IGP abeba zigo la Dk. Mwakyembe
SIKU nne tangu Mbunge wa Kyela, Dk. Harisson Mwakyembe (CCM) kulishutumu Jeshi la Polisi kwa kuliambia kuwa linafanya kazi chini ya kiwango na kukosa umakini, kutokana na ripoti iliyotolewa kuhusu ajali yake, kuna taarifa jeshi hilo limeamua kupitia upya ripoti hiyo na kuchukua maelezo yake.
Uamuzi huyo unasemekana umefikiwa ili kumaliza utata na malumbano yaliyoanza kushamiri mara baada ya kamati iliyoundwa na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Said Mwema kuchunguza chanzo cha ajali hiyo, kutoa ripoti kuwa ilisababishwa na uzembe na mwendo kasi wa dereva wa mbunge huyo, Joseph Msuya.
Awali, kabla ya kutangazwa kwa ripoti hiyo, Dk. Mwakyembe akiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alielezea mazingira ya ajali hiyo na kudai kuwa kulikuwa na lori mbele yao na ndilo lililosababisha ajali na kusema kwamba mbinu zilizotumika na dereva wa lori hilo kutengeneza ajali hiyo ni za hali ya juu ambazo amekuwa akiziona kwenye sinema.
Lakini maelezo hayo yalikanushwa vikali na ripoti ya kamati iliyokuwa ikiongozwa na Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, James Kombe ambayo ilienda mkoani Iringa eneo ilipotokea ajali hiyo na kufanya uchunguzi.
Ripoti ya kamati hiyo, ilisema kuwa mbunge huyo hapaswi kusema mambo asiyojua kwa kuwa kabla ya ajali kutokea alikuwa amelala hivyo haelewi chanzo cha ajali hiyo.
Akizungumza na Tanzania Daima, kwa niaba ya IGP Mwema, msaidizi wake, Hamis Juma, alisema kuwa kutokana na taarifa hizo mbili; ya Mwakyembe na Kamati ya Kombe kutofautiana, sasa jeshi hilo limeamua kuzipitia upya.
Hamis ambaye alisema IGP Mwema hasingeweza kuzungumza na Tanzania Daima, kwa siku ya jana kwa kuwa yupo katika mapumziko, alibainisha kuwa baada ya kukamilisha upitiaji wa ripoti hizo, majibu yake yatatolewa hadharani ili jamii iweze kujua undani wa suala hilo.
Msaidizi huyo alisema, ili kumaliza mkanganyiko wa taarifa zilizoanza kutolewa katika jamii, Jeshi la Polisi limechukua ripoti ya kamati yake na ile taarifa iliyotolewa na Mwakyembe kupinga kile kilichoelezwa na kamati hiyo.
"Siwezi kukuambia msimamo wa IGP kuhusu suala hilo, lakini ndani ya siku mbili tutatoa taarifa rasmi, na ni vema mkumbuke kuwa wakati ripoti ile inatolewa, Mwema alikuwa nje ya nchi," alisema Hamis.
Taarifa ambazo Tanzania Daima ilizipata kutoka katika chanzo kimoja cha habari zilisema kuwa, IGP Mwema alienda kumjulia hali Mwakyembe nyumbani kwake Kunduchi Mtongani, jijini Dar es Salaam, na kumuahidi kuwa atalifanyia kazi suala hilo.
Chanzo hicho kilizidi kupasha kuwa, IGP hakuweza kuiona taarifa ya ripoti hiyo kabla ya kutolewa, kwa kuwa alikuwa nje ya nchi ingawa yeye ndiye aliyeunda kamati hiyo, lakini hata hivyo aaliahidi kuwa, tayafanyia kazi madai hayo katika kipindi kifupi.
"IGP alikwenda kumuona Dk. Mwakyembe na kumuahidi kuwa atafanyia kazi sakata hili ili kutatua utata unaonekana kuanza kushamiri, hasa baada ya kutolewa kwa ripoti ya Kamati Maalum aliyoiunda," kilisema chanzo hicho.
Hata hivyo, msaidizi wa IGP Mwema alikataa kuzungumzia kukutana huko kwa bosi wake na Mwakyembe.
"Siwezi kuzungumzia suala la IGP kukutana na Dk. Mwakyembe, muulizeni vizuri aliyewaambia au kama mnaweza mnaweza kumuuliza IGP kesho," alisema Hamza.
Tanzania Daima iliwasiliana na Mwakyembe kwa njia ya simu ambapo alisema hawezi kuzungumza kwa kuwa hasikii sauti ya upande wa pili kutokana na kelele zilizopo nyumbani kwake, hasa katika kipindi hiki anachoumwa.
Alisema kumekuwa na idadi kubwa ya wageni wanaokwenda kumjulia hali, akalitaka gazeti hili kumuandikia ujumbe mfupi wa maneno (SMS).
"…Haloo nani mwenzangu? Unasemaje? Siwezi kukusikia vizuri kwa kuwa hapa kuna kelele, itakuwa vizuri kama utanitumia message," alisema Dk. Mwakyembe na kukata simu.
Hata hivyo, Tanzania Daima ilipomuandikia SMS mbunge huyo hakuweza kujibu mpaka tunakwenda mitamboni.
Dk. Mwakyembe ambaye alijipatia umaarufu mara baada ya kuwasilisha ripoti ya kamati teule ya Bunge iliyoundwa kuchunguza uhalali wa zabuni iliyoipa ushindi Kampuni ya Richmond Development ambapo ilibaini kuwapo kwa mazingira ya rushwa wakati wa utoaji wa zabuni hiyo, aliikosoa taarifa ya Kamati ya Kombe na kusema kuwa kamati hiyo ilifanya kazi kama wapiga ramli.
Katika ukosoaji huo, alitumia maneno na vifungu mbalimbali vya sheria ambapo alisema kuwa, uamuzi wa kamati hiyo kutaka dereva wake akamatwe na kushitakiwa, ni sawa na kumuhukumu mapema (pre-judge) kuwa ni mwongo na mzembe.
"Uamuzi huo hauendani na utawala na misingi ya haki inayolindwa na katiba, na unaigeuza mahakama kuwa ni chombo cha kupiga muhuri (rubber-stamp) maamuzi ya polisi," alisema Mwakyembe.
Alisisitiza ukweli kuwa, ripoti hiyo imedanganya na kwamba hakuwa amelala kutokana na safari yake hiyo ilikuwa imeanzia Makambako alipokuwa amelala, hivyo si kweli kwamba alikuwa katika usingizi kabla na baada ya ajali hiyo kutokea.
Aidha, alisema kuwa hakutendewa haki kwa mujibu wa kanuni za haki za asili na kuhoji kuwa, kuna kitu gani kilichozuia kumhoji yeye na dereva wake ili kukidhi matakwa ya kanuni hiyo na kupata picha iliyo kamilifu zaidi.
"Laiti mimi na dereva wangu tungelisikilizwa, nina uhakika kuwa taarifa ya kamati hiyo maalum isingelisomwa kuchelea kulidhalilisha Jeshi la Polisi kwa kukosa umakini na viwango," alisema Mwakyembe.
Wakati huo huo, watu 12 wamekatwa na Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro kwa tuhuma za kupanga mawe barabarani kwa lengo la kutaka kumteka Mbunge wa Vunjo, Aloyce Kimaro (CCM) akiwa na familia yake pamoja na na rafiki yake Joseph Temu aliyekuwa akiendesha gari aina ya Mercedes Benz.
Ajali hiyo ilitokea juzi katika Kijiji cha Mikongeni, Kata ya Lembeni wilayani Mwanga ambapo inadaiwa kuwa mbunge huyo na rafiki yake walikuta mawe yamepangwa katikati ya barabara katika eneo lenye kona jambo lililosababisha gari hilo kuyagonga na kuharibika.
Baada ya kupata ajali hiyo, Kimaro na wenzake walipata msaada wa kuvutwa na gari kubwa kuelekea sehemu salama na walipiga simu polisi ambao walikwenda eneo la tukio na kukuta mawe hayo yameondolewa.
Kwa mujibu wa chanzo kimoja cha habari, vijana hao wanashilikiwa na polisi kwa uchunguzi zaidi na wakionekana kutenda kosa hilo watafikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Source:Tanzania Daima.