HII NI PAMOJA NA KUONGEZA MAZINGIRA YA AJIRA NA PIA UFANISI KATIKA KAZI. MAISHA BORA KWA KILA MTANZANIA YANAWEZEKANA...
Mishahara minono bajeti ijayo-Kikwete
2007-04-29 10:05:09
Na Godfrey Monyo
SOURCE NIPASHE
Watumishi Serikalini kuchekelea bajeti ijayo, kwa kuongezewa mishahara, kwa mujibu wa kauli ya Rais Jakaya Kikwete Jijini Dar es Salaam jana.
Rais Kikwete, katika utekelezaji wa dhati wa ahadi zake, amewahakikishia walimu pamoja na watumishi wengine wa serikali kwamba, wataongezwa mishahara yao katika bajeti ijayo na itaendelea kuongezeka katika kila bajeti na kuboresha mazingira yao ya kufanyia kazi.
``Suala la mishahara katika bajeti ijayo, itaongezeka na itaendelea kuongezeka kila bajeti na tutaendelea kuboresha mazingira yenu ya kufanyia kazi, pamoja na ya watumishi wote,`` alisema Rais Kikwete.
Alitoa ufafanuzi huo jana alipokuwa akifungua jengo la kisasa la Kitega Uchumi `Mwalimu House` ambalo limejengwa na kumilikiwa na walimu nchini.
Jengo hilo lenye thamani ya Sh. bilioni 5.7, liko katika Manispaa ya Ilala, Jijini Dar es Salaam.
Alisema nia ya Serikali ni kuongeza mishahara ya watumishi wake na kwamba itaendelea kuongeza kwa kadri mapato ya serikali yatakavyokuwa yakiongezeka.
Rais Kikwete alisema wakati serikali inaendelea kuongeza mishahara hiyo, pia itakuwa ikiendelea kujenga mazingira mazuri ya kazi na yale ya kufundishia kwa walimu na watumishi wote wa serikali.
Hata hivyo, Rais Kikwete alisema, serikali ililazimika kuondoa posho kwa watumishi wa umma, ikiwamo ya kufundishia kwa walimu na kuziingiza kwenye mishahara ili kuwawezesha watumishi kupata mafao mazuri pale wanapostaafu.
``Hili la posho naomba nilisema hivi, ingawa halitawapendeza sana. Serikali katika miaka ya 1995/96, iliamua kuzifuta posho zote pamoja na hii ya kufundishia, baada ya kugundua kwamba wafanyakazi walikuwa wakiishi maisha mazuri kwa kupata posho hizo, lakini walikuwa wanapata mafao duni baada ya kustaafu kwa kuwa posho hizo hazikuwa zinaingizwa kwenye mishahara,`` alisema Rais Kikwete.
Aliongeza kuwa, kutokana na hali hiyo, ndipo ilipopendekezwa kwamba posho hizo ziwe sehemu ya mishahara ili kutunisha mafao ya kustaafu hatimaye mtumishi awe na maisha mazuri baada ya ajira yake kumalizika.
Rais Kikwete alilazimika kutoa ufafanuzi huo baada ya baadhi ya walimu waliohudhuria sherehe hizo, kumuomba kupitia nyimbo na ngonjera walizoimba, aangalie uwezekano wa kuwarejeshea posho ya kufundisha.
Kuhusu jengo hilo la kisasa ambalo linamilikiwa kwa asilimia 100 na walimu, Rais alisema kukamilika kwa mradi huo ni kielelezo cha heshima waliyonayo walimu kupitia kazi yao ya ualimu.
``Naamini uzuri wa jengo hili ni kielelezo cha wazi cha kazi nzuri mnayoifanya ninyi walimu hapa nchini mwetu na sote tunatambua kuwa kazi ya ualimu ni ya heshima na jasho...hili mlilolijenga kwa nguvu zenu linadhihirisha heshima hiyo, alisema na kuwapongeza.
Alisema uamuzi wa walimu kuwa na kitega uchumi chao ambacho wamekijenga kwa jasho lao na kukimiliki wenyewe, ni mfano unaotakiwa kuigwa na vyama vingine kwa kuwa ni kielelezo kizuri cha matumizi ya fedha na raslimali za wanachama wake.
Rais aliwataka walimu nchini kupitia chama chao, kuendeleza mipango mizuri ya matumizi ya fedha za wanachama wao na zitakazotokana na kitega uchumi hicho kwa kutunisha mitaji ya vyama vyao vya kuweka na kukopa.
Alibainisha kuwa, uamuzi huo kama utatekelezwa vizuri utasaidia sana katika kuongeza kipato cha walimu na kuboresha hali ya maisha yao kwa kipindi hiki na kwa siku za usoni.
Hata hivyo, aliwashauri walimu kujipa muda na kutafakari kwa kina mpango wao wa kutaka kuanzisha Benki ya Ushirika ya Walimu.
``Wazo la kuwa na Benki yenu ya Ushirika ni zuri, lakini naamini linahitaji kufanyiwa kazi zaidi kwa kuwashirikisha wanachama wote na kupata ushauri wa kina kutoka kwa wataalam wa mambo hayo, halitakuwa jambo jema kuanzisha mradi ambao hatimaye utawashinda kuendesha au mkapata hasara,``alisema Rais Kikwete.
Akitoa taarifa fupi ya ujenzi wa kitega uchumi hicho, Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu, Bw Yahya Msulwa, alisema jengo hilo halikuweza kukabidhiwa kwa CWT mwaka jana baada ya kupewa ushauri wa kulifanya liwe la kisasa zaidi.
Alisema hadi sasa, asilimia 70 ya jengo hilo limepangishwa huku mteja mkubwa akiwa ni benki ya NMB.
Alifafanua kuwa, mtaji wa ujenzi wa jengo hilo ni michango ya kila mwezi ya walimu na unatarajiwa kurejeshwa katika kipindi cha miaka 10.
Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Bi. Margaret Sitta ambaye katika salamu zake aliwataka walimu kumpa muda Rais Kikwete kuzishughulikia kero zao mbalimbali.