Aina za fimbo

Aina za fimbo

Frumence M Kyauke

JF-Expert Member
Joined
Aug 30, 2021
Posts
630
Reaction score
1,262
AINA ZA FIMBO
By
Frumence M Kyauke

Fimbo ni kijiti kirefu ambacho kinatumika kwa namna nyingi ili kufikia mbali kuliko mkono wa mtu. Kwa mfano fimbo hutumika kuua nyoka au kutoa adhabu kwa kuchapa mtoto kutokana na kosa fulani.
Hizi ni aina za fimbo na matumizi yake:

Mpapure
Fimbo ya kungwi ya kuchapia mwari aliyeshindwa kufumbua fumbo la unyangoni.

Mtobwe
Fimbo nyembamba yenye kuweza kupindwa.

Ubati
Fimbo nyembamba ya kuchapia kama vile watoto.

Mkongojo
Fimbo ndefu inayotumiwa na wazee au wagonjwa kuwasaidia kutembea.

Mkosha
Fimbo maalumu ya kuwaswagia ng'ombe.

Asa
Fimbo inayotumiwa na viongozi kama ishara ya mamlaka.

Ndoaro
Fimbo yenye kirungu kilichopinda kama ile ya kuchezea gofu.

Ndongoa
Fimbo yenye fundo la mviringo kwenye upande wake mmoja.

Kigoe/ugoe /upembo/kiopoo
Fimbo yenye panda nchani inayoelekea chini, inayotumiwa kuinamisha tawi la mti ili kuchuma matunda pia hutumiwa kuchezea gofu.

Rungu
Fimbo yenye kivimbe upande mmoja na aghalabu huwa mviringo na ndilo upande unaotumiwa kwa kupiga.

Kirungu
Fimbo ndogo yenye nundu upande mmoja itumiwayo na askari polisi.

Kimangare
Kirungu kinachotumiwa sana na Wamaasai hasa Wakwavi.

Wenzo
Fimbo au gongo kinachotumiwa kuinulia vitu ambavyo ni vizito.

Gongo
Fimbo nene.

Bakora
Fimbo ya kutembelea ambayo sehemu yake ya kushikia imepindika.

Kibarango
Fimbo fupi na nene.

Siwa
Fimbo maalumu anayobeba mlau wakati wa maandamano ya wataalamu katika mahafali ya chuo kikuu.

Kiboko
Mjeledi uliotengezwa kwa ngozi ya kiboko, faru au mkia wa taa; fimbo yoyote ya kuchapia.

Ukonzo
Fimbo uliochongwa yenye ncha au chembe ya chuma ambayo hutumiwa kuchokolea samaki.

Uloo
Fimbo ya chuma ambayo mwishoni ina kipindo kama ndoana ambayo hutumiwa na wavuvi kuvulia samaki wakubwa katika maji ili kuwapakia kwenye chombo.

Upongoo
Fimbo yoyote ile aghalabu ya mnazi itumiwayo kwa kusikia makuti.

Cheo
Kifimbo cha chuma, shaba au pembe anayotumia mganga kupungia wagonjwa au kutafutia vitu vilivyopotea.

Fido
Kifimbo cha kupigia ramli.

Mkwiro
Kigongo cha kupigia ngoma.

Mjeledi
Kitu kinachonepa kama vile kiboko cha kuchapia.

Kipigi
Fimbo ndogo ya kupiga au kuangalia matunda.

images - 2021-10-28T094408.948.jpeg
 
Back
Top Bottom