HOJA Ahadi ya mkopo wa Tsh. Bilioni 2 kwa watengeneza maudhui(Content Creators), tutasubiri hadi lini? Hakuna mrejesho

HOJA Ahadi ya mkopo wa Tsh. Bilioni 2 kwa watengeneza maudhui(Content Creators), tutasubiri hadi lini? Hakuna mrejesho

Hoja ya Mdau inayopendekeza maboresho au mabadiliko ndani ya jamii, inayotakiwa kuangakiwa kwa mapana na Mamlaka husika
A

Anonymous

Guest
Mapema mwezi Januari 2026, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, alisema Wizara ilipatiwa kiasi cha Shilingi bilioni 2 ambacho kingewawezesha watengenezaji wa maudhui mbalimbali mitandaoni kuimarisha kazi zao na kuongeza kipato kupitia majukwaa ya kidijitali.

Makonda alisema hayo Januari 29, 2026, jijini Dodoma, na kubainisha kuwa fedha hizo zilitolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kuyawezesha makundi mbalimbali ya watengenezaji wa maudhui, yakiwemo yanayojihusisha na sekta za Utalii, Michezo, Habari, Jamii, Muziki, Filamu na sanaa nyinginezo.

Awali, mkopo huo ulitarajiwa kuanza kutolewa Aprili 18, 2026, baada ya kukamilika kwa zoezi la kujiandikisha na kuchambua wanufaika.

Zoezi la uandikishaji wa walengwa lilianza rasmi Januari 30 hadi Februari 15, 2026, ambapo watengenezaji wa maudhui walitakiwa kufika katika ofisi za Halmashauri za Wilaya, Manispaa na Majiji kupitia vitengo vya habari, ili kuchukua na kujaza fomu za maombi zilizokuwa zikihitaji taarifa binafsi pamoja na maelezo kuhusu shughuli wanazozifanya.

Hata hivyo, utekelezaji wa utoaji wa mkopo huo uliahirishwa kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kuhakikisha unatekeleza kikamilifu maelekezo ya Rais, baada ya kubainika kuwa kulikuwa na tofauti katika sifa za waombaji. Aidha, ilielezwa kuwa uamuzi huo ulihusishwa pia na viwango vya riba vilivyoonekana kuwa vikubwa na ambavyo vingekuwa mzigo kwa walengwa.

“Lengo la Rais ni kuwawezesha vijana wanaohustle katika maisha yao ya kila siku. Hatuwezi kuweka riba kubwa na masharti ya dhamana (collateral) ambayo yatawazuia vijana wa hali ya chini kupata mkopo huu,” alisema Makonda.

Lakini hadi sasa, takribani miezi sita imepita tangu zoezi la uandikishaji wa walengwa kukamilika na kutolewa taarifa ya kusitisha ili kuweka taratibu rafiki, lakini bado hakuna dalili zinazoonekana za fedha hizo kutolewa kwa walengwa kama ilivyotarajiwa.

Kwa wengi tuliojitokeza kuwasilisha taarifa zetu, mpango huo ulikuwa na matumaini makubwa ya kutusaidia kukuza shughuli zetu, kuongeza kipato na kujijenga kiuchumi. Baadhi yetu tulitumia muda na rasilimali katika kufuata taratibu zilizoelekezwa na Wizara, tukiamini kuwa baada ya zoezi hilo tungepata mrejesho na hatua inayofuata ya utekelezaji.

Sasa, swali tunalojiuliza fedha hizo zitatolewa lini, na ni lini walengwa watapewa taarifa rasmi kuhusu hatua iliyofikiwa? Au mpango umeyeyuka.

Tunaomba Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kutoa ufafanuzi kuhusu lini itakamilisha mwongozo ambao ilieleza kuwa unaandaliwa ili kuhakikisha fedha hizo zinawanufaisha walengwa waliokusudiwa.

Aidha, ni muhimu Wizara kutoa mrejesho kwa waombaji na hatua iliyofikiwa tangu walipotoa taarifa ya mwisho. Izingatiwe wananchi tuliwasilisha taarifa zetu kwa kufuata taratibu tulizoelekezwa, hivyo tunayo haki ya kufahamu mchakato umefikia wapi na tunapaswa kutarajia nini.

Hoja yangu hapa si kupinga uamuzi wa Serikali wa kufanya maboresho katika utaratibu wa utoaji wa mkopo huo, bali ni kuomba uwajibikaji, uwazi na mrejesho rasmi kwa watu ambao walipewa matumaini na kuhamasishwa kushiriki katika mchakato huo.

Ikiwa kuna changamoto zinazochelewesha utoaji wa fedha hizo, ni muhimu wananchi na walengwa kuambiwa wazi changamoto hizo ni zipi, zimefikia hatua gani katika kutatuliwa na ni lini wanatarajiwa kuona utekelezaji wa mpango huo.

Uwazi na mrejesho wa wakati ni sehemu muhimu ya uwajibikaji wa taasisi za umma, hasa pale ambapo wananchi wameombwa kutoa taarifa zao na kushiriki katika mchakato unaoahidi kuwawezesha kiuchumi.
 
Poleni sana, Mungu awafanikishe katika hustle zenu. Mungu jalia
 
Back
Top Bottom