendeleo ya teknolojia ili kuikomboa sekta ya afya.
 
Upvote 7
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…