Akijibu madai hayo, Reli alisema nafasi ambazo Wazanzibari wanaweza kupewa zisizokuwa na ushindani wa sifa ni zile za kupika chai, ulinzi na udereva, lakini nafasi nyengine zote za kitaalamu zinatakiwa kuombwa na watu wenye sifa na hakuna nafasi maalumu zilizotengwa kwa ajili ya Wazanzibari.
"Waheshimiwa wajumbe nafasi za ajira ya kupika chai, ulinzi na udereva hizi Wazanzibari wanaweza kuzifanya na ni zao hatuna sababu ya kumchukua mpika chai au mlinzi ama dereva kutoka Tanzania Bara, lakini zile za kitaalamu kama uhasibu, IT na nyinginezo, hizo ni lazima watu waombe na kushindaniwa na Watanzania wote wenye sifa," alisema Naibu Gavana.
Majibu hayo yaliwachukiza karibu wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi ambao wasisitiza kwamba Zanzibar wapo watu wenye sifa ambao wanaweza kufanya kazi za kitaalamu.
Hata hivyo, mjumbe wa Kamati ya Fedha na Uchumi wa Baraza la Wawakilishi, Salmin Awadh Salmin alikiri kuwa ni kweli vijana wengi wa Zanzibar hawana sifa za kuwawezesha kuajiriwa katika kazi za kitaalamu BoT.