Ona kilichowapata Watanzania mgodi ambao Dr. Kikwete aliweka sahihi.
Baesi: Sitasahau yaliyonikuta Bulyanhulu
Asha Bani
IKIWA ni miaka 12 tangu kutokea vifo vya wachimbaji wadogowadogo wa madini katika mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu, mkoani Shinyanga, bado wingu zito limetanda. Kutanda kwa wingu hilo kunatokana na matukio mbalimbali ambayo kwa baadhi ya wanajamii wanaoishi karibu na mgodi huo, bado wanatokwa na majonzi ya kupotelewa na ndugu zao.
HIVI karibuni, madhehebu mbalimbali ya dini yaliamua kufanya ziara ya kutembelea baadhi ya vijiji vilivyoathirika na tukio, kujionea hali halisi iliyopo kwa zaidi ya miaka 12 sasa.
Miongoni mwa madhehebu hayo ni pamoja na Baraza la Kuu Waislamu Tanzania (Bakwata), Kanisa Katoliki, Anglikana, Shirika la Misaada la Makanisa ya Norway, Wanasheria wa Mazingira (LEAT), na taasisi nyingine.
Sababu kubwa ya madhehebu kutembelea eneno hili ilikuwa kuona maisha ya wachimbaji wadogo na kuendesha utafiti juu ya faida ya madini yanayozaliwa, sanjari na matatizo yaliyotokea mwaka 1996 na kusababisha vifo vya watu 52.
Lakini pamoja na viongozi hao wa dini kukumbuka tukio hilo, walikutana na mmoja wa akina mama muathirika wa tukio hilo, Melania Baesi. Mama huyo anasema katika tukio hilo alipoteza wanawe wawili, kwa kile anachodai kwamba walifukiwa na kifusi kwenye mashimo makubwa yaliyoko kwenye mgodi huo.
Katika mahojiano na Tanzania Daima hivi karibuni, mama huyo alianza kwa kusema: "Nina wasiwasi kama utaweza kuandika ninachokueleza kwa sababu kama umetoka serikalini itakuwa vigumu".
Amekuwa akipata wakati mgumu wa kuzungumza na viongozi wa serikali kwa vile wameshindwa kumtekelezea malalamiko kwa kipindi chote hicho.
"Napata wakati mgumu kueleza kilio changu kwani sasa ni muda mrefu sioni kama natekelezewa, tangu haya yametokea sijawahi kulipwa fidia, nimepoteza familia yangu, nimeyumbishwa kimaisha sasa sijui nitakimbilia wapi," anasema Baesi.
Kinachomsumbia kichwa hadi leo ni kuona tume mbili zilizoundwa chini ya Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, na moja iliyoundwa na Jakaya Kikwete kuchunguza suala hilo hazikuweza kutoa majibu sahihi.
"Nasema kutokana na yote niliyofanyiwa na serikali yangu kamwe siwezi kuzungumza kutokana na kukosa imani na serikali yangu na njia pekee labda nikutane na rais mwenyewe," anasema Baesi.
Huku akibubujikwa machozi, Baesi anasema Septemba 1996, wakati akijishughulisha na uchimbaji mdogo mdogo wa madini kwenye mgodi wa Bulyanhulu na watoto wake watatu, kulitolewa na taarifa na Mkuu wa Mkoa Shinyanga wakati huo, Jenerali Tumainiel Kiwelu aliwataka wananchi wanaozunguka mgodi huo kuhama ili kupisha wawekezaji.
Anasema baada ya kupata taarifa ya kuondolewa kwao, akiwa miongoni mwa familia za watu zaidi ya 300, ilimwia vigumu kukubalina na suala hilo kwa kuwa yeye alikuwa pale muda mrefu na ni wazawa wa maeneo hayo.
"Tuligoma kuondoka eneo lile kwa sababu ya kudai malipo ya fidia kwa ajili ya kuhama, lakini baadae tukasikia kwenye redio kwamba tumepewa siku 30 kwa ajili ya kujiandaa kuhama...tulipata mshutuko mkubwa na hatua na namna yoyote," anasema Baesi.
"Tuligoma kuondoka lakini nguvu za ziada zilitumika na askari hao waliingia nyumba hadi nyumba na kutuharibia mali zetu zilizokuwemo ndani huku wakitutaka kuondoka mara moja," anasema Baesi.
Kutokana na hali hiyo, walilazimika kukimbilia msituni kwa lengo la kuokoa maisha yao kwa vile hawakutegemea nini kingetokea usiku huo.
"Nasema hayo yote yalinikuta naweza kuyasahau lakini kikubwa ambacho siwezi kukisahau ni siku niliyoshinda nikiwasubiri wangu - Ernest na John Rwekama - lakini hawakutokea hadi leo hii," anasema Baesi.
Baada ya kuasubiri, siku iliyofuata alipokea taarifa kuwa kuna wachimbaji wa madini wadogowadogo waliokuwa wakiendelea na shughuli zao wamefukiwa na chini ya migodi na kupoteza maisha.
"Sikuamini kama katika hao waliyopoteza maisha siku kama wanangu walikuwa miongoni mwao, lakini baada ya kupita siku mbili ndipo niliamini...nimewaza hadi nimekata tamaa,"anasema Baesi.
Baada viongozi wa juu kuona vyombo vya habari vimelalamikia na kuandika vifo hivyo, Rais wa awamu ya tatu, Mkapa, aliunda tume mbili na kwenda kuchunguza tukio hilo.
Tume zilizoundwa hakuna hata moja iliyopeleka majibu ya ukweli kwa rais, jambo ambalo limesababisha hadi sasa hakuna hatua zilizochukuliwa dhidi ya wahusika.
Mikasa ya watu kwenda kumhoji ilikuwa ni ya mara kwa mara. Anakumbuka siku moja alikwenda mtu mmoja (hakumbuki jina), alijitambulisha kuwa ni Rais wa Kanisa la Misaada la Norway na kumtaka aelezee mkasa wa Bulyanhulu.
"Nilimweleza kwa kina juu ya tukio hili lote huku akichukua mkanda wa video na kuongeaza jambo lililosaidia watu mbalimbali kuchukua mikanda hiyo, lakini sijaona manufaa yake hadi leo," anasema Baesi.
Mwanasiasa pekee aliyeamua kuzungumza ukweli wa tukio ni Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Augustine Mrema, na mwanasheria maarufu Tundu Lisu aliyewasaidia kufungua kesi mahakamani.
"Tena nashangaa kesi hiyo kusikia imefutwa hadi mikanda ya video haipo, tena hadi askari wakiwa wanahamisha watu kwa kutumia bunduki ipo, sijui kwa nini Mrema ameshindwa kuishitaki serikali huku jambo likiwa ni ukweli mtupu!"
Beasi amebakiwa na familia ya watoto wanne. Mmoja kati ya hao bado anajishughulisha na uchimbaji madini. Anawataja wengine kuwa ni David, Denis, Method na Mushobozi.
"Naiomba serikali isikie kilio changu kwa vile kipato changu nilitegemea sana matumizi kutoka kwa wanangu...lakini sasa natabika mno," anamalizia.
ashabani48@yahoo.com
From:
Makala -Baesi: Sitasahau yaliyonikuta Bulyanhulu
Aombe basi walau msamaha yeye na Che Nkapa wake.