SoC02 Afya ya akili kwa Vijana

SoC02 Afya ya akili kwa Vijana

Stories of Change - 2022 Competition

AnonymousVee

New Member
Joined
Jul 27, 2022
Posts
1
Reaction score
0
Habari ndugu zangu mliomo humu. Ningependa leo tutafakari kwa pamoja kuhusu hili suala la "Afya ya akili kwa vijana".

Tuanze na kujiuliza kuwa; Kijana ni nani? Na kwanini afya yake ya akili iathirike zaidi kuliko kundi lingine? Si kwamba watu wazima afya zao za akili haziathiriki, la hasha, ila sote tukubali kwamba mtu mzima ni mtu ambaye amekwisha jifunza vya kutosha kuhusu maisha hivyo akili yake ipo "stable" zaidi na anaweza kusimamia hisia, fikra na matendo yake.

Kwanza kabisa, katika ufafanuzi wangu Ningependa kusema kuwa ili kijana kufafanuliwa kama kijana ni mtu ambaye anabadilika kutoka utotoni hadi utu uzima. Neno "ujana" hauangazii umri ambao mtu anaweza kuitwa kijana. Ni vigumu kuweka umri kwenye fasili ya ujana kwa sababu kuna mpito hadi kwenye utu uzima na hutofautiana kadiri wanavyofikia watu wazima. Kuna baadhi ya sehemu wana mtazamo kuwa ujana huanzia miaka 15 hadi 24 na wengine husema ujana huishia miaka 35 na wengine wanapitiliza hadi 40.

Ujana ni kipindi muhimu cha kukuza tabia za kijamii na kihemko muhimu kwa ustawi wa kiakili. Mambo yanayoweza kuchangia mfadhaiko wakati wa ujana ni pamoja na kukabili hali ngumu kimaisha yaani umaskini, shinikizo la kufuatana na marafiki (peer pressure) na kujikuta akijaribu kile akili yake inachomtuma pia ushawishi wa vyombo vya habari na kanuni za kijinsia (transgender, LGBTQ na kadhalika) zinaweza kuzidisha tofauti kati ya maisha halisi ya vijana na mitazamo au matarajio yao ya siku zijazo. Unyanyasaji wa kijinsia hasa unyanyasaji wa kingono na uonevu na mwisho kabisa mahusiano hafifu kati ya vijana hawa na wazazi au walezi.

Kimsingi hivi sasa tumekuwa tukiona vijana wengi mitandaoni hususani Instagram wakionesha tabia ambazo si sawa au hazikubaliki katika jamii hususani jamii za Kiafrika na moja kwa moja tumekimbilia kuwahukumu na kuwanyanyapaa vijana hawa bila ya kutaka kuelewa shida iko wapi au ilianzia wapi mpaka wakafikia katika hali hii. Wazazi na walezi tunapenda kutumia ile msemo wa "mimi namjua mwanangu bwana!!" ilihali hatuwajui kabisa kwani kuna mambo mengi wanapitia ila hawatuhusishi kwani sisi ni wepesi wa kuhukumu na si kutoa msaada. Tumeshindwa kujenga urafiki na watoto wetu ili kuwasahihisha kiurahisi pindi wanapokosea wakifikia hali ya ujana.

Nakupa mkasa mmoja ambao unaweza kuwa ni wa ukweli au si wa ukweli. (Tafadhali msihusishe majina yeyote hapa).

Kuna binti mmoja mwanafunzi wa Sekondari alitokea katika familia ya kiustaarabu au "geti Kali" kama tunavyosema siku hizi. Siku moja binti yule alitoroka na kwenda "klabu". Hatujui alikuwa na matatizo gani kwao ila ni dhahiri umri wake wa ujana ulimuendesha na hakuwa na mshauri kwani wazazi wetu wengi ni mahakimu na si washauri hivyo hatuwezi mlaumu.

Basi huko alikoenda alikutana na kijana mwenzie ambaye kidogo alimpita kiumri. Walijenga urafiki na Binti huyu akahamia kwa yule kijana. Familia ilifanya juhudi za kumtafuta na kumrudisha huyu binti nyumbani ila juhudi ziligonga mwamba na binti huyu shule kwake ikawa ndio basi. Baada ya miezi kadhaa Binti huyu akashika ujauzito na baadae kujifungua mtoto wa kike.

Urafiki kati ya Binti huyu na yule kijana haukudumu kwani ulitawala usaliti, vipigo na unyanyasaji tele! Hatimaye waliachana na binti akabaki mtaani na mtoto wake. Familia ilimsamehe na akarudi kwao. Baada ya miaka kadhaa huyu binti akapata mume wa kumuoa ila ndoa hii iliishia jela kwani bwana huyo alifungwa jela na binti naye alihusishwa kama msaidizi wake ila binti alisaidiwa akatoka. Katika hii shida tuweke akilini kwamba mtoto wa huyu binti alikuwa karibu anaingia kwenye umri wa ujana yaani kati ya miaka 12-14 hivyo pata picha maisha yake yalivyokuwa shuleni na nyumbani au hata njiani Kwa wale waliomfahamu mama yake.

Maisha yalisonga na shida zikapita zikaja zingine. Mtoto huyu hakubarikiwa kiwango kikubwa cha elimu na unajua namna jamii yetu ilivyoshikamana na elimu ya makaratasi. Mtoto huyu alipitia fedheha na kejeli ambazo kwa miaka yake (17-19) ilikuwa ni "too much" ila yeye na mama yake waliyaweka kwenye mfuko wakatumia msemo wa wahenga "Yaliyopita si ndwele, tugange yajayo". Mpaka leo hii mtoto huyu anaendelea kusakamwa na kunyooshewa vidole kwa tabia zake zisizo za kawaida mitandaoni.

Kujihusisha na mahusiano ya kimapenzi katika umri mdogo, kushindwa kuendelea na elimu na kutokujua umuhimu wake na mengine mengi. Itoshe kusema kwamba jamii imemuangusha mtoto huyu. Wakati alipopitia mambo mazito na kukosa malezi bora ya baba na mama waliomzunguka mtaani hawakumsaidia na sisi mahakimu wa mitandao tunaohukumu na si kufundisha pia tulifeli ila hatuyaangalii hayo, tunabaki kumsema na kumuita majina mengi mabaya mabaya.

Fikira zetu zielekee katika jinsi ya kuwa karibu na vijana wetu na namna ya kuwasaidia vijana wengine walioathirika afya ya akili.

Nisimalize maneno yote kwani najua mna la kuchangia
 
Upvote 4
Back
Top Bottom