Agenda iliyombele yetu ni uhusiano wa ongezeko la ajira zilizotajwa na Mhe. Rais kwenye hotuba yake ya juzi na hali mbaya ya uchumi (economic recession) ya nchi yetu na dunia kwa ujumla.
Kwanza kabisa nianze na kuelezea aina mbalimbali za ajira ambazo nchi inaweza kuona zinapatikana nchini kwa kipindi fulani kilichohusishwa katika utafiti au mjadala:
1. Ajira binafsi: Ajira hizi hutokea pale ambapo serikali hutengeneza mazingira mazuri ndani ya nchi kwa watu wake hasa wajasliamali (Entrepreneurs) hujiajiri wenyewe. Hili linawezekana pale ambapo kwa mfano mitaji na masoko ya bidhaa fulani itakuwa rahisi kupatikana kama matunda ya kazi ya Serikali husika kuweka miundombinu mizuri kwa uchumi wake kufanya kazi kwa ufanisi na kujitoshereza (kuwepo kwa taasisi za kifedha na miundombinu mingine muhimu kwa watu binafsi kuwekeza. Lingine katika hilo, ni kuwawezesha wananchi walio wengi kuwa na kipato cha juu kiasi cha kuwa na uwezo wa kununua bidhaa ndani ya nchi yao zizalishwazo na wajasiliamali (entrepreneurs).
2. Ajira za Sekta binafsi: Hapa ni pale mashirika ya kitaifa na kimataifa ndani na nje ya nchi yanapoweza kutoa ajira wa jamii yetu (Tanzania). Mfano ni pale ambapo mashirika kama TIGO, VodaCom, TBL, n.k kupitia ama FDI (Foreign Direct Investment) au mitaji wa wananchi wetu, huweza kuwekeza kwenye viwanda na mashirika ya kutoa huduma. Haya mashirika huweza kuajiri watanzania kwa asilimia kubwa (kwa mjibu wa Sera ya Ajira ya nchi yetu). Lakini kutokana na hali ya uchumi wa dunia kuwa mbaya, tuliona mashirika ya kimataifa kama mdau hapo juu alivyosema hujaribu kujiendesha kwa kupunguza gharama. Ikiwezekana kupunguza hata waajiriwa wake (employees lay-off). Hivyo kuna uwezekano mkubwa tu kwamba ajira zilipungua kwa kigezo hicho kwenye makampuni yenye mitaji ya FDI;
Kipengele kingine ambacho kinaweza kuwa ni kikwazo kwa ajira nchini Tanzania hasa hizi za FDI ni kipato kidogo kwa wananchi wetu, maana soko sasa linakuwa funyu kuweza kununua bidhaa zizalishwazo na makampuni hayo yaliyowekeza kwa mfumo wa FDI (market seeking FDI). Tanzania tunategemea zaidi FDI zinazokuja kutafuta maeneo na mali ghafi kama vile kwenye madini, vinginevyo hatujajenga mazingira ya kuwavutia wawekezaji kutoka nje waje kuwekeza nchini kwetu kwa kutegemea kuuza ndani ya nchi. Hivyo, Serikali ifanye bidii kuongeza kipato cha watu wake ndipo ajira nyingi zitapatikanaj;
3. Ajira za Sekta za Kiserikali: Hapa ni ajira ambazo Serikali yenyewe huajiri watanzania kulingana na hitaji, ili kuweza kutekeleza kwa urahisi majukumu yake ya kukuza uchumi. Hapa naomba niandike zaidi maana ndipo hapo tulipo na matatizo makubwa yanayotufanya tubaki nyuma siku hadi siku katika kukuza uchumi wetu. Serikali ya Tanzania, huajiri watumishi wapya bila kufanya uchambuzi wowote wa kisayansi kwamba tunahitaji waajiriwa wangapi na fani gani ili kuongeza tija (productivity) ya sekta mbalimbali nchini? Kwa sababu Rais aliahidi ajira kwa kipindi cha miaka minne watu wameajiriwa tu kwa agizo la Ikulu kwamba kila Halmashauri lazima iajiri watu kadhaa, Wizara lazima iajiri watu kadhaa ili hesabu ya idadi ya ajira milioni moja ifikiwe kabla ya uchaguzi wa 2010. Hii ni kweli na nina ushahidi juu ya hili. Ilitokea watumishi fulani ndani ya Serikali waliajiriwa 2009, walipowasili kuanza kazi Wakurugenzi wa Idara waliwakataa maana kwanza hawakuwa na taarifa za ajira hizo, Pili hawakuwa na hitaji la watu hao kuingia kwenye idara zao. Kwa sababu ni agizo la wakubwa, waajiriwa hao waliweza kupokelewa na kuwa waajiriwa wa kudumu wa Serikali.
Madhara ya hatua hiyo ni kuongeza matumizi kupita kiasi cha kawaida na ndiyo maana tunaona sasa mfumko wa bei ulipanda kwa kasi sana tangu JK alipoingia madarakani. Mfumko wa bei ulitoka namba 1 ya asilimia hadi kufikia namba 2 za asilimia kama (18%, 2009), sikumbuki vizuri.
Kiwango cha ukosefu wa ajira (unemployment) katika nchi yeyote ile hauwezi kuondolewa kwa 100%, bali hulinganishwa na kiwango cha mfumko wa bei nchini (nchi yeyote) kwamba kuna kiwango tu kinachoruhusiwa kupunguza ukosefu wa ajira (unemployment), katika kiwango fulani cha mfumko wa bei (inflation). Kama kiwango fulani kati ya viashiria hivyo vya uchumi itakiukwa kupita kiasi, basi hali ya uchumi nchini huharibika hata kama Serikali itafanya marekebisha kwa muda mrefu (Phillip Curve) inaeleza uhusiano huo kuwa huwa wa kutengana (inverse relationship between inflation and unemployment). Tanzania imeajiri kupita kiwango kinachotakiwa kiwe kwa kawaida hivyo kuurudisha nyuma mfumko wa bei (inflation) itakuwa kazi ya kutoa jasho. Tunatumia kingi zaidi kuzalisha kidogo ambacho haturudishi hata gharama za uzalishaji (mishahara). Tanzania hatuzalishi kwa kuongeza tija (there is no productivity among employees). Kila mwajiriwa anafanya kazi na kuzalisha chini ya hitaji ndani ya masaa aliyojihusisha kufanya kazi hiyo (kazi ndogo na yenye matokeo madogo inafanywa na watu wengi kuliko kawaida). Hivyo hatuwatumii wataalamu wetu ipasavyo, ndiyo maana utakuta mtumishi wa Serikali siku hizi anaweza kuwa na muda wa ziada kufanya mambo yake hata kama ni wakati wa masaa ya kazi ya mwajiri wake.
Hivyo, uchumi umeshuka maana uzalishaji umeshuka ukilinganisha na gharama za uzalishaji husika. Hivyo kipato cha Taifa kitaendelea kudumaa kwa sababu ya Sera mbovu zilizotawaliwa na msukumo wa Kisiasa zaidi kuliko kitaalamu.
Haya ni machache tu ambayo naweza kuelezea kuhusiana na thread ya M. M. Mwanakijiji.