Afya za wanafunzi wengi Manispaa ya Shinyanga ipo hatarini, upungufu wa vyoo unavyowasukuma kujisaidia vichakani

Afya za wanafunzi wengi Manispaa ya Shinyanga ipo hatarini, upungufu wa vyoo unavyowasukuma kujisaidia vichakani

UTPC

Journalists' Union
Joined
Apr 17, 2026
Posts
51
Reaction score
38
AFYA za wanafunzi wa shule za msingi na sekondari katika Manispaa ya Shinyanga zipo hatarini kutokana na tabia ya kujisaidia hovyo, hali inayochangiwa na upungufu mkubwa wa matundu ya vyoo pamoja na ukosefu wa vyumba maalumu vya kujistiri wakati wa hedhi kwa wanafunzi wa kike.

Uchunguzi uliofanywa na Nipashe kwa kipindi cha miezi mitatu, pamoja na kutembelea shule mbalimbali katika Manispaa ya Shinyanga za Msingi na Sekondari, umebaini kuwapo na upungufu mkubwa wa matundu ya vyoo, na vyumba maalumu vya kujistiri wakati wa hedhi, hali inayohatarisha afya za wanafunzi na walimu.

Mwongozo wa kitaifa wa maji, usafi wa mazingira na afya shuleni (SWASH) wa mwaka 2009, unaelekeza shule kuwa na miundombinu ya kutosha ya maji, vyoo na usafi wa mazingira, ili kulinda afya za wanafunzi na kuboresha mazingira ya kujifunzia.

Hata hivyo, ni zaidi ya miaka 15 tangu mwongozo huo uanze kutumika, lakini shule nyingi zilizotembelewa na mwandishi wa makala hii, zimekutwa zikiwa na upungufu mkubwa wa matundu ya vyoo na vyumba maalumu vya kujistiri wakati wa hedhi.

Shule ya Msingi Ng'ihando iliyopo Kata ya Old Shinyanga, ni miongoni mwa shule zilizobainika kuwa na changamoto hiyo. shule hiyo ina wanafunzi 1,114, wakiwamo wasichana 588 na wavulana 526, lakini ina matundu 21 tu ya vyoo, wakati mahitaji halisi ni matundu 45. hivyo kuna upungufu wa matundu 24, huku ikiwa haina kabisa chumba maalumu cha kujistiri wakati wa hedhi.

Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule hiyo Shabani Mwitenga, anasema kutokana na upungufu wa matundu ya vyoo, wanafunzi hasa wa madarasa ya kwanza hadi la tatu, hulazimika kujisaidia vichakani na wengine nyuma ya majengo ya vyoo.

Anasema, wakati wa mapumziko huwa kuna foleni kubwa ya wanafunzi wanaosubiri kutumia vyoo, hivyo baadhi yao wakizidiwa na haja hukimbilia vichakani kujisaidia.

"Shule yetu ipo jirani na vichaka vingi. kutokana na upungufu wa matundu ya vyoo, baadhi ya wanafunzi, hasa wa madarasa ya chini, hujisaidia huko," anasema Mwitenga.

Anasimulia kuwa, kipindi cha masika wanafunzi wengi hupata magonjwa ya tumbo, huku wengine wakilazimika kuomba ruhusa ya kurudi nyumbani.

Mwalimu wa Afya na Mazingira wa shule hiyo Peter Msato, anasema wamekuwa wakitoa elimu kwa wanafunzi kuhusu matumizi sahihi ya vyoo, lakini kutokana na upungufu wa miundombinu hiyo, bado baadhi yao hulazimika kujisaidia vichakani na kuchafua mazingira.

"Idadi ya wanafunzi tulionao ni kubwa, lakini matundu ya vyoo ni machache. ndiyo maana tunalazimika kupambana kuhakikisha mazingira yanakuwa safi wakati wote. tukilegeza kidogo tu, tunaweza kukumbwa na magonjwa ya mlipuko," anasema Msato.

Mwalimu wa Malezi wa shule hiyo Suzana Mabula, anasema wanafunzi wa kike wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya kujistiri wakati wa hedhi, kutokana na ukosefu wa chumba maalumu, hali inayowalazimu kuwapa ruhusa ya kurudi nyumbani.

Anasema, baadhi ya wanafunzi wanapoingia katika siku zao hukumbwa na maumivu makali ya tumbo na kutapika, hivyo kutokana na kutokuwapo kwa sehemu salama ya kujistiri hulazimika kuwaruhusu kwenda nyumbani kupumzika.

"Hapa shuleni hapo awali tulikuwa na chumba maalumu cha kujistiri wakati wa hedhi, lakini kiliharibika tangu mwaka 2018 na hakijatumika tena. tulikifanyia tathmini na kubaini kuwa kinahitaji shilingi 600,000 kwa ajili ya ukarabati ili kianze kutumika tena," anasema Mabula.

Naye mwanafunzi wa darasa la saba katika shule hiyo Haidaly Samweli, anasema kutokana na foleni kubwa ya vyoo wakati wa mapumziko, baadhi ya wanafunzi hulazimika kujisaidia vichakani au nyuma ya majengo ya vyoo.

Anasema, hali hiyo imekuwa ikisababisha baadhi yao kuugua magonjwa ya tumbo na kuomba ruhusa ya kurudi nyumbani.

"Tunaomba tujengewe vyoo. afya zetu zipo hatarini, hasa kipindi cha mvua ambapo wengi wetu huumwa na tumbo na kuhara," anasema Samweli.

Mwanafunzi mwingine Lucy Gabriel, anasema wamekuwa wakisumbuliwa na maambukizi ya njia ya mkojo (UTI), maumivu ya tumbo pamoja na miwasho sehemu za siri, kutokana na baadhi ya wanafunzi kujisaidia maeneo yasiyo rasmi baada ya kushindwa kuvumilia foleni za vyooni.
CHUMBA CHA HEDHI NG'WIHANDO.JPG

Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi Ng’wihando, Shabani Mwitenga akiwa jirani na moja ya vyoo vilivyochakaa, ambacho hakitumiwi tena na wanafunzi.
PICHA: MARCO MADUHU

​
Anasema, wanapokuwa katika siku zao za hedhi hupata wakati mgumu kujistiri kutokana na kutokuwapo kwa chumba maalumu, hali inayowalazimu kuomba ruhusa na kurudi nyumbani kujisafisha.

"Ukianza hedhi ghafla ukiwa shuleni na hakuna sehemu ya kujistiri wala maji ya kutosha, unalazimika kuomba ruhusa na kurudi nyumbani. Wengine huamua kutokuja kabisa shuleni," anasema Lucy.

Changamoto kama hiyo pia imejitokeza katika shule ya msingi Bugimbagu yenye wanafunzi 395, wakiwamo wavulana 107 na wasichana 288. shule hiyo ina matundu sita tu ya vyoo, wakati mahitaji ni matundu 11, hivyo kuna upungufu wa matundu matano, huku ikiwa pia haina chumba maalumu cha kujistiri wakati wa hedhi.

Mwalimu wa Malezi, Afya na Mazingira wa shule hiyo, Cletisia Manda, akizungumza kwa niaba ya Mwalimu Mkuu msaidizi, anasema wavulana wana matundu matatu na wasichana matatu, hali inayosababisha baadhi ya wanafunzi kujisaidia vichakani kutokana na uhaba wa vyoo.

Anasema, shule hiyo imezungukwa na vichaka, hivyo baadhi ya wanafunzi huona ni rahisi kwenda kujisaidia huko kuliko kusubiri foleni ndefu ya vyooni wakati wa mapumziko.

"Baadhi ya jamii ya Wasukuma katika maeneo haya hazina utamaduni wa kutumia vyoo ipasavyo. tabia hiyo imeigwa na watoto wao, ndiyo maana kwao kujisaidia vichakani si jambo la ajabu. wakibanwa na haja utaona mwanafunzi ameelekea moja kwa moja vichakani," anasema Manda.

Anaongeza kuwa changamoto ya kujistiri wakati wa hedhi bado ni kubwa katika shule hiyo. anasema mwanafunzi anapoanza hedhi akiwa shuleni, walimu hulazimika kumpatia huduma ya awali katika nyumba ya mwalimu, kisha kumruhusu kurejea nyumbani kwa ajili ya kujisitiri na kujisafisha.

Katika shule ya sekondari Mwawaza, Mkuu wa Shule Vincent Kanyogoto, anasema shule hiyo ina wanafunzi 245, wakiwamo wasichana 165 na wavulana 80. na wana matundu manane ya vyoo pekee, manne kwa wasichana na manne kwa wavulana, huku ikiwa haina kabisa chumba maalumu cha kujistiri wakati wa hedhi.

Mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule hiyo Devota Emmanuel, anasema uchache wa matundu ya vyoo umekuwa ukiwasababishia usumbufu mkubwa kutokana na vyoo vya wavulana na wasichana kujengwa katika jengo moja na kugeuziana migongo.

Anasema, hali hiyo si salama kiafya kwa wanafunzi wa kike, kwani wakati mwingine wavulana huingia kwenye vyoo vya wasichana na kukojoa nje ya matundu ya vyoo, jambo linalosababisha uchafu unaochangia maambukizi ya magonjwa sehemu za siri.

"Sisi watoto wa kike tunapata changamoto kubwa shule inapokuwa haina matundu ya kutosha ya vyoo. wakati mwingine wavulana huingia kwenye vyoo vyetu na kukojoa pembeni ya matundu, jambo linalotusababishia miwasho sehemu za siri, UTI na fangasi," anasema Devota.

Anaongeza kuwa, pia wanafunzi wa kike hushindwa hata kujistiri ipasavyo wakati wa hedhi, kutokana na milango mibovu ya vyoo, wakihofia kufumaniwa na wavulana, sababu jambo hilo linahitaji faragha.


Mwalimu wa Malezi (Matroni) wa shule hiyo Amina Ngaroka, anasema kutokana na shule kutokuwa na chumba maalumu cha kujistiri wakati wa hedhi, pamoja na changamoto ya wavulana kuingia katika vyoo vya wasichana, hulazimika kuwaruhusu wanafunzi wa kike kutumia choo cha walimu kwa ajili ya kujistiri.

Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Oldshinyanga Mathayo Isaya, anasema kipindi cha masika wamekuwa wakipokea wanafunzi wawili hadi watatu kwa kila wiki wakisumbuliwa na magonjwa ya matumbo na kuharisha.

“Kipindi cha masika magonjwa mengi ya mlipuko ndiyo hua yanatokea, ambayo husababishwa na uchafuzi wa mazingira, ambapo mvua zinaponyesha maji hupeleka uchafu au kinyesi kwenye vyanzo vya maji na wanafunzi wakiyatumia katika maeneo yao ya shule ndipo huanza kuugua matumbo,” amesema Dk. Mathayo.

Daktari wa Magonjwa ya dharura na mlipuko katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga Kambi Buteta, anasema upungufu wa vyoo shuleni husababisha wanafunzi kujisaidia hovyo vichakani, au karibu na vyanzo vya maji na kusababisha vijidudu vya magonjwa ya tumbo.

Anasema, vijidudu hivyo huenezwa kwa kinyesi kuchanganyika na maji ya kunywa, kupitia mvua, mafuriko na visima visivyosalama, hasa vile ambavyo havina mifuniko.

Anaongeza, wanafunzi kujisaidia vichakani, pia inz huchukua kinyesi na kutua kwenye chakula, na kusababisha maambukizi.

Anataja madhara ambayo husababishwa na kujisaidia vichakani, kuumwa magonjwa ya tumbo, kuharisha, kipindupindu na homa ya inni.

“Takwimu za kuanzia Marchi hadi May 31. 2026 watoto waliofika kutibiwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga wakikabiliwa na magonjwa yanayotokana na uchafuzi wa mazingira ni 878, hawa ni wengi sana ndani ya miezi mitatu, hii siyo dalili nzuri, kuna hatua zinapaswa kuchukuliwa,” amesema Dk. Buteta.

Halima Hamisi ni Mratibu wa Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto Mkoa wa Shinyanga, anaelezea madhara ambayo wanaweza kupata wanafunzi kutokana na ukosefu wa vyumba maalumu vya kujistiri na hedhi shuleni, kupatwa fangasi ukeni, miwasho na kutokuwa huru darasani.

Anataja mazingira ya hedhi salama shuleni, kuwa ni upatikanaji wa taulo za kike, maji safi, na sehemu sahihi ya mwanafunzi kujistiri na hedhi, ili kulinda afya, utu na hadhi ya mtoto wa kike.

"Wanafunzi wa kike wanahitaji mazingira salama yanayowawezesha kujistiri kwa faragha wakati wa hedhi, kukosekana kwa vyumba maalumu, maji safi na vifaa salama shuleni, kunaweza kuongeza hatari ya maambukizi pamoja na kuwafanya baadhi yao kushindwa kuhudhuria masomo," anasema Halima.

Afisa Takwimu wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga Bopali Mwakiluma, anasema manispaa hiyo ina jumla ya wanafunzi 43,078 wa shule za msingi, wakiwamo wavulana 21,233 na wasichana 21,845.

Anasema, kutokana na idadi hiyo ya wanafunzi, mahitaji halisi ya matundu ya vyoo ni 2,009, yaliyopo ni 864 pekee, na upungufu ni matundu 1,145.

"Kwa mujibu wa mwongozo wa elimu, uwiano unaotakiwa ni tundu moja la choo kwa wasichana 20, na tundu moja kwa wavulana 25. hivyo kwa idadi ya wanafunzi tulionao ndiyo maana kuna upungufu mkubwa wa matundu ya vyoo," anasema Mwakiluma.

Anafafanua kuwa, upungufu huo wa matundu ya vyoo, umechangia pia ukosefu wa vyumba maalumu vya kujistiri wakati wa hedhi katika shule nyingi.

"Vyoo vingi vya shule vilijengwa kabla ya kuwapo kwa mwongozo unaotaka kujengwa kwa chumba maalumu cha kujistiri wakati wa hedhi, ndiyo maana shule nyingi hazina miundombinu hiyo," anaongeza Mwakiluma.

Anasema, halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga imeshachukua hatua kukabiliana na tatizo hilo, kwamba kila mwaka wa fedha, hutenga bajeti kwa ajili ya kujenga matundu mapya ya vyoo na vyumba vya kujistiri na hedhi, hasa katika shule zenye upungufu mkubwa

Anasema katika mwaka wa fedha 2026/2027, Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga imetenga sh. milioni 118.8 kwa ajili ya ujenzi wa matundu 54 ya vyoo, yatakayoambatana na vyumba maalumu vya kujistiri wakati wa hedhi katika shule zenye changamoto kubwa zaidi.


Na Marco Maduhu, SHINYANGA
Makala imeandaliwa na Mwandishi anayeshiriki katika programu maalum ya kukuza uandishi wa maslahi kwa umma (Public Interest Journalism Fellowship) inayoratibiwa na UTPC kwa kushirikiana na IMS.
 
Hivi ujenzi wa vyoo vya shule ya msingi nao unasubiri maagizo kutoka kwa Waziri mkuu?
HII NCHI NI NGUMU SANA!
 
Back
Top Bottom